26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tanesco yawataka wananchi kuweka mitengo ya radi

ELIZABETH KILINDI – NJOMBE

WANANCHI wilayani Makete katika Mkoa wa Njombe, wametakiwa kuweka mitego ya radi katika makazi yao kutokana na hali ya matukio ya radi ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na kugharimu maisha ya watu.

Ushauri huo ulitolewa jana na watalamu kutoka Shirika la Umeme nchini (Tanesco), waliofanya ziara wilayani humo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi pamoja na wananchi juu ya utunzaji wa miundombinu ya umeme na usalama.

Ofisa Masoko Tanesco Makao Makuu, Sirivester Matiku alisema elimu hiyo inakwenda sambamba na utunzaji wa mazingira pamoja na miundombinu ya nishati hiyo kwa kuwa vijiji hivyo vitapatiwa umeme kwa mara ya kwanza.

Alisema Tanesco inawaelimisha wananchi kutambua utofauti kati yake na wakandarasi wa REA, ili wajue majukumu ya pande zote ambapo itasaidia kuepusha migongano wakati wa utekelezaji majukumu. 

“Ambacho tunakifanya katika Wilaya ya Makete, ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na masuala ya umeme tunataka wananchi wajue namna ya kutumia umeme kwa faida na sio kwa hasara pamoja na kuwasaidia kutambua watu wasio waaminifu maarufu kama vishoka,”alisema Matiku.

Alisema mwitikio wa wananchi kuhitaji umeme wilayani humo, umekuwa mkubwa kwa kuwa wananchi wengi katika vijiji vinavyotarajia kunufaika na umeme wameshafanya maandalizi ya kusuka nyaya katika nyumba zao.

Vijiji 29 wilayani Makete vinatarajia kupata umeme kupitia mradi wa REA, ambapo timu ya watalamu ilitoa elimu katika kata nne za Bulongwa, Luwumbu Tandala na Tupalilo ambapo Matiku aliwataka wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za kusuka waya katika nyumba zao kutumia kifaa cha umeme tayari ‘Umeta’ ambacho kinapatikana katika ofisi za Tanesco kwa gharama ya Sh 36,000 kinachofaa kwa nyumba yenye vyumba vichache.

Aliwataka wananchi kukamilisha uingizaji wa umeme katika nyumba zao kabla ya mradi kuisha ifikapo Juni mwaka huu, pamoja na kutumia vifaa vyenye ubora ili kuepuka madhara ikiwemo nyumba au vifaa kuungua mara kwa mara.

“Nawashauri ndugu zangu wananchi msipende kutumia vifaa vya gharama nafuu katika nyumba zenu kwa kuwa mtapata hasara ya kuunguza vyombo vyenu jitahidini kutumia vifaa bora,”alisema.

Mmoja wa wananchi akiwemo Jihekela Soveli alilalamikia baadhi ya maeneo ya vitongoji kutofikiwa na miundombinu ya umeme katika awamu ya kwanza, lakini pia aliipongeza serikali kwa kufanikisha umeme kufika vijijini kwa kuwa umeanzia katika taasisi binafsi na serikali ambazo zinawanufaisha wananchi wote huku wao wakisubiri awamu nyingine.

Msimamizi wa miradi ya REA mkoani Njombe, Mhandisi Yusuph Salimu alisema zoezi la usambazaji wa umeme wilayani Makete linaenda vizuri licha uwepo wa changamoto za mvua nyingi huku akiwataka wakazi wa Makete kuendelea kuingiza umeme katika nyumba zao mpaka ifikapo Juni mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles