26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Kenyatta apokea tausi aliopewa na Magufuli

NAIROBI, KENYA

RAIS Uhuru Kenyatta wa Kenya  amepokea zawadi maalumu ya tausi wanne kutoka kwa Rais John Magufuli.

Ndege hao wa kuvutia walifikishwa Ikulu ya Nairobi jana asubuhi  na balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Pindi Chana ambaye pia alifikisha  ujumbe mwingine wa heri kutoka kwa Rais Magufuli.

Rais Kenyatta alipewa ndege hao katika ziara binafsi aliyoifanya hivi karibuni nyumbani kwa Rais Magufuli Chato, ikiwa ishara ya heshima kwa kiongozi huyo wa Kenya.

Akizungumza wakati akipokea tausi hao wanne, Rais Kenyatta alitoa shukrani za dhati kwa Rais Magufuli akisema ndege hao ni ishara ya upendo, umoja na undugu baina ya watu wa nchi hizo mbili.

“Kwa niaba yangu mwenyewe na watu wa Kenya, napokea zawadi hii maalumu. Hii ni ishara ya undugu na urafiki baina ya wakazi wa Afrika Mashariki,” alisema Rais Kenyatta.

“ Ni heshima kubwa si tu kati yetu sisi marais bali na kwa watu wa Afrika Mashariki. Undugu na urafiki huu mkubwa unapaswa kuendelea kwa ajili ya maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho,” aliongeza.

Rais Kenyatta alisema Kenya haiichukulii Tanzania kama jirani tu bali ndugu wanaoshirikiana malengo ya kuwaletea watu wake maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Tutapambana na yote hasi yanayoathiri watu wetu na changamoto nyingine zozote zitakazoibuka  hadi tujenge undugu wenye nguvu na mshikamano ambao utawezesha watu wetu wa Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na  Burundi  kutajwa kama Waafrika Mashariki,” alisisitiza Kenyatta.

Aliuhakikishia ujumbe ulioongozwa na Dk. Chana kwamba Kenya itahakikisha tausi hao wanne wanapewa matunzo makubwa.

Kwa upande wake Dk. Chana alimpongeza Rais Kenyatta kwa uongozi wake na kuongeza kuwa tausi aliowakabidhi wanatoa ishara ya upendo, heshima na kuthamini urafiki baina ya nchi hizo.

 Wakati Rais Kenyatta akipokea tausi hao walikuwapo Katibu Wizara ya Afya, Sicily Kariuki, Spika wa Bunge la Kenya, Justin Muturi  Seneta Ken Lusaka, Kiongozi wa walio wengi bungeni,  Aden Duale  na kiongozi wa maseneta , Kipchumba Murkomen.

Wengine ni Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu na Mwambata wa kijeshi  wa Tanzania nchini Kenya Kanali Fabian Machemba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles