24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

TOST yawaahidi wafanyabiashara ushirikiano

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital 

Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), imewahakikishia walipa kodi nchini kuwa itashughulikia malalamiko ya wafanyabiashara yanayohusiana na  kodi kwa haki na usawa ili kuchochea ulipaji kwa hiyari.

Hayo yameelezwa leo Desemba 15,2023 jijini Dar es Salaam na Msuluhishi wa TOST, Robert Manyama, alipokutana na wadau wa kodi katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) wakati akitambulisha malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo. 

Amesema taasisi hiyo imeundwa na Serikali chini ya Wizara ya Fedha, ikiwa ni taasisi huru itakayokuwa na jukumu la kutoa usuluhishi wa malalamiko baina ya walipa kodi na wanaotoza ambao ni Mamlaka ya Mapato Tanzania-(TRA) ili kupunguza malalamiko ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu na kuwa  kikwazo kwa ulipaji kodi wa hiyari. 

‘‘Tunatoa uwanja huru wa mlipakodi kupata haki yake bila kuona kuwa anayetoa usuluhishi wa malalamiko yake ni yule yule aliyesababisha kutokea kwa malalamiko, lakini pia nitoe wito kwa wafanyabiashara wajitahidi kutunza kumbukumbu za biashara kwa usahihi ili kupata suluhu kwa kuzingatia ukweli na haki,’’amesema Manyama.

Amesema haki inaambatana na wajibu hivyo wafanyabiashara ni vema kutekeleza wajibu wao wakati taasisi ikiwa inashugulikia malalamiko yao kwa kutoa ushirikiano wakati wanapohitajika kutoa taarifa fulani ili kuwezesha mchakato kufanyika ndani ya muda uliowekwa. 

Manyama, amesema katika kuzuia malalamiko wanaendelea kutambua matatizo yaliyo ndani ya mfumo wa kodi yanayosababisha migogoro na kuyafanyia kazi ikiwemo kutoa mapendekezo ili kufanyike marekebissho ndani ya mfumo wa kodi. 

“Tutashughulikia malalamiko kama yalivyo ila nasisitiza tuwe wa kweli, tukiwa wa kweli tutatatua malalamiko na tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kupita mikoani ili kuweza kuwafikia katika maeneo yao,”amesema. 

Amesema kuwa taasisi hiyo inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kuwa hakuna namna itaingiliana na majukumu ya taasisi nyingine ya Serikali na kuwa Sheria iliyounda TOST imeipa uhuru wa kutokuingiliwa kiutendaji.

Nae Meneja wa Usajili wa Malalamiko na Taarifa za Kodi , Naomi Mwaipola amesema kuwa maoni yaliyotolewa na wadau kuhusu kushirikiana ili kuwa na taasisi imara, yatafanyiwa kazi ili kuwa na mazingira yatakayochochea ulipaji wa kodi kwa hiyari.

“Nawapongeza kwa michango yenu mliyotoa katika kikao hiki na tunaahidi kuwa itafanyiwa kazi na watumishi watatenda kazi kwa uadilifu ili kujenga imani ya wadau kwa taasisi kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla,”amesema Mwaipola.

Ameongeza kuwa wapo tayari kupokea malalamiko pamoja na maoni na kutoa rai kwa walipakodi kuanza kutumia huduma za taasisi hiyo na kuwa itawafikia walipakodi katika mikoa yote. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Hamisi Livembe ameipongeza Serikali kwa kuanzisha taasisi hiyo na kutoa rai ianzishe ofisi mikoani ili kuweza kuwafikia wafanyabiashara wengi wa kati ambao wako mikoani ili  changamoto zao za kikodi ziweze kushughulikiwa kikamilifu.

‘‘Waliopewa dhamana wawe na dhamira ya dhati kufanya kazi hiyo kwani ni kazi ngumu na waongeze uwazi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kulinda haki za walipakodi,” amesema Livembe.

TOST imekutana na wawakilishi wa wadau mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Chama cha Wasafirisha Mizigo Tanzania (TAFFA), Jumuiya ya Walipakodi pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya kodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles