24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

TUMIA LUGHA VIZURI KUONGEZA USHAWISHI WAKO

Na CHRISTIAN BWAYA


HESHIMA ni hitaji la msingi la kila binadamu. Lugha kama chombo cha mawasiliano, ina nafasi kubwa ya ushawishi. Lugha kwa kawaida ikijenga taswira ya heshima kwa watu huongeza ushirikiano na masikilizano.

Kipimo kimojawapo cha heshima kwa mtu ni kumtambua kwa jina lake. Nakumbuka kuna mwanafunzi wangu mmoja aliwahi kunifuata kunieleza furaha yake kwa sababu tu nilimtaja kwa jina lake katika darasa la watu zaidi ya wanafunzi 1,400. Hakutarajia ningemfahamu kwa jina lake. Nilijifunza nguvu ya majina yetu.

Nikajifunza kuwa watu hujisikia vibaya wanapogundua huwafahamu. Kutokujua jina la mtu, kunakufanya uonekane huna tabia ya kujali. Ilivyo, ni kwamba huwezi kuwa na mahusiano mazuri na watu kama unawafanya wawe na hisia kuwa huwajali. Iwe kazini, nyumbani au kwingineko, ni muhimu ujenge tabia ya kuwaita watu kwa majina yao.

Hata hivyo, ni muhimu kuchukua tahadhari. Kulingana na nafasi ya mtu, yapo mazingira ambayo ukitumia jina la mtu unaonekana hujampa heshima anayostahili. Wakubwa kazini, kwa mfano, hupenda kutambulika kwa vyeo vyao. Kama unazungumza na meneja, usione haya kumwita kwa cheo chake ‘meneja’ hata kama unamwona ni mdogo wako kiumri. Utambulisho wa namna hii, ‘daktari, injinia, afande, mchungaji, padrI, sheikh’ unamfanya mhusika ajisikie kupewa hadhi anayostahili. Kwa namna hii, inakuwa rahisi kukusikiliza ukiwa na jambo unalohitaji alifanyie kazi.

Lugha ya uungwana

Kuna lugha unaweza kuzitumia kwa nia njema kabisa lakini zikachora taswira ya mtu asiye muungwana. Uungwana ni pamoja na kujenga taswira ya mtu mkomavu asiyeoongozwa na hisia. Pia, uwezo wa kujali hisia na heshima ya mwenzako nao ni uungwana. Nimewahi kuhudhuria mkutano mmoja wa wafanyakazi na wakubwa wao wa taasisi. Mfanyakazi mmoja alinyanyuka na kupaza sauti, ‘Nimechoka na manyanyaso yako (boss). Sitaweza kuvumilia tena. Umekuwa na upendeleo wa wazi kwa watu. Jambo hili halivumiliki.’

Maneno kama haya yanaweza kuwa kweli lakini hayana uungwana. Kule yanakoelekezwa maneno haya, yanaweza kueleweka kama chuki na udhalilishaji. Katika mazingira kama haya, vigumu anayelengwa kuyachukulia kwa uzito na kuyafanyia kazi kwa sababu atalazimika kutetea heshima yake kwa kukudhalilisha. Unahitaji kujifunza kuwa mstaarabu hata pale unapokuwa na madai ya msingi kwa mtu. Huhitaji kumdhalilisha unayemwomba jambo hata kama ni kweli anakudhalilisha.

Tumia lugha ya unyenyekevu. Maneno kama, ‘tafadhali,’ ‘ninaomba,’ ‘nisaidie’ yanapamba ujumbe na kufanya uonekane hujichukulii kuwa muhimu kuliko watu wengine. Hata kama ni kweli unanyanyaswa, unahitaji kujenga ustahimivu wa kihisia na kutumia lugha ya kistaraabu. Lugha ya kiungwana, kwa kawaida, humfanya yule unayelenga asikie ujumbe wako ajisikie kuheshimiwa. Heshima, kama nilivyotangulia kudokeza, inaongeza ushawishi wako.

Umakini unapokosoa

Pamoja na kuwa muungwana, zipo nyakati unalazimika kuonesha mapungufu ya mtu yule yule unayetaka kumshawishi. Hata katika mazingira kama haya, bado unahitaji kuwa makini unapokosoa. Kwanza, ni muhimu uanze na suala chanya kumvuta anayekusikiliza aamini unatambua mazuri aliyonayo. Baada ya kubainisha mazuri hayo, sasa unaweza kuonesha mapungufu kwa lugha isiyo na ukakasi. Kanuni hapa ni kwamba usichopenda kuambiwa na wenzako, usimwambie mwenzako.

Lakini pili, kuwa makini unapotumia maneno kama ‘lakini’, ‘pamoja na hayo’ na ‘hata hivyo.’ Maneno haya yasipotumiwa vizuri yana tabia ya kufuta sifa zinazoyatangulia. Kwa mfano, unaposema, ‘Umefanya kazi kubwa sana kubadilisha taasisi hii lakini wewe ni mbabe.’ Mlengwa anaweza kufarijika kusikia maneno ya mwanzo. Maneno hayo mazuri yanapofuatiwa na neno ‘lakini,’ msikilizaji huzingatia ujumbe uliobebwa baada ya neno hilo na kuamini ulichotaka akisikie ni huo ubabe wake.

Tunapenda kutumia maneno haya katika mazungumzo yetu ya kawaida bila kujua athari za kisaikolojia kwa wasikilizaji. ‘Wewe ni kijana mzuri lakini hujui kuishi na watu’, ‘Wewe ni mtu mwenye bidii lakini huna nidhamu.’ Ingawa kwa haraka haraka huwezi kubaini athari ya maneno yanayofuata baada ya ‘lakini,’ ukweli ni kwamba anayeambiwa maneno hayo anaishia kujisikia vibaya.

Jifunze kutumia maneno yanayoonesha matarajio chanya badala ya kuonesha matatizo moja kwa moja. Kwa mfano, ‘Unaweza kufanya vizuri zaidi kwenye nidhamu kama unavyofanya kwenye bidii,’ ‘Najua wewe ni kijana mzuri unayeweza kujifunza kuishi na watu vizuri zaidi.’

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles