30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

TRA kutaifisha magari yanayoingiza bidhaa za magendo

NA PETER FABIAN -KILIMANJARO


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro inakusudia kutaifisha pikipiki, bajaji, magari na malori makubwa yanayotumika kubeba bidhaa za magendo zinazoingizwa na kuuzwa kinyume cha sheria ya kodi hapa nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo alipozungumza na gazeti hili juzi.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara wanaoagiza na kuingiza bidhaa mbalimbali kutoka Kenya wamekuwa wakikwepa kodi kwa kutumia njia za panya, huku wengine wakifanya udanganyifu katika nyaraka katika vituo vya mpakani eneo la Tarakea na Holili vilivyopo mkoani hapa.

Mbibo alisema licha ya udhibiti mkubwa unaofanywa na maofisa wa TRA waliopo katika vituo hivyo kupambana na wafanyabiashara wadanganyifu na wasiopenda kufuata utaratibu na sheria za uagizaji na uingizaji zilizopo kwa kutumia mtandao, wamekuwa wakikumbana na kibano cha kutozwa kodi bila msamaha, huku baadhi yao wakizikimbia bidhaa zao na kuzitelekeza yakiwamo magari madogo, malori na pikipiki wanapokamatwa.

“Tutaendelea kuwakamata baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoingiza bidhaa kwa njia ya magendo, sasa tutataifisha bidhaa zote ambazo watakutwa nazo wakiingiza bila kuwa na nyaraka halali za malipo ya kodi na ushuru kwa mujibu wa sheria, katika maeneo ya mipakani, Moshi Mjini katika maduka yao na maghala, TRA tumejipanga vizuri kufanya ukaguzi ili kuwakamata waliodanganya,” alisema.

Akifafanua kuhusu utaifishaji huo, alisema watafanya hivyo hata kama magari hayo yamekodishwa kubeba bidhaa hizo za magendo.

Alisema wamiliki wa magari, bajaji na pikipiki waepuke vyombo vyao kutumiwa na wafanyabiashara waliozoea kuingiza bidhaa za magendo kwa kuwa vitataifishwa.

“Watambue taratibu za vituo vya mpakani ziko kisheria, wafanyabiashara wanazifahamu sheria na taratibu, hivyo hakutakuwa na visingizio watakapokamatwa.

“Boda za Tarakea na Holili tumeweka taratibu za kuyakagua magari yenye bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufungua ‘sili’ kujiridhisha na kilichopo katika nyaraka za forodha, ikibainika umepakia bidhaa nyingine zaidi ili kuja kukadiriwa kodi mpakani bidhaa hiyo itataifishwa.

“Hata upekuzi mkali upo katika Uwanja wa KIA katika mizigo inayoletwa kwa ndege na ile ambayo abiria wanasafiri nayo lengo likiwa ni udhibiti,” alisema.

Pia alisema taarifa mbalimbali kutoka kwa raia wema wanazofikisha ofisi za TRA zimekuwa zikifanyiwa kazi ikiwamo kuchukua hatua na uamuzi wa kuwabadilisha baadhi ya watumishi (maofisa) wakitajwa kushirikiana na wafanyabiashara katika eneo la mpaka wa Tarakea (Kilimanjaro) – Loitoktoku (Kenya) na Holili (Kilimanjaro) – Taveta (Kenya) ili kuongeza uwajibikaji katika maeneo hayo na Uwanja wa KIA.

“Tumechukua hatua hii ya kuwabadilisha maofisa ili kutofanya kazi kwa mazoea na kuepuka kushirikiana na wafanyabiashara wasio waminifu kutumia mwanya wa mazoea katika kukwepa kodi na kuingiza bidhaa zilizopigwa marufuku na zinazoingizwa kinyume cha taratibu za mtandao wa TRA na uagizaji wa bidhaa za viwandani katika soko la Afrika Mashariki  na bidhaa zinazotakiwa kuuzwa nchi moja pekee,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles