24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii ijiandae matumizi ya mifuko mbadala

Na Robert Hokororo, OMR

SERIKALI imetangaza Juni mosi mwaka huu kuwa ni mwisho wa matumizi yote ya mifuko ya plastiki na hivyo wananchi wanapaswa kuanza kutumia mifuko mbadala kubebea bidhaa.

Kutokana na zuio hilo, wananchi hawataruhusiwa kufanya uzalishaji, uingizaji, usafirishaji nje ya nchi, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko hiyo kwa namna yoyote.

Watu wengi wamekuwa wakijiuliza mifuko gani watumie kubebea bidhaa baada ya hatua hiyo ya Serikali ya kupiga marufuku mifuko ya ‘rambo’.

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inawatoa hofu wananchi na kusema kuwa ipo mifuko mbadala wa ile ya plastiki ambayo inaweza kutumika kubebea bidhaa.

Mifuko inayotajwa kuwa mbadala ni ile ya karatasi, nguo, vikapu na gunia ambayo ni rafiki kwa mazingira, kwani inapoisha muda wake huoza katika mazingira tofauti na ile ya plastiki iliyokatazwa.

Pamoja na hayo, pia mifuko mbadala haina madhara kwa afya ya binadamu na mazingira kwani pindi imalizapo matumizi, huweza kuharibika kwa urahisi na kwa haraka inapochomwa.

Unaweza kujiuliza wakati mifuko ya plastiki inazuiwa je, uhakika wa upatikanaji wa mifuko mbadala utakuwaje? Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, anawahakikishia wananchi upatikanaji wake utakuwa wa uhakika.

Waziri Makamba anasema wapo wawekezaji ambao tayari wameonesha nia ya kuzalisha mifuko mbadala ya karatasi na kuwa hapa nchini zipo malighafi za kutosha.

Uwezo na utayari wa uzalishaji wa mifuko mbadala ni wa kuridhisha na kuwa vipo viwanda 25 vya karatasi hapa nchini sambamba na viwanda vinavyozalisha mifuko mbadala ya karatasi, ukili na nguo.

Viwanda hivyo vinatarajiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji katika muda mfupi kuanzia sasa, hivyo kusaidia wananchi kupata nyenzo za kubebea bidhaa zao.

Lipo kundi jingine la wawekezaji na wamiliki wa viwanda ambao walikuwa wanasubiri tamko la Serikali ili waweze kuwekeza mara moja katika uzalishaji wa mifuko mbadala.

Kundi la tatu ni lile la viwanda ambavyo vinazalisha kwa ajili ya soko la nje zaidi ikiwemo kiwanda cha Mufindi Paper Mills (MPM) cha Iringa ambacho huzalisha malighafi za karatasi katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Zambia.

Sambamba na hilo, tayari wamiliki wa viwanda hivyo wameihakikishia Serikali kuzalisha kwa wingi malighafi za kutosheleza watengenezaji wa ndani wa mifuko ya karatasi.

Kwa upande wa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeendesha kikao cha wadau mbalimbali ili kujadili fursa za uwekezaji wa uzalishaji mbadala wa mifuko ya plastiki.

Wakati huo imeandaa mpango kazi wa utekelezaji wa katazo hilo kwa kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha wananchi wote wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.

Wananchi wanahimizwa kuwekeza ili kuongeza kasi katika uzalishaji wa mifuko mbadala ili kwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na wakati huo huo kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, Serikali inatoa wito kwa wadau wote wakiwemo wawekezaji katika viwanda nchini kuzingatia umuhimu wa uchumi wa mbadala wa mifuko ya plastiki.

Serikali inatoa wito kwa wenye nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko mbadala wa plastiki, wawasiliane na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Baraza la Taifa la Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Maendeleo la Viwanda Vidogo (SIDO) na taasisi za fedha.

Hatua hiyo itawezesha ajira nyingi zaidi na kukuza kipato kwa wananchi wa kawaida hasa wanawake katika kutengeneza mifuko mbadala ikiwemo kusuka vikapu ambako kunahitaji teknolojia rahisi na nguvu kazi.

Katika kuhakikisha shehena ya mifuko ya plastiki inamalizika, utaratibu maalumu unafanywa kwa kila wilaya kutenga eneo maalumu la kuikusanyia na wananchi kutangaziwa maeneo hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles