26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tirdo wanadi maabara inayozuia upotevu wa umeme

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limewataka wenye viwanda na wafanyabiashara kutumia maabara za kupima na kutambua upotevu wa umeme ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi katika uzalishaji.

Maabara hiyo inamwezesha mtumiaji wa umeme kwenye majengo makubwa, viwandani na majumbani kupunguza matumizi ya nishati hiyo huku akiendelea kufanya uzalishaji.

Akizungumza Julai 9,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba, Mhandisi kutoka TIRDO, Paul Kimath, amesema wanahamasisha umma kutumia maabara hiyo kuepuka kuathiri matumizi ya nishati.

“Tunayo maabara kwa ajili ya jamii ambayo inatumika katika shughuli za kitafiti na kuhudumia Watanzania, kwenye viwanda vikubwa, majengo ya biashara na majumbani wataweza kutumia nishati kwa ufanisi zaidi na kupunguza upotevu. Tunatumia maonesho ya Sabasaba kuelimisha umma uweze kubadili tabia juu ya matumizi ya umeme ili kuepuka gharama zisizokuwa za lazima,” amesema Kimath.

Aidha amesema anayetaka huduma hiyo anapaswa kwenda TIRDO kisha wataalam watamtembelea kufanya tathmini na kumshauri jinsi ya kupunguza matumizi ya umeme.

Kwa mujibu wa mtaalam huyo, hatua zinazofanyika kwanza ni kukagua matumizi ya umeme ya mtumiaji husika, kupima kitaalam matumizi ya umeme kwa kutumia vifaa kisha kupanga mkakati wa jinsi ya kupunguza.

Amesema wanaweza kuboresha miundombinu au kufunga vifaa maalumu kuzuia upotevu na kumuelimisha mteja jinsi ya kusimamia matumizi yake ya umeme ya kila siku.

“Unapopunguza matumizi ya umeme haimaanishi kwamba utaathiri uzalishaji wa bidhaa au huduma unayoitoa, unapunguza matumizi ya nishati huku ukiendelea kutoa huduma bora zaidi kwa kutumia nishati kidogo.

“Kwenye viwanda kipo kifaa kinachopima matumizi ya umeme ya wakati wote ambacho kinatoa uwezo wa kujua matumizi makubwa na madogo yako wakati gani na ubora wa umeme unaotumika hivyo, upotevu wowote unaofanya kwenye kiwanda iwe kwenye mifumo au vifaa vinavyotumika kunasababisha matumizi ya umeme kuwa mabaya. Ndio maana tumekuja na maabara kuwasaidia wadau wetu wenye viwanda vikubwa kujua hatua za kupunguza umeme bila kuathiri matumizi yao ya kila siku,” amesema.

Amesema nishati inachangia kwa kiasi kikubwa bei za bidhaa kuwa juu hivyo kwa kutumia maabara hiyo kutapunguza gharama za uendeshaji na kuokoa upotevu wa umeme.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles