31.3 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

TRA KUAJIRI 400 WAKATI WOWOTE KUANZIA SASA

Na BENNY MWAIPAJA- SHINYANGA

SERIKALI inatarajia kuajiri wafanyakazi 400 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi kifupi kijacho, ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika Mamlaka hayo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na makusanyo ya kodi.

Ahadi hiyo imetolewa Mjini Shinyanga na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utendaji wa Mamlaka hayo mkoani humo.

Dk. Kijaji amesema taratibu zote zimekamilika na wakati wowote nafasi za ajira zitatangazwa na kwamba nafasi hizo zimelenga kuiwezesha TRA kuwafikia watu wengi zaidi na kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi.

“Tunatambua changamoto ya uchache wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ndio maana tumeamua kuajiri wafanyakazi hao 400 ambao ni wengi kuliko kada nyingine ili tuweze kuimarisha utendajikazi wa Mamlaka na hivyo kuongeza makusanyo ya kodi zinazotakiwa kwa shughuli za maendeleo nchini,” alisema Dk. Kijaji.

Alisema pamoja na uhaba wa watumishi, anaamini kuwa lengo la mwaka huu la kukusanya shilingi trilioni 17 ambazo Mamlaka hayo imepangiwa yatafikiwa na ikiwezekana kuzidi kwa kutumia wafanyakazi waliopo.

Dk. Kijaji alitoa rai kwa wafanyakazi wa TRA kuwa waadilifu na kwamba atakayebainika kukiuka maadili yake ya kazi atachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria.

Awali Meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Shinyanga, Jumbe Samson, alieleza kuwa mkoa wake umepangiwa lengo la kukusanya shilingi bilioni 18 na kwamba wana uhakika wa kufikia lengo hilo kutokana na mikakati mbalimbali waliyojipangia ikiwemo kusimamia ukusanyaji kodi kikamilifu katika sekta ya madini.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles