Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na Kampuni Tanzu ya GASCO limeendea kuelimisha umma juu ya ulinzi na usalama wa miundimbinu ya bomba la gesi kwa njia mbalimbali ikiwemo mikutano ya hadhara.
Ikumbukwe kuwa elimu ya mara kwa mara imekuwa na matokeo chanya kwani ulinzi wa miundombinu ya gesi asilia umeendelea kuimarika hali inayosaidia miundombinu hiyo kuwa salama nyakati zote. Â
Aidha, katika kuhakikisha miundombinu inakuwa salama ajenda ya ulinzi na usalama imekua ya kudumu kwenye Mitaa na Vijiji vyote vinavyopitiwa na miundombinu hiyo kuanzia Mtwara hadi Dar es Salaam.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Juni 8, mwaka huu katika mtaa wa Ulongoni A Gongo ka mboto jijini Dar es Salaam, wananchi wa mtaa huo sambamba na mambo mengine walipewa elimu ya ulinzi na usalama wa miundombinu ya bomba la gesi asilia.
Dickson Kibala ambaye ni Afisa Ulinzi na Usalama wa miundombinu ya bomba la gesi asilia alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Mtaa wa Ulongoni A katika kuimarisha ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za kiusalama na kushirikiana kukomesha shughuli zote za kibinadamu ndani ya Mkuza wa gesi asilia kama kuchimba mchanga/kokoto, ujenzi na shunguli nyingine.
“Tunapongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Mtaa wa Ulongozi A kwa kuimarisha ulinzi pamoja na kusimamia vizuri fedha zinazotolewa na TPDC/GASCO kwa ajili ya kutekeleza  miradi ya maendeleo pamoja na  usafi wa Mkuza,” amesema Kibala.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Mtaa wa Ulongoni A, Abdulrahim Munisi, amepongeza jitihada zinazofanywa na TPDC kwenye kutoa elimu pamoja na kuinua huduma mbalimbali za kijamii kwenye mitaa inayopitiwa na midombinu ya bomba la gesi ikiwemo mtaa wa Ulongoni A.
“TPDC/ GASCO mmekuwa wadau wa mfano kwenye kushirikiana na jamii, tunashukuru kwa kutupatia fedha za kujenga  ofisi nzuri ya Mtaa tena ya kisasa ambayo kwa sasa imekamilika na inatumika kuhudumia wananchi, mtaa wetu utaendelea kutoa ushirikiano katika kulinda miundombinu ya bomba la gesi asilia,” amesema Munisi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Gongo la Mboto, Lucas Lutainurwa, ametoa shukrani kwa uongozi wa TPDC/GASCO kwa kuendelea kuinua huduma za kijamii ikiwemo sekta ya elimu kwenye kata ya Gongo la Mboto.
Aidha, ametoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kusaidia juhudi za serikali kwenye kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kama maji, elimu na afya. Â
“Katika mwaka wa fedha umliopita wa 2022/2023 tulipokea Shilingi 69,000,000 kutoka TPDC/GASCO kwa ajili ya Ujenzi wa Bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Mzambarauni, ni jambo kubwa na la kujivunia kwani ujenzi wa bweni ulikamilika na tayari  linatumika,’’ amesema Lutainurwa.