23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAWAONDOA

Theresia Gasper-Dar es salaam

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Shirikisho la Soka Afrika(Caf), timu za Yanga na Azam leo zitashuka  dimbani kusaka ushindi maeneo tofauti, ili kufuzu raundi ya kwanza.

Yanga itakua ugenini nchini Botswana kukabiliana na Township Rollers, katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaochezwa jijini Gaborone.

Mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Township iliilazimisha Yanga sare ya bao 1-1.

Matokeo hayo yanaufanya mchezo  wa leo kuwa mgumu zaidi kwa Yanga, kutokana na kuruhusu bao la ugenini.

Kutokana na mazingira hayo, Yanga itatakiwa kuhakikisha inapata ushindi wa idadi yoyote ya mabao au sare ya kuanzia mabao 2-2, ili kutinga raundi ya kwanza.

Kinachoongeza mzuka kwenye kambi ya Yanga, ni kurejea kikosini kwa beki tegemeo wa kikosi hicho, Kelvini Yondan.

Yondan alikosekana katika kikosi kilicholazimishwa sare ya bao 1-1, kutokana na kuwa  mapumzikoni.

Mkongwe huo alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’  kilichoibwaga Kenya, kwenye michezo ya kusaka tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani(Chan).

Tanzania iliitupa nje Kenya, baada ya kutoka suluhu Dar es Salaam na kisha kushinda kwa mikwaju ya penalti 4-1, jijini Nairobi.

Miamba hiyo ya Jangwani itaendelea kuwakosa nyota wake wapya kipa Mkenya Farouk Shikalo, mshambuliaji raia wa DRC, David Molinga na beki wa kimataifa wa Burundi Mustapha Seleman kutokana na kukosa hati za uhamisho wa kimataifa(ITC).

Ili kujihami na mchezo wa ugenini, Yanga ilicheza michezo miwili ya kirafiki ya kujipima ubavu na timu za Polisi Tanzania, ambapo ilichapwa mabao 2-0, Uwanja wa Ushirika, Moshi kisha ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AFC Leopards  ya  Ligi Kuu Kenya.

Kocha wa Yanga,  Mwinyi Zahera aliliambia MTANZANIA jana kuwa, wanafahamu mchezo huo utakuwa mgumu, lakini wameijiandaa kwa mapambano wakiwa na lengo la kuhakikisha wanapata ushindi ugenini na kusonga mbele hatua inayofuata.

 “Tumejiandaa vizuri kwa mchezo huu, kila mchezaji yupo fiti, sina kikubwa cha kuwaambia mashabiki wetu lakini watarajie ushindi,” alisema Zahera mwenye uraia wa DRC na Ufaransa.

Kwa upande mwingine, Azam itaikaribisha Fasil Kenema ya Ethiopia,  katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali wa Kombe la Shirikisho Afrika, utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex Dar es Salaam.

Azam  itakuwa na kibarua kizito cha kuhakikisha kinapata ushindi wa kuanzia mabao mawili kwenye uwanja wake huo wa nyumbani, baada ya kutandikwa 1-0, katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Bahir Dar nchini Ethiopia.

Matajiri hao wenye maskani yao eneo la Chamazi pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam, wamepania kupindua matokeo.

Kocha wa Azam, Etienne Ndayiragije alisema jana kuwa wamepata fursa ya kurekebisha udhaifu wao kupitia mazoezi.

Ndayiragije ni wazi atakuwa ameboresha eneo lake la ushambuliaji pamoja na ulinzi ambayo yaliyonekana kuwa dhaifu pia wakati wa mchezo wa Ngao ya Jamii, kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba uliochezwa Agosti 18.

Katika mchezo huo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-2.

“Tumefanya maandalizi ya kutosha kwa kurekebisha maeneo yaliyoonekana yana kasoro, ombi kwa mashabiki wa Azam na Watanzania kwa ujumla wajitokeze kuwa kuiunga mkono, kwavile hii timu inawakilisha nchi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles