25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

TARI KUJA NA TEKNOLOGIA MPYA KILIMO CHA PAMBA

 PAMBA (dhahabu nyeupe), zao ambalo limeendelea kuzalishwa na wakulima zaidi ya 500,000 katika mikoa 17 ya Tanzania bara, changamoto kubwa ikibaki katika kuongeza tija.

Kila wakati wadau ikiwemo serikali wamekuja na teknologia mbalimbali katika zao hilo ambazo zimekuwa zikilenga kuongeza tija na kumwongezea kipato mkulima ili aweze kunufaika na zao lake. 

Kwa muda mrefu zao la pamba limekuwa na teknologia moja tu katika vipimo vya upandaji wa mbegu, teknologia ambayo watalamu wa kilimo wanaeleza kuwa imepitwa na wakati kutokana na kukaa muda mrefu. 

Teknologia hiyo ya vipimo iliyokuwa ikitumika katika upandaji wa mbegu ni Sentimeta 90 kwa Sentimeta 40 (mstari na mstari sentimeta 90 pia mbengu na mbegu sentimeta 40). 

Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo chake cha utafiti Ukiriguru kilichopo mkoani Mwanza, inasema kuwa teknologia ya 90 kwa 40 imetumika kwa muda mrefu lakini bado haijamkomboa mkulima. 

Mkurugenzi wa utafiti na ubunifu kutoka taasisi hiyo Evelina Lukonge anasema kuwa mabadiliko ya tabia nchi yameifanya teknologia hiyo ya zamani kupitwa na muda na kushindwa kumsaidia mkulima. 

Kutokana na hali hiyo taasisi hiyo ya utafiti nchini kupitia Ukiruguru inaendelea na utafiti wa teknologia mpya nne za vipimo vya upandaji wa mbegu za zao hilo. 

Mkurugenzi huyo wa anasema kuwa utafiti wa teknologia hizo mpya unaoendelea ulianza mwaka 2017 na utakamilika mwaka 2020, kwa kushirikiana na nchi ya Brazil. 

“ Nchi ya Brazil imekuwa kinara wa uzalishaji wa pamba duniani kwa muda mrefu na katika kilimo chao wamekuwa wakitumia teknologia hizo ambazo tunazifanyia utafiti kwa kushirikiana na wao,” 

Mkurugenzi huyo anasema kuwa wakulima wengi wa pamba nchini wamekuwa wakilima mashamba makubwa lakini mavuno wanapata kidogo hali ambayo inasababisha wabaki katika umaskini. 

“ Mkulima analima hekari tano mpaka saba, lakini mavuno ambayo anapata ni kidogo sana, wengi wamekuwa wakiingia hasara…wanatumia nguvu kubwa na gharama nyingi lakini wanachokipata hakiendani na ukubwa wa eneo,” anasema Lukonge. 

Mtaalamu huyo wa utafiti na Ubunifu anasema kuwa juhudi ambazo zinafanywa na TARI kwa kushirikiana na nchi ya Brazil kupitia shirika lake la maendeleo (ABC) wanafanyia kazi teknologia hizo nne. 

“ Kupitia mradi wa Cotton Victoria tuna uhakika wakulima wa pamba wanaenda kupata suruhisho la kupata tija kubwa kwenye eneo dogo, teknologia hizo zitamfanya mkulima mwenye hekari moja kupata mazao ya mtu mwenye hekari mbili hadi tatu aliyetumia njia ya zamani,” anaeleza Lukonge. 

Robert Ngumuo ni Mtafiti kutoka TARI Ukiriguru anasema kuwa teknologa ambazo wanazifanyia utafiti ili kuzileta kwa wakulima, zinataweza kuwakomboa na kuwapunguzia gharama za uzalishaji. 

Ngumuo anasema taasisi hiyo inakuja na teknologia ambazo zinaongeza idadi ya mimea katika shamba, ambapo matumizi ya mbolea likiwa jambo la muhimu katika kuongeza lishe na mmea. 

Ngumuo anazitaja teknologia hizo mpaya ambazo TARI inazifanyia utafiti kuwa ni Sentimeta 50 kwa Sentimeta 30 (mstari na mstari sentimeta 50, mbengu na mbegu sentimeta 30), Sentimeta 60 kwa 30. 

Nyingine ni vipimo vya Sentimeta 70 kwa 30, pamoja na Sentimeta 80 kwa 30 “ Lakini pia vipimo hivyo vinaweza kubadilika vikawa Sentimeta 50 kwa 16.67, 60 kwa 16.67, 70 kwa 16.67 pamoja na 80 kwa 16.67” 

 anasema Ngumuo. 

Mtafiti huyo anasema kuwa kwenye teknologia zote hizo, lengo lake kubwa ni kuongeza mazao shambani, kwani wameona matumizi ya teknologia ya zamani 90 kwa 40 imekuwa ikiacha nafasi kubwa na kufanya mazao kuwa machache shambani. 

“ Kwenye Hekta moja yenye hekari moja na nusu kwa kutumia teknologia hizi mpya, mkulima akipanda mbegu atakuwa na miche 71,000 na ataweza kuvuna kg 700 hadi 800 kwenye hekari moja,” anasema Ngumuo… 

“ Kwa sasa wakulima wengi katika hekari moja wanazalisha siyo chini ya kg 350 hadi 400, lakini walio wengi wanazalisha chini ya hapo, anasema Ngumuo. 

Dkt. Paul Saidia Mtafiti kutoka TARI Ukiriguru anasema kuwa katika teknologia hizo mpya, suala la mbolea ni muhimu sana kwani itafanya mazao yakue kwa ustawi mzuri zaidi. 

Dkt Saidia anasema kuwa katika mashamba wanayofanyia utafiti wamekuwa wakitumia mbolea za kisasa, ikiwemo ya Urea na mbolea ya kukuzia ili mmea uweze kuwa na afya nzuri ya kuzaa matunda ya kutosha. 

“ Kwa kutumia mbolea kila mche mmoja wa pamba anatakiwa kuwa na vitumba kuanzia 20 na kwenda juu, lakini ukifanya vizuri na kufuata kanuni zote mche unaweza kubeba vitunda hadi 40 hata mbolea ya samadi ni sahihi kwa matumizi,” anasema Dkt. Saidia. 

Watalaamu hao wa wa kilimo wanasema endapo wakulima wataweza kutumia njia itakayopendekezwa na mara baada ya utafiti, watapata mazao mengi katika eneo dogo na kuwapunguzia gharama za uzalishaji na muda. 

WAKULIMA. 

Wakulima wa Mkoa wa Simiyu na Mwanza walioko katika utafiti huo, wanasema kuwa wamejaribu katika mashamba yao na kuona teknologia hizo ni nzuri na muhimu sana kwao. 

Wanasema kuwa kwa kufuata kanuni za upandaji wa vipimo vipya vya sentimeta 80 kwa 30, 70 kwa 30, 60 kwa 30 na 50 kwa 30 mavuno yanakuwa mengi tofauti na ilivyokuwa mwanzo. 

“teknolojia hii inaongeza mavuno yanakuwa mengi kwa sababu kunakuwa na miche mingi ya pamba katika eneo dogo,” alisema Omar Sayi Mahuga mkulima ambaye shamba lake limetumika katika utafiti. 

Sayi anasema kuwa wakati anaandaa shamba alitenga robo ya hekari moja, na kwenye eneo hilo la robo alitumia teknologia hizo mpya ambapo yeye alitumia 70 kwa 30 na alitumia mbolea ya samadi. 

“ Nilichokiona ni kama maajabu, kwenye hii robo pamba imekuwa nzuri sana na nyingi jambo la ajabu katika mavuno pamba ambayo nimevuna kwenye robo imelingana na ile ambayo nimevuka katika kipande kingine kilichokuwa kimebaki ambacho nilitumia teknologia ya zamani 90 kwa 40,” anaeleza Sayi. 

Naye Martine Kaganda Mkulima kutoka Kwimba Mwanza, anasema kuwa teknologia hizo mpya zitakuwa mkombozi mkubwa wa wakulima wa pamba, kwani wataweza kulima eneo dogo na kupata mazao mengi. 

“ Tunachokiomba Teknologia hizi mpya ziwafike wakulima wengi vijijini, zinaonekana kuwa bora, na sisi wakulima tunaenda kuwaeleza na kuwaelimisha, tunaomba ziletewe vijijini,” anaeleza Kaganda. 

Hata hivyo TARI kupitia Ukiruguru wanaendelea na utafiti wa teknologia hizo katika Mikoa ya Geita, Simiyu na Mwanza na mwisho wa utafiti huo mwaka 2020 ndiyo watapendekeza teknologia moja kutumika. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles