28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Msigwa awakaribisha wawekezaji wa Urusi kuchangamkia fursa Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, ametoa wito kwa wafanyabiashara na sekta binafsi za Urusi kuja kuchangamkia fursa nyingi ambazo bado hazijatumika Tanzania.

Msigwa ameyasema haya Julai 10, 2024, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano baina ya wafanyabiashara wa Urusi na Tanzania kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa, ikiwa ni siku maalumu ya Urusi.

Msigwa amesema kuwa kuna maeneo mengi ya kuwekeza nchini na amewaomba wawekezaji kutoka Urusi kuja na kushirikiana na serikali ya Tanzania. “Serikali imeamua kufanya hivyo ili kutengeneza jukwaa zuri zaidi la namna nchi hizi zinaweza kushirikiana katika biashara na uwekezaji,” alisema Msigwa.

Akizungumza kuhusu uwiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Urusi, Msigwa alisema, “Uwiano wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili hauko sawa. Tanzania inauza bidhaa zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 6.4 kwa Urusi, lakini Urusi inauza bidhaa Tanzania zenye thamani zaidi ya dola za Kimarekani milioni 179. Maana yake wao wanapata zaidi, sisi tunapata kidogo.”

Msigwa aliongeza kuwa Tanzania bado inahitaji uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, madini, biashara, utalii, na maeneo mengine. Serikali imeweka utaratibu mzuri kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kurahisisha uwekezaji huo. Alisema pia kuwa teknolojia ni muhimu na kwamba Tanzania inakabiliwa na changamoto ya teknolojia ndogo katika uzalishaji.

Kwa upande wake, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrew Avetisyan, alisema kongamano hilo ni muhimu kwa wafanyabiashara wa nchi zote mbili kubadilishana uzoefu na fursa za uwekezaji. Alisisitiza kuwa Urusi na Tanzania wamekuwa na ushirikiano mzuri na maonesho hayo yatatumika kuonesha bidhaa mbalimbali za nchi hizo.

“Tupo tayari kusaidia wafanyabiashara wa Tanzania na kufanya uwekezaji nchini, pamoja na kubadilishana uzoefu na ujuzi katika masuala mbalimbali,” alisema Avetisyan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles