NA DERICK MILTON – GEITA
WAKATI Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa katika mapambano kuhakikisha hakuna maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi (VVU), juhudi hizo zinaonekana kutoungwa mkono na watu wanaoishi na virusi hivyo.
Udanganyifu wa makazi na mawasiliano, ni moja ya changamoto kubwa katika Mkoa wa Geita kwa watu wanaoishi na VVU na kuhatarisha uwepo wa maambukizi mapya.
Sera ya Ukimwi ya mwaka 2001 inaeleza katika kuhakikisha maambukizi mapya hayatokei, Serikali na wadau mbalimbali wa afya na jamii lazima kushirikiana.
Inaeleza Serikali peke yake haiwezi kufikia lengo, hivyo ni lazima kila mdau kwa nafasi yake kuhakikisha anatoa mchango wake katika kuzuia maambukizi mapya.
Licha ya sera hiyo kutoa mwelekeo wa kupambana na ugonjwa huo, katika Mkoa wa Geita watu wanaoishi na VVU wanaonekana kwenda kinyume.
Wataalamu wa afya wanasema ili kuweza kuzuia maambukizi mapya, ni lazima watu wote wanaoishi na VVU na Ukimwi, kuhudhuria kliniki kwa muda mwafaka na kupatiwa dawa za kufubaza virusi (ARVs).
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko, wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu uandaaji wa programu bora za VVU na Ukimwi, alisema takwimu zinaonyesha Watanzania 225 huambukizwa VVU kwa siku.
Kulingana na takwimu hizo, kwa mwezi watu 6,750 huambukizwa VVU na kwa mwaka ni 81,000.
Alieleza hali ni mbaya zaidi kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24.
“Asilimia 40 ya maambukizi mapya hutokea kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 na kati yao wengi ni wanawake. Hii ina maana kwamba kati ya vijana waliopata maambukizi mapya, asilimia 80 ni wanawake,” anasema Dk. Maboko.
Licha ya tume hiyo kueleza maambukizi ya VVU yanapungua kutoka asilimia 5.1 mwaka 2011/2012 hadi asilimia 4.7 mwaka 2017, hualisia bado unaonyesha kuna maambukizi mapya yanatokea kila siku.
HALI ILIVYO GEITA
Katika Mkoa wa Geita baadhi ya maeneo ya kutolea huduma, watalaamu wanasema maambukizi yanazidi kuongezeka.
Kuwapo kwa wagonjwa wapya kila siku ni dhahiri nguvu kubwa bado inahitajika katika kuhakikisha watu wote wenye VVU wanaendelea kuhudhuria katika maeneo ya kutolea huduma za afya, wanapatiwa dawa na kuzitumia.
Katika mkoa huo wengi ambao wamepimwa na kugunduliwa kuwa na maambukizi, wamekuwa wakitoa taarifa za uongo za makazi yao na mawasiliano kwa wahudumu wa afya.
Mtaalamu wa afya katika Kituo cha Afya Katoro kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Geita, anayehusika na Kitengo cha Tiba na Matunzo (CTC), Augustino Mnyeti, anasema kuanzia Oktoba hadi Desemba 2017, wagonjwa 220 waliacha kutumia dawa.
Mnyeti anasema baada ya watu hao kuacha kutumia dawa, walianza kuwafuatilia. Asilimia 80 walikuwa hawajulikani walipo kutokana na kutopatikana katika makazi yao waliyotoa taarifa na mawasiliano yao.
“Kawaida mtu anapogundulika kuwa na maambukizi ya Ukimwi, tunamwanzishia huduma, hivyo hutakiwa kuacha mawasiliano yake na makazi yake ya kudumu yalipo.
“Tumekuwa tukipata wakati mgumu kuwapata, ukienda kumtafuta katika makazi ambayo ametuachia hapa, huwezi kumwona, hata ukiuliza majirani, viongozi wa eneo husika wanasema hawamfahamu.
“Lakini hata mawasiliano ya simu na yenyewe wanadanganya, na ndiyo maana hapa kwenye kituo chetu kila siku lazima tupate wagonjwa wapya watatu hadi watano, na tunahisi tatizo ni hilo, wengi kupotea,” anaeleza Mnyeti.
