28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

ICC ILIUNDWA KWA AJILI YA BARA LA AFRIKA TU?

NA HILAL K SUED


Ingawa lengo la kuundwa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (International Criminal Court – au ICC) ilikuwa ni kutumika kwa dunia nzima, lakini kinachoonekana hadi sasa hivi ni kwamba chombo hicho ni kwa ajili ya nchi za Bara la Afrika tu.

Sasa hivi chombo hicho si cha kimataifa kamwe – hivyo ni sahihi kabisa kingeitwa Mahakama ya Afrika ya Makosa ya Jinai (African Criminal Court – au ACI). Hii inatokana na ukweli kwamba tangu kuundwa kwa Mahakama hiyo na kuanza kazi mwaka 2002 watuhumiwa wote 31 waliofunguliwa mashitaka katika mahakama hiyo ni wa kutoka Bara la Afrika.

Hao ni pamoja na Charles Taylor, aliyekuwa mbabe wa kivita wa Liberia ingawa huyu awali alishitakiwa katika mahakama maalum iliyoundwa mwaka 2000 kwa makubaliano kati ya serikali ya Sierra Leone na Umoja wa Mataifa na baadaye mwaka 2006 kesi yake ilihamishiwa ICC. Mahakama hii iliundwa kwa lengo la kusikiliza kesi za watuhumiwa waaliotokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone.

Kati ya wote hao, watuhumiwa 10 (pamoja na Taylor) wanashikiliwa katika gereza la Scheveningen karibu na The Hague (mji mkuu wa Uholanzi) na waliobaki ama wako nje kwa dhamana au hawajakamatwa bado ingawa hati za kukamatwa kwao imeshatolewa.

Watuhumiwa hawa wanatoka katika nchi za Sudan, Congo-DRC, Uganda, jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR)Libya na Liberia.

Orodha ya watuhumiwa hawa isichanganywe na ile ya watuhumiwa wengine waliotoka nje ya Bara la Afrika, ambao kesi zao zimekuwa zikiendelea hapo hapo The Hague, hususan wale waliotokana na vita ndani ya iliyokuwa Yugoslavia.

Hawa walifunguliwa mahakama yao maalum iitwayo Mahakama ya Jinai ya Kimataifa kuhusu Yugoslavia (International Criminal Tribunal for the former Yugoslavia – ICTY) kwa ajili ya kuwafungulia mashitaka wahalifu wa kivita wakati wa vita nchini Yugoslavia. Mahakama hii isiyo ya kudumu iliundwa na wa Umoja wa Mataifa chini ya Azimio Na. 827 la Mei 25 1993 na ilimaliza kazi zake mwaka 2014.

Kama nilivyoeleza hapo juu ICC haina uhusiano mahakama ile nyingine maalum ya watuhumiwa waliotokana na vita nchini Sierra Leone, au ile Mahakama ya Maalum ya Kimataifa kuhusu Rwanda (ICTR) iliykuwa Arusha kuhusu watuhumiwa waliotokana na mauaji ya Rwanda ya mwaka 1994, na ambayo ilimaliza shughuli zake mwaka 2015.

Au hata ile ya Cambodia iliyoundwa mwaka 2003 kwa makubaliano kati ya nchi hiyo na Umoja wa Mataifa kuhusu wahalifu wa mauaji ya kimbari wa uliokuwa utawala wa Khmer Rouge kati ya mwaka 1975 na 1979.

Mahakama inayolalamikiwa kwa ubaguzi wa wazi wazi dhidi ya watu wa Afrika ni hii ya kudumu – ICC – ambayo iliundwa kutokana na mkutano wa nchi 116 za kimataifa huko Roma, Italia mwaka 1998, mkutano ambao ulizaa dhamira ya makubaliano ya kimsingi yanayojulikana kama  Rome Statute ili kuunda Mahakama hiyo ya kudumu, ambayo ilianza kazi rasmi mwaka 2002.

Lengo la mahakama hiyo ni kuwafungulia kesi za jinai watu mbali mbali wanaotuhumiwa makosa mauaji ya kimbari, makosa dhidi ya ubinadamu, makosa ya kivita, na makosa ya kufanya uvamizi wa kivita. Dhamira yakuwepo kwa mahakama ya aina hii ya kudumu ilianza tangu baada ya Vita vya Pili, wakati mahakama maalum ya kimataifa iliundwa kuwashitaki wababe waliosababisha vita hiyo – akina Hitler na wenzake.

Hadi kufikia mwaka 2016 nchi 116 ni wanachama wa ICC, ikijumlisha nchi zote 26 za Amerika ya Kusini, nchi 43 za Ulaya, nchi 32 za Afrika na nchi 15 za Asia. Jumla ya nchi 34 (ikiwemo Russia) zilizotia saini makubaliano ya Roma zimekataa kuridhia (ratify) mkataba.

Nchi nyingine nne, Marekani, Sudan Burundi na Israel zimejitoa kabisa katika mkataba na zimezikana saini za wawakilishi wao walizoweka katika mkataba hapo awali.

Hivyo basi jumla ya nchi 45 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa ama hazikutia sahihi mkataba wa Mahakama hiyo, au kuuridhia, zikiwemo China na India ambazo zinapinga uwepo wa Mahakama hiyo.

 

Kwa upande wake Marekani ilishiriki katika mchakato wote wa awali wa kufikia mkataba wa ICC wakati wa Rais Bill Clinton, lakini utawala wa mrithi wake wa Rais George W. Bush uliamua kujitoa mwaka 2001.

Wakati anatangaza kujitoa Bush alizionya nchi ambazo zitathubutu kuwakamata na kuwatoa raia wa Marekani kwa ajili ya kushitakiwa katika Mahakama hiyo.

Wakati wa mchakato wa Mkataba Marekani yenyewe ilipinga vikali kuwepo makosa ya kufanya kuingilia kibabe nchi nyingine (aggression) na kipengele hicho kiliahirishwa kuwekwa hadi hapo itakapofika 2017. Hivyo basi ilivyofanya Marekani dhidi ya Iraq si lololte au chochote chini ya Mahakama hiyo.

Lakini kama nilivyotaja hapo juu Mahakama hii imekuwa ikiwaandama watu wa kutoka Bara hili, na mtu anaweza akadhani kwamba ni watu au viongozi wa Bara hili tu ndiyo ambao peke yao wanafanya makosa ya uhalifu wa kivita duniani hapa.

Kwa mfano Kipengele Na. 8(a) (i-viii) cha Mkataba wa ICC kinachoorodhesha makosa ya kivita (war crimes), baadhi yake yakiwa ni kuua raia kimakusudi, kumtesa au kumdhalilisha binadamu, kumpa maumivu makubwa hadi kumharibu afya au maungo ya mwili wake, uharibifu mkubwa usio wa lazima kwa mali na miundominu, kuwakamata na kuwahamisha kwa nguvu watu na baadaye kuwaweka kizuizini bila kufuata sheria n.k.

Hapa ndipo utaona kwa nini Marekani, taifa linalojigamba kuwa ni la kistaarabu kuliko yote ilijitoa katika mkataba huo mwaka 2001. Karibu makosa yote hayo Marekani huwa inayafanya kwa watu wa nchi nyingine hasa zile dhaifu au mahasimu wake.

Karibu vitendo vyote hivi vya jinai Marekani imevifanyia dhidi ya nchi ya Iraq ilipoivamia bila sababu za msing au za kisheria mapema mwaka 2003. Kwa mfano, kwa amri ya Jemadari Mkuu wa majeshi ya Marekani George W. Bush vikosi vya jeshi la anga la nchi hiyo vilidondosha mabomu katika mji wa Falluja mwishoni mwa 2004 na kuuwa mamia ya watu wasio na hatia wakiwemo watoto na wanawake.

Lakini hadi leo hii ICC inaonyesha upofu mkubwa kwa uhalifu aliofanya Bush na Tony Blair huko Iraq, ingawa ilikuwa rahisi kwa mahakama kuubaini ‘uhalifu’ wa Hassan Al-Bashir, Rais wa Sudan kwa kutenda uhalifu huko Darfur, uhalifu kama ule ule wa Bush huko Iraq.

Kuhusu mateso kwa binadamu kwa mfano, askari wa Bush waliwatesa na kuwadhalilisha wafungwa wa Iraq waliokuwa wakishikiliwa katika gereza la Abu-Ghraib mwaka 2004. Sidhani iwapo akina Uhuru Kenyatta au William Ruto walifikira kufanya unyama kama huo huko Kenya.

Huko Sri Lanka nako katika miezi ya mwisho mwisho ya vita yao ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2009, majeshi ya serikali yaliuwa maelfu ya raia wasiokuwa na silaha, wengine wakiwa wamechukuwa hifadhi mahosptalini, kufuatana na ripoti za waandishi wa habari wa nchi za magharibi.

Lakini pale Umoja wa mataifa ulipotoa wito wa kuunda tume ya kuchunguza mauaji hayo, serikali ya Sri Lanka iliitolea nje, ikihoji mbona haikufanya hivyo kwa Marekani kuhusu mauaji ya Iraq?

Utata mwingine unakuja pale Marekani, ingawa ilijitoa kabisa katika Umoja huo, bado inajiweka kimbelembele sana kuhusu uendeshaji wa ICC.

Kwa mfano ili mtuhumiwa akamatwe Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC lazima atoe hati ya kukamatwa, na hizi huzitoa kutokana na mojawapo ya mambo haya: iwapo ataombwa na nchi mwanachama, au ataombwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, au ataombwa na ICC yenyewe baada ya kupata taarifa kutoka vyanzo mbali na baada ya yenyewe (Mahakama) kufanya uchunguzi wake wa awali na kuridhia.

Kwa kuwa Marekani haiitambui ICC lakini ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mwenye ushawishi mkubwa sana, na kwa kuwa Sudan na Marekani hawaivi, basi suala zima la Baraza hilo kumuomba mwendesha mashitaka mkuu wa ICC kutoa hati ya kukamatwa kwa Al-Bashir hakukai sawasawa kimasilahi.

Kwa kifupi, ICC ni mahakama inayolinda masilahi ya nchi za magharibi tu na maswahiba zao.

Mahakama ya ICC iliyopo The Hague, Uholanzi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles