AVELINE KITOMARY
HAKUNA ubishi kwamba asilimia kubwa ya watumiaji dawa za kulevya wamepoteza mwelekeo na hawana malengo tena ya maisha.
Dawa za kulevya zinaharibu maisha ya vijana wengi hivyo kushindwa kufikia malengo yao, huku wakibaki mitaani kuendeleza vitendo vya kihalifu.
Kwasasa, watumiaji wa dawa za kulevya wanaingia kwenye hatari kubwa zaidi, kwa sababu wameanza kutumia dawa za kuua panya baada ya kuadimika kwa dawa za kulevya kama Cocain.
Hata hivyo, Serikali kupitia Kamishina wa Kinga na Tiba katika Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Dk. Peter Mfisi, anasema tayari wameshabaini tatizo hilo na wanachukua hatua kuweza kuwanusuru watumiaji hao.
Imebainika kuwa watumiaji wa dawa hizo pia wamekuwa wakitumia dawa za usingizi au za kutuliza maumivu zilizopo katika kundi la Indocid, ambazo ni hatari zaidi kwa afya zao.
Hata hivyo, hali hiyo inatokana na kuzibwa kwa mianya mingi ya uingiaji wa dawa za kulevya nchini hivyo, kusababisha kuadikimika kwa dawa za kulevya.
Kwanza, naipongeza Serikali kwa kufanikiwa kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya hapa nchini. Hii ni dalili nzuri ya kuondokana na tatizo hili.
Aidha, naishuri Serikali iwasaidia waathirika wa dawa za kulevya wanaotumia njia mbadala kwa kuchanganya dawa hizo na sumu ya panya, kwa kuwajengea vituo maalumu vya uangalizi ili wapewe ushauri na kuwawezesha kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.
Wakati mwingine malezi mabaya ya wazazi au walezi yanachangia vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya hivyo, ni jukumu la kila mzazi au mlezi kuwa karibu na watoto wao ili kuwafundisha na kuwashauri kuhusu kusimamia malengo yao hatimaye kutojiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.
Tumeshuhudia watoto wengi wakizurura hovyo mitaani kwa kukosa malezi bora ya wazazi, jambo hili limekuwa likiharibu mlolongo mzima wa maisha yao.
Siku zote, mtoto anapojichanganya na makundi ya watu mitaani ndio chanzo cha yeye kufanya hata kile ambacho kitagharimu maisha yake ya baadaye, kama kuvuta bhangi na mambo mengine mengi.