Mtaalamu huyo anasema hali hiyo inaweza kuwa kisababishi kikubwa cha ongezeko la wagonjwa wapya, kutokana na waliopo kuacha kutumia dawa na kusababisha usugu wa virusi vya Ukimwi.
“Tumekuwa tukiwaomba mawasiliano kwa ajili ya kuwafuatilia na kujua kama wanaendelea kutumia dawa, kama wanafuata masharti tunayowapatia, lakini tunapowakosa tunahisi madhara yanaweza kuwa makubwa,” anasema Mnyeti.
Anasema kwa kutumia muda mrefu na mbinu mbalimbali, wengi wamekuwa wakiwapata huku wakiwa na madhara makubwa kama ya magonjwa nyemelezi, ukiwamo ugonjwa wa mkanda wa jeshi, Kifua Kikuu na fangasi.
“Si wote ambao tunafanikiwa kuwapata, lakini kwa asilimia kubwa tunawapata, tena kwa muda mrefu, wanakuja na matatizo makubwa ya kupungua kwa kinga zao. Tumebaini shughuli za kiuchumi na kujinyanyapaa ndivyo vinawafanya wadanganye,” anasema Mnyeti.
Mratibu wa Ukimwi Wilaya ya Bukombe, Dk. Range Nyamhanga, anasema kati ya Oktoba na Desemba mwaka 2017 walipotea wagonjwa 1,396.
Nyamhanga anasema katika wilaya hiyo, kiwango cha maambukizi ni asilimia tano na kwamba wagonjwa waliopotea ni asilimia 26 ya wote waliopo wilayani humo.
Mratibu huyo anasema idadi hiyo ni kubwa na kwamba imekuwa ikisababisha juhudi za Serikali za kuzuia uwepo wa maambukizi mapya kugonga mwamba.
“Kitendo cha kupotea na sisi kuanza kuwatafuta, inatufanya tutumie muda mwingi kuwatafuta badala ya kufanya kazi za kuzuia ugonjwa usiendelee kuenea,” anasema Myamhanga.
Baada ya hali hiyo kuendelea kushamiri, wataalamu wa afya walifanya utafiti na kugundua chanzo ni shughuli za kibinadamu zinazowafanya wengi kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine.
WAGANGA WAKUU
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Bukombe, Dk. Irene Mukelebe, anasema eneo kubwa la Mkoa wa Geita limekuwa na shughuli za uchimbaji madini ambazo wananchi wengi wamekuwa wakijihusisha nazo.
“Tumebaini licha ya kuonekana wanajinyanyapaa wenyewe, wengi wanapotea kutokana na shuguli za uchimbaji madini. Eneo letu lina maeneo mengi ya wachimbaji wadogo.
“Kwahiyo unakuta wagonjwa wengi wanahama na kwenda eneo jingine kuchimba madini, wengi wamekuwa wakisahau au kupuuzia kuendelea kutumia dawa wakijiona bado wana nguvu za kutosha,” anasema Dk. Mukelebe.
Anaeleza wengi ambao wamekuwa wakipatikana baada ya kufuatwa katika machimbo hayo, wamekuwa hawatumii dawa na huku wakishambuliwa na magonjwa nyemelezi.
“Kudanganya makazi yao pamoja na mawasiliano mengine ni tatizo kubwa kwa wilaya yetu, tabia hii ni sawa na kujinyanyapaa.
“Baadhi wanaogopa kuonwa na wenzao kama wameshaambukizwa, lakini pia kutokuwa na elimu nako kumechangia hali hii,” anasema.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chato, Dk. Atanas Ngambakubi, anasema bila Shirika lisilo la kiserikali la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) kuja na mbinu ya kuanzisha Waviu Washauri (vikundi vya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi) kuwafuatlia watu waliocha dawa, hali ingekuwa mbaya zaidi.
Anasema shughuli nyingi za Ukimwi katika Halmashauri ya Chato zinafanywa na shirika hilo.
WADAU WA AFYA
Sera ya Ukimwi ya mwaka 2001 inawataka wadau wa afya nchini kutoiachia mzigo Serikali katika mapambano ya ugonjwa huo na badala yake wanatakiwa kushiriki kikamilifu kuhakikisha hakuna maambukizi mapya na kutokomeza ugonjwa huo.
Miongoni mwa wadau wa afya ambao wameanza kutekeleza agizo ni AGPAHI, ambao wamejikita katika kuboresha huduma kwa watu wanaoishi na VVU na Ukimwi.
Kupitia mradi wake wa tiba na matunzo unaojulikana kama “Boresha”, shirika hilo lisilo la kiserikali limeanza kuboresha vitengo vya tiba na matunzo (CTC) kwenye vituo vya afya na hospitali za wilaya na mkoa.
Aidha shirika hilo limekuwa likianzisha huduma za upimaji katika zahanati mbalimbali kwenye mikoa ambayo mradi huo unatekelezwa, ambayo ni Geita, Simiyu, Tanga, Mwanza, Shinyanga, Mara, Mwanza na Manyara katika Wilaya ya Simanjiro.
Katika Mkoa wa Geita, AGPAHI inatekeleza mradi huo kwa muda wa mwaka mmoja na hadi sasa imefanikiwa kukarabati majengo yanayotoa huduma za CTC zaidi ya 15 kwenye vituo vya afya na hospitali.
Shirika hilo pia limekuwa likifanya shughuli za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kupima familia nzima ya mteja ambaye anakuja kwenye kituo cha kutolea huduma za afya.
Licha ya kutekeleza mambo mengi kupitia mradi huo, jambo kubwa ambalo linafanywa na AGPAHI ni kusaidia Serikali kuwatafuta watu wanaoishi na VVU, ambao wameacha kutumia dawa au wamepotea.
Kwa kuwatumia washauri na watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (Waviu), shirika hilo limefanikiwa kuwarejesha katika matibabu zaidi ya watu 600 katika Wilaya ya Bukombe na Geita Vijijini wanaoishi na VVU ambao waliacha kutumia dawa.
Ofisa mradi kutoka AGPAHI, Adam Masesa, anasema kwa kutumia washauri hao ambao wanawezeshwa na shirika, wamekuwa wakiwatafuta wagonjwa walioacha kuhudhuria hospitali.
Masesa anasema washauri hao wamekuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha wanawatafuta watu walioacha dawa kwa kuwashauri na kuwatia moyo na hufanikisha kuwarejesha kuendelea kutumia dawa.
“Hawa Waviu Washauri tunawapa kila kitu, kama vitendea kazi, posho na mahitaji mengine. Kila baada ya miezi mitatu wanalipwa kwa kazi ya kuwafuatilia wagonjwa ambao wamekuwa watoro na wanafanikisha kuwarejesha.
“Kila mviu mshauri akimpata mgonjwa mmoja hulipwa Sh 10,000. Pia tunawapatia usafiri, vifaa vingine vya kufanyia kazi kama viatu, mwamvuli kwa ajili ya kujikinga na mvua na jua na kwa motisha hiyo wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii kubwa ndiyo maana tumefanikiwa,” anasema.
Mratibu huyo anasema pia washauri hao wamekuwa wakipatiwa mafunzo mara kwa mara jinsi ya kuwashawishi wagonjwa ambao wameacha kutumia dawa ili warejee na kuendelea na dawa.
“Waelimishaji rika wamekuwa na kazi kubwa ya kuwapatia elimu na ushauri wagonjwa ambao wameacha kutumia dawa, wengi wanaendelea kutumia dawa bila ya kuwa watoro tena,” anasema Masesa.
WAVIU WASHAURI
Mmoja wa washauri, Emmelda Assayi, anasema kwa ufadhili wa AGPAHI, wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa moyo na kujituma na kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kuwarejesha wagonjwa.
Hata hivyo, anasema bado wagonjwa wengi wamekuwa wakidanganya sehemu wanazoishi na mawasiliano yao hali ambayo imekuwa ikiongeza ugumu wa kuwapata.
“Tatizo kubwa wengi wanatudanganya makazi yao na hata mawasiliano yao, tunapata tabu kubwa sana kuwapata na kutumia muda mwingi kuwatafuta,” anasema Assayi.
Mshauri mwingine, Paul Nghata, analiomba shirika hilo kuwapatia usafiri wa pikipiki ili kufanya kazi hiyo kwa urahisi.
“Kuna baadhi ambao tumepewa baiskeli, lakini tunaona kama hazikidhi kwa sababu ya ugumu wa kuwapata. Hivyo tukipata usafiri huo itakuwa rahisi, tutaweza kuwapata kwa haraka zaidi,” anasema Nghata.