WAKATI Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akitoa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 ya Sh trilioni 31.6, ilihali ile ya Sh trilioni 29.5 ya mwaka 2016/17 ikiwa haijatekelezeka, wadau wametoa maoni tofauti, wengi wakisema bajeti iliyopita ilitawaliwa na siasa.
Wamesema pia mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2017/18 yaliyotolewa mbele ya wabunge Jumanne wiki hii yanatia wasiwasi kutokana na vipaumbele vyake kujielekeza kwenye miradi ya ujenzi huku ile inayogusa wananchi walio wengi, ikiwamo elimu, maji, kilimo, afya na nishati vikiachwa nyuma.
Baadhi ya vipaumbele vya bajeti hii ni pamoja na mradi wa kuendeleza miradi ya makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga (Njombe), ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge), kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATC), ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi kimiminika, Lindi na uendelezaji wa maeneo maaalumu ya kiuchumi.
Taarifa ya Dk. Mpango iliyotolewa Jumanne inaonyesha katika mwaka 2017/18, Serikali inapanga kutumia Sh trilioni 31.69 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.
Katika bajeti hiyo, Sh trilioni 19.70 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, kati yake Sh trilioni 7.20 ni za mishahara na Sh trilioni 9.46 ni za kulipia deni la Taifa.
Matumizi mengineyo yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 3.03 ambapo Sh trilioni 2.08 ni matumizi yaliyolindwa; na Sh bilioni 274.9 ni matumizi yanayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh trilioni 11.99 ambapo kiasi cha Sh trilioni 8.96 ni fedha za ndani na Sh trilioni 3.02 ni fedha za nje.
Wakati katika mwaka ujao wa fedha Serikali ilipanga kutumia Sh trilioni 11.99 kwa ajili ya shuguli za maendeleo, katika bajeti ambayo bado miezi mitatu kumalizika, kati ya Sh trilioni 11.82 zilizopangwa kutumika kwa shughuli za maendeleo, mpaka Februari mwaka huu, ni Sh trilioni 4.168 sawa na asilimia 35.26 ya lengo ndizo zimetolewa.
Ni kutokana na hali hiyo baadhi ya wadau wanaona bajeti ya mwaka 2017/18 ambayo imeizidi ile ya mwaka 2016/17 kwa Sh trilioni 2.1, kama ya kisiasa na isiyotekelezeka.
Kwamba hatua ya Serikali kushindwa kutekeleza bajeti ya 2016/2017 imetokana na uwepo wa matumizi mabaya yaliyokuwa yakifanyika kwa amri za kisiasa.
Kwamba serikalini walikuwa wakijisahau na kufanya uamuzi katika masuala ya fedha kwa vitu ambavyo hata havikuwapo katika mpangilio wa bajeti.
Kwamba bajeti haikutekelezeka kwa sababu matumizi hayakuwa mazuri, vitu kama ununuzi wa ndege, kuhamia Dodoma vimegharimu fedha; na vyote hivyo havikuwapo kwenye bajeti. maamuzi yalifanyika kisiasa badala ya kusubiri
ili waweze kutekeleza mwaka unaofuata.
Tunadhani wadau hawa wako sahihi kabisa.
Tunapendekeza pia kuangalia umuhimu wa Taifa kuondokana na kutegemea fedha za nje kwani wengi wa wahisani wamekuwa wakiahidi bila kutekeleza ahadi zao.
Tunasema kuna umuhimu wa kuondoa utegemezi kama Kenya ambayo imeshafikia huko kwani bajeti nzima inatekelezwa kwa vyanzo vya ndani. Hakuna fedha za kutoka nje.
Tukiamua kwa dhati na sisi inawezekana.