27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kabendera apekuliwa mara ya pili

LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi limefanya tena upekuzi nyumbani kwa mwandishi wa habari za uchunguzi, Eric Kabendera, anayeshikiliwa kwa zaidi ya siku tano sasa tangu Julai 29 mwaka huu kuhusu utata wa uraia wake.

Zaidi mwanasheria wa Kabendera amesema, Serikali kupitia jeshi la polisi sasa imeamua kumshtaki Kabendera kwa uchochezi. 

Wakati huo huo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, ameliamiba gazeti hili kuwa bado wanaendelea kumuhoji mwandishi huyo na kwamba atafikishwa mahakamani wiki ijayo.

Alipoulizwa kama mtuhumiwa huyo amepatikana na tuhuma zozote zinazomlazimu kupelekwa mahakamani alisema ni vigumu kuthibitisha kwa sababu watu huwa wanakataa hadi mwisho.

“Kuthibitisha inatengemea, watu huwa wanakataa hivyo ni hadi mahakamani, kwa hiyo hajathibitisha na upelelezi unaendelea,”  alisema Mambosasa.

Wakati Mambosasa akisema hayo Wakili wa Kabendera, Jebra Kambole, alitoa taarifa akieleza kuwa jana polisi ilituma maofisa wake  kwenda kupekua nyumbani kwa Kabendera.

Mwanasheria huyo pia ameelezea jinsi mwanahabari huyo alivyohojiwa  katika maeneo matatu tofauti, kitengo cha uhalifu wa mtandao na uhamiaji.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, Serikali kupitia jeshi la polisi sasa limeamua kumshtaki Kabendera kwa uchochezi  kutokana na kuandika habari iliyochapishwa katika jarida la The Economist la nchini Uingereza Julai 31 mwaka huu ikiwa na kichwa cha habari ‘ John Magufuli is bulldozing Tanzania’s Freedom’.

Akielezea jinsi mahojiano yake yalivyochukua muda mrefu na pasipo kupewa dhamana, Jebra alisema siku ya kwanza pamoja na kumiliki hati yake ya kusafiria, Kabendera alihojiwa na maofisa wa uhamiaji kwa saa nne kuhusu uraia wake. 

Alisema Agosti 1 alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi na kuhojiwa na Kitengo cha uhalifu wa mitandao kwa saa tatu kwa kosa la uchochezi  chini ya kifungu cha 52 na 53 cha Sheria ya Huduma ya Habari

 “Erick amenyimwa dhamana na polisi licha ya kwamba dhamana ni haki ya kikatiba nchini Tanzania. Polisi wametuma maafisa wa polisi kupekuwa nyumba ya Erick leo. Kama mtetezi wa Erick, ninafuatilia kwa karibu suala hilo na nitautaarifu umma kitaifa na kimataifa juu ya hatma yake,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa za kukamatwa kwa Kabendera zilianza kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii jioni ya Julai 29 na kuthibitihswa na ndugu zake waliodai kuwa mwanahabari huyo alichukuliwa nyumbani kwake Mbweni, Dar es Salaam na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi.

Siku moja baadaye Mambosasa katika mkutano na waandishi wa habari alisema polisi wanamshikilia Kabendera kwa mahojiano kuhusu uraia wake na kwamba alikamatwa baada ya kushindwa kutii wito wa kumtaka kufika polisi kwa mahojiano.

Julai 31 Idara ya Uhamiaji ilidai kuwa imekuwa ikimfuatilia mwandishi huyