TUMESIKIA kupitia vyombo vya habari kuwa Serikali ya Tanzania iko mbioni kujitoa katika mpango wa uendeshaji shughuli za Serikali kwa uwazi.
Suala hili haliko wazi na ndio maana tungependa kuelewa iwapo ni kweli au la. Rais wa awamu ya nne, Rais Jakaya Kikwete aliunga mkono dhana ya uwazi na ukweli serikalini iliyoibuka wakati huo.
Dhana hii iliwezesha Tanzania kuingia katika mpango wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi. Mpango huu kwa lugha ya kigeni unaitwa Open Government Partnership (OGP).
Mpango huu ni mkakati ulioanzishwa rasmi Septemba mwaka 2011, pale Serikali za nchi nane anzilishi zilipoafiki mpango huo na kuweka bayana mpango wa utekelezaji wa nchi zao. Nchi hizo ni pamoja na Brazil, Indonesia, Mexico, Norway, Ufilipino na Afrika Kusini.
Baada ya nchi hizi kuafiki mpango huu zilialika nchi nyingine duniani na hadi sasa nchi zipatazo 75 zilishaafiki. Tanzania iliafiki mwaka huo huo wa 2011 na ikawa nchi ya pili barabani Afrika kujiunga na mpango huo kufuatia Afrika Kusini.
Huu mpango una nia ya kupata ahadi za Serikali kuwa zitakuza na uwazi, zitajenga uwezo wa raia wake, zitapambana na rushwa na kuhuisha teknolojia mpya ili kukuza utawala bora.
Ili nchi iwe sehemu ya mpango huu inabidi ikubali kuridhia azimio la Serikali yenye uwazi na ionyeshe mpango kazi wake katika kutimiza mpango huo. Mpango umekuwa na nia ya kuwaunganisha au kuwaweka karibu au pamoja watendaji wa serikali na wale wana jamii hasa mashirika ya kijamii ili kufanya kazi kama wabia wa kweli katika ngazi ya kitaifa na hata kimataifa.
Kwa hiyo hata katika kuandaa mpango kazi, Serikali hukaa na mashirika ya kijamii kuuandaa. Serikali zimeshauriwa kujaribu kurasimisha mpango huu ili kuwepo na mawasiliano endelevu na mashirika ya kijamii.
Ndani ya mpango huo kuna timu ya mashirika ya kijamii ambayo kazi yake ni kukuza jamii ili ishiriki katika mpango huu. Timu hii kazi yake huwa katika ngazi ya kitaifa kuwasaidia wana jamii kuwa sehemu ya mpango huu ili kufikia malengo watakayojiwekea ambayo ni pamoja na uhuru wa habari, uwazi katika data, uwazi katika bajeti, ardhi na uchimbaji wa madini.
Tanzania ilishafika mbali katika kuweka miundombinu kama vile mpango wa utekelezaji ambapo mpango kazi uliokuwa unashughulikiwa sasa ni wa tatu baada ya ile miwili ya kwanza kumaliza muda wake. Pia Rais wa awamu ya nne alifanikisha mkutano uliofanyika mwaka 2015 miezi michache kabla ya kuondoka madarakani. Mpango huu bado haujafahamika sana wa jamii kama makusudio yake yalivyo, lakini hatua ya kwanza ilikuwa uwepo wake na upo. Nia ya mpango huu ni njema kwa vile ukiweza kutekelezeka kikamilifu nchi inaweza kuondokana na ukiritimba wa usiri kati ya Serikali na wanachi wake.
Kama tunavyojua Serikali ipo kwa ajili ya wananchi wake. Chochote Serikali inachofanya ni kwa ajili ya wananchi wake iwapo Serikali hiyo si ovu au yenye nia ovu.
Tunaposikia hizo tetesi ambazo zinapaswa kuwekwa wazi, inatia shaka iwapo kweli Serikali ilioingia kwenye mpango huu inataka kughairi wakati huu. Wakati huu wa Serikali hii inayopambana na rushwa na kujibidiisha kutaka kurudisha rasilimali kwa watanzania si wakati muafaka kabisa kujiondoa katika mpango huu.
Katika maelezo yaliyoonekana katika moja ya magazeti yupo msemaji kutoka serikalini aliyenukuliwa akisema kuwa kujitoa huko kutakuwa ni kwa muda tu ili Serikali ijiangalize iwapo mpango huu una tija.
Hoja iliyopo ni kuwa iweje Serikaili iwe haifahamu mpango huu hadi ijitoe na iwe nje kuuchunguza? Ninavyoelewa ni kuwa hadi Serikali ikaukunbali huu mpango na kutengeza mipango kazi kufikia mitatu ilikuwa imefanya uchambuzi na kuuona uafaa.
Pia ni sawa kujiangaliza lakini si kwa kujitoa kisha kurudi. Kwa vile mpango ulikuwa katika kutekelezwa kitu ambacho kingefanyika wakati wa kuandaa mpango kazi wa pili au wa tatu ingefaa kufanya tathimini kuona iwapo mpango huo unafaa au haufai na kama unafaa ni zipi changamoto na zinaweza kutatuliwa vipi.
Ni uwazi usiopingika kuwa Serikali iliingia haraka katika mpango huo na tumeona wadau wakieleza wengi wa watekelezaji serikalini waliuona mpango huu kuwa kitu cha kigeni.
Yaani ulikuwa kama ni mpango uliotoka juu kuwashukia watu wasiouelewa na wasioweza kuufanyia kazi. Yapo mengi ya aina hii, lakini nikiangalia nia na dhamira ya mpango huu ilihitajika hamasa tu kwa watekelezaji ili waelewe umuhimu wa mpango na jinsi ambavyo ungeweza kurahisisha utendaji wa serikali na kuifanya jamii kuwa karibu zaidi na Serikali yao.
Kwa jinsi Serikali inavyofanya kazi na kwa hali ya usiri hata kwa masuala yanayopaswa kuwa wazi mpango huu, ukisitishwa utarudisha nyuma juhudi zote ambazo tayari zilishaanza na pia itakuwa ni vigumu sana kuurejeshwa na ukaweza kushika kasi kama unavyotegemewa.
Nadhani huu mpango umefanana sana na kauli za Rais wa awamu hii ambaye ana mipango kabambe ya kupambana na rushwa. Tukirudi kwenye huo usiri wa ‘sirikali’ mafanikio katika eneo hilo yatakuwa yamezorota.
Suala la mikataba ya madini kutokuwa wazi na hatimaye kugundulika kuwa ina mapungufu katika kuiletea nchi maendeleo yatapungua kama si kuondoka kabisa. Sasa hivi raia wana uchu mkubwa wa kujua kikao cha kujadili makinikia kimefikia wapi na wajumbe wa Tanzania katika kamati hiyo ukimwacha waziri ni nani?
Majibu hayapo na ukweli ni kuwa yote hayo yanafanyika kwa manufaa ya jamii hii . Hali hii ni wakati tuko katika mpango na sera ya uwazi tukijitoa si ndio usiri utazidi na matokeo si mazuri. Wana jamii hupenda sana kuelezea mambo kwa kuwazia tu pale wanapokuwa hawayajui. Hii ni hatari kwani yawazwayo husambazwa yakafanana na ukweli. Huu mpango ungeboreshwa zaidi ili wana jamii wapate taarifa sahihi na kwa wakati muafaka nao wawe tayari kutoa taarifa sahihi na muafaka kwa wakati muafaka . Hapo tutakuwa tunamaanisha kuingia kwenye mpango wa uendeshaji shughuli za Serikali kwa uwazi na dhana ya UWAZI na UKWELI itapata nguvu ndani ya Jamii.
Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).