22.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ubadhirifu ofisi ya CAG

mtz1*Yakarabati nyumba ya kigogo kwa mamilioni

*Yanunua samani, gari kinyume na utaratibu

 

Na Masyaga Matinyi, Dar es Salaam

OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imeingia katika kashfa nzito na kudaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.

Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli inapambana na kudhibiti matumizi makubwa pamoja na vita dhidi ya ufisadi.

Ofisi hiyo ambayo inaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Profesa Juma Assad, imethibitika kufanya matumizi hayo pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.

MTANZANIA limebaini katika uchunguzi wake kuwa tangu Profesa Assad alipoteuliwa kushika wadhifa huo Novemba 5, 2014 na kuapishwa Desemba 2 mwaka huo na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ofisi hiyo imebariki mambo kadhaa kinyume na maadili na majukumu yake.

 

UKARABATIWA NYUMBA

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo MTANZANIA inazo, Aprili mwaka jana Ofisi ya CAG ilianza mchakato wa kukarabati nyumba ya Serikali Plot namba 973 iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam inayotumiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa kwa mujibu wa taratibu, nyumba zote za Serikali zipo chini ya Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) na taratibu zote za ukarabati hufanywa na kusimamiwa na wakala huyo.

“Lakini hapa kwetu hali ilikuwa tofauti kabisa, ofisi ya CAG iliamua kufanya yenyewe ukarabati huku ikijua kabisa inakiuka utaratibu na ikatoa kazi hiyo kwa kampuni bila hata kutangaza zabuni, hata kampuni husika haikuwa na mkataba wowote na ofisi ya CAG.

“Cha kushangaza zaidi kampuni hiyo ya M/SAfriq-Engineering and Construction Co. Ltd si ya kigeni, ni ya Waswahili wenzetu, lakini ililipwa gharama za kazi kwa dola za Marekani badala ya shilingi ya Tanzania.

“Na si kwamba ililipwa kwa wamu kama ilivyo kawaida, bali wao walilipwa jumla ya dola za Marekani 102,570 kwa mkupuo, tena hata kabla ya kuanza kazi, ambapo pamoja na gharama zikiwamo kodi za Serikali, jumla ilifika Sh milioni 281.8,” kilisema chanzo chetu.

 

Mtaalamu mmoja wa majengo katika Chuo Kikuu cha Ardhi jijini Dar es Salaam (jina tunalihifadhi), ameliambia MTANZANIA kuwa kiasi hicho cha fedha kinatosha kujenga nyumba nzuri ya kisasa ambayo inaweza kutumiwa na ofisa yoyote mwandamizi wa Serikali.

Kabla ya Profesa Assad kuingia katika nyumba hiyo, ilikuwa ikitumiwa na CAG aliyestaafu, Ludovick Utouh.

 

UNUNUZI SAMANI ZA NDANI

Pamoja na hali hiyo ofisi hiyo ya CAG ilikiuka sheria na taratibu za Serikali kutokana na kiongozi wa taasisi hiyo ya umma kulipwa posho ya Sh milioni 18 kwa ajili ya kununua samani za ndani ambazo hubadilishwa kila baada ya miaka mitano.

Katika kutekeleza stahiki yake hiyo, Profesa Assad alikwenda mwenyewe Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kwa ajili ya kununua samani hizo za ndani Desemba 27, mwaka juzi.

Inadaiwa katika safari hiyo CAG alikiuka sheria na taratibu za Serikali kwa kutumia zaidi ya Sh milioni 18, ambazo zinaruhusiwa kwa “KUNDI A” la viongozi kwa mujibu wa waraka wa Idara Kuu ya Utumishi (Ofisi ya Rais) namba 1 wa mwaka 2014.

Baada ya kununua samani hizo, ofisi yake ililipa fedha za ziada kiasi cha Sh milioni saba kwa ajili ya kuzisafirisha, pamoja na dola za Marekani 4,265 (sawa na shilingi milioni 9) kwa ajili ya kodi, visa na gharama nyingine za usafiri.

 

UNUNUZIWA SHANGINGI

Mei 13, 2015 ofisi hiyo ya CAG ilimwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) barua yenye kumbukumbu namba FA.242/305/01 yenye kichwa cha habari; “UNUNUZI WA GARI MOJA KWA AJILI YA MATUMIZI YA CAG TOYOTA LAND CRUISER GX-V8 200 HIGH.”

Baada ya Mtendaji Mkuu wa GPSA, J. Mwambega kupokea barua ya ombi hilo, alimjibu kwa barua ya Mei 15, mwaka jana, yenye kumbukumbu Na. CAD.124/318/01/64.

Sehemu ya barua hiyo ambayo nakala ilipelekwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha inasomeka; “Napenda kukujulisha kwamba ombi lako la ununuzi wa dharura halikubaliki kwa sasa kwa sababu upo utaratibu ulioandaliwa na Serikali kwa ajili ya ununuzi wa magari ya viongozi.

“Kwa kuzingatia hilo, nakushauri ulipie gharama za ununuzi wa gari hilo US $ 84,480.05 kupitia akaunti ya GPSA – UNUNUZI WA MAGARI KWA PAMOJA yenye Na. 0250095100500 ‘US$ Account’ iliyopo benki ya CRDB Bank (Plc) Tawi la Vijana, Dar es Salaam.”

Pamoja na maelekezo hayo, ofisi hiyo ya CAG ilikiuka maelekezo ya Mtendaji Mkuu wa GPSA na kununua gari hilo kwa dharura, ambapo malipo yalifanyika Mei, 15, 2015.

 

SAFARI YA SEYCHELLES, CHINA

Septemba 5, mwaka jana maofisa kadhaa akiwamo Profesa Assad walisafiri kikazi kwenda nchini Seychelles, ambapo Septemba 11, waliondoka nchini humo na kwenda Dubai, Septemba 12 waliondoka Dubai kwenda Nanjing (China), Septemba 19, waliondoka Shanghai kwenda Beijing na Septemba 22, waliondoka Beijing kurejea Dar es Salaam.

Uchunguzi umebaini kuwa ukiacha safari ya Seychelles ambako kulikuwa na mkutano wa wakaguzi wa hesabu, safari ya China haikuwa na uhusiano na majukumu ya kiofisi, ambapo tiketi za ndege ziligharimu Sh milioni 26.4.

Mbali ya CAG, ofisa mwingine kutoka ofisi yake, Edwin Rweyemamu, naye alisafiri kwa mzunguko kama huo, ambapo tiketi yake iligharimu Sh mil 21.7.

Ofisa wa tatu ambaye hakwenda Seychelles, lakini aliambatana na CAG kwingineko ni Elibariki Lyatuu, ambaye tiketi yake iligharimu Sh milioni 21.4.

Wote walisafiri kwa kutumia daraja la “Business Class” ambapo jumla ya gharama za tiketi zote tatu ilikuwa Sh mil 69.6, gharama ambazo zinatajwa kuwa kubwa kulinganisha na gharama halisi za safari kwenda nchi hizo, gharama ambazo hubadilika kutegemea na msimu wa safari.

Uchunguzi wa MTANZANIA ulibaini fedha hizo zilikopwa kutoka fungu la fedha za Umoja wa Mataifa (UN) zinazotumika katika shughuli mbalimbali ya ukaguzi wa hesabu, ambapo ofisi ya uhasibu ilisema katika dokezo.

Dokezo hilo linasomeka; “Lipa Sh 69,659,200 kwa ajili ya tiketi za safari ya CAG na ujumbe wake nchini Seychelles na China. Fedha hii ilipwe toka UN, lakini tukumbuke kuirudisha mara tutakapopokea mgawo wa fedha ujao.”

 

KAULI YA CAG

MTANZANIA ilipomtafuta Profesa Assad na kufanya mahojiano naye Alhamisi iliyopita ofisini kwake, alikataa kujadili au kuzitolea ufafanuzi tuhuma dhidi yake.

“Kwanza unajua ni makosa kuwa na nyaraka za ofisi ya Serikali, sasa kama ukiandika basi na sisi tutachukua hatua. Pia hayo yote uliyosema mimi sihusiki, watafute watendaji wakupe majibu,” alisema Profesa Assad.

Pamoja na kutoa majibu hayo, alisema atahakikisha anampata mfanyakazi anayetoa siri za ofisi na kumfukuza kazi mara moja.

Baada ya mwandishi kuagana na CAG na kuondoka, akiwa nje ya ofisi hizo, ofisa mmoja ambaye alihudhuria mahojiano hayo, alimwita na kumwomba nakala ya nyaraka husika, ambapo alipewa, lakini hakuna majibu au maelezo yoyote ambayo yalitoka baada ya hapo.

 

MAJUKUMU YA CAG

Kwa mujibu wa sheria, majukumu ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ni pamoja na kuhakikisha wizi, upotevu na ufujaji wa fedha na mali za umma unadhibitiwa mapema, kwa kufuata taratibu za uhasibu na kanuni za fedha.

Majukumu mengine ni kusaidia utendaji wa mara kwa mara kwa kutathmini taratibu za fedha, ili kuhakikisha kuwa zinafaa kwa wakati uliopo na zinakidhi makusudi ya kuwapo taratibu hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles