28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Tanesco yamwaga ajira

ANDREW MSECHU

SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco) limetangaza ajira 596 kwa nafasi mbalimbali, zinazotakiwa kujazwa kupitia utaratibu wa usimamizi wa Sekretarieti ya Utumishi wa Umma.

Ajira hizo zilitangazwa rasmi Julai 31 kupitia tangazo lenye kumbukumbu namba Ref.No.EA.7/96/01/J/54, likieleza kuwa kwa niaba ya Tanesco, Sekretarieti hiyo inawatangazia Watanzania wenye stadi na vigezo husika kujitokeza kujaza nafasi hizo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Sekretatrieti ya Ajira, ajira hizo zimetangazwa katika maeneo 32 ndani ya shirika hilo, zikihitaji watu wenye uzoefu kazini na wale wasio na uzoefu, ambao watahitajika kujifunza moja kwa moja wakiwa kazini kulingana na ujuzi walio nao.

Akizungumzia ajira hizo, Waziri wa Utumishi Wa Umma, George Mkuchika alisema zimetangazwa rasmi kupitia Sekretarieti ya Ajira kwa kuwa ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia ajira zote za watumishi wanaotakiwa kulipwa mshahara na Serikali.

Alisema kutokana na utaratibu uliopo, Sekretarieti hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza ajira, kufanya uchambuzi na kufanya interview (mchakato wa mahojiano) na kisha kutoa majina ya walioteuliwa na kupewa nafasi ya kupata ajira hizo.

“Sekretarieti ndiyo inayohusika moja kwa moja, kwa hiyo ndiyo inayosimamia mchakato wote, isipokuwa kuna baadhi ya nafasi, hasa za ngazi za juu ambazo Bodi za Taasisi husika ndizo zinazofanya usahili,” alisema.

Nafasi zilizotangazwa

Kwa mujibu wa taarifa ya Sekretarieti ya Ajira, zinawahusu wahasibu 12 watakaokuwa mafunzoni, wahasibu wasaidizi 25 na Wahandisi na Wabunifu wawili.

Pia wanatakiwa mafundi mchundo (uashi) mmoja, mwanafunzi mchundo (umeme) mmoja, mafundi mchundo 232 katika maeneo mengine manne.

Wawakilisjhi wa huduma kwa wateja wanatakiwa wawili, msimamizi wa mifumo ya mawasiliano, walimu wawili wa kituo cha kutunzia watoto, madereva 43 wa daraja la II, mtaalamu wa uchumi mmoja, mwanafunzi na mhandisi mwanafunzi katika masuala ya uhandisi wa vifaa.

Wengine ni mtaalamu wa nishati ya maji mwanafunzi, mtaalamu wa usalama wa Teknolojia ya Mawasiliano, mtaalamu mwanafunzi katika masuala ya mtandao wa mawasiliano, wauguzi wawili, ofisa ulinzi mmoja, wahudumu 14 wa stoo, wahudumu wasaidizi 50 wa stoo, maofisa wawili wanafunzi wa stoo na maofisa ugavi wasaidizi 15.

 Wengine ni mafundi umeme saba, mafundi 25 wa mifumo ya umeme, mafundi watatu wa mifumo ya friji na upoozaji, maofisa 21 wanafunzi katika usafirishaji, maofisa wawili wanafunzi katika manunuzi, maofisa wanne wanafunzi katika masuala ya stoo, maofisa ugavi wanafunzi watano na ofisa usimamizi wa ukaguzi wa vifaa mwanafunzi.

Mwelekeo wa Tanesco

kwa mujibu wa tangazo hilo la Sekretarieti ya Ajira, hatua hiyo ya Tanesco ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Tanzania 2025 unaotarajia kuifanya nchi iwe ya kipato cha kati ifikapo 2025.

Inamaanisha kuwa Pato la Taifa kwa kichwa litaongezeka kutoka dola 640 hadi angalau dola 3,000 ifikapo 2025.

Inaeleza kuwa ili kufikia lengo hilo, unahitajika ukuaji wa uchumi wa haraka ambao lazima uongezwe na vifaa vya umeme vya kutosha, vya kuaminika, vya gharama nafuu na mazingira rafiki ya upatikanaji wa umeme.

“Kwa hivyo Uwezo wa uzalishaji unahitaji kuongezeka kutoka MW 1,583 hadi angalau MW 10,000 ifikapo 2025. Pia kuongeza viwango vya uunganishwaji umeme kutoka asilimia 24 uliorekodiwa mwaka 2014 hadi angalau asilimia 50 na viwango vya ufikiaji kutoka asilimia 36 hadi angalau asilimia 75 ifikapo 2025,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Linaainisha kuwa kwa mtazamo ya maono hayo, Serikali, kupitia maagizo mbalimbali, imeiagiza Tanesco kukagua muundo wake wa shirika ili kutimiza malengo ya 2025, hivyo katika kutekeleza majukumu yake ya msingi  shirika hilo linaongozwa na Sera ya Taifa ya Nishati ya 2003 na Sheria ya Umeme ya mwaka 2008.

Tangazo hilo linaeleza kuwa Tanesco inafanya kazi chini ya mwongozo wa udhibiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) iliyoanzishwa na Sheria ya mwaka 2001 na kwa kufuata maagizo hapo juu,  imekuja na muundo ambao unapunguza gharama za kiutendaji bila kuathiri utendaji na ufanisi.

Hatua hiyo imeelezwa kuzingatia pia ajenda ya kitaifa ya viwanda ambayo inakusudia kubadilisha uchumi wa Tanzania kuwa kipato cha kati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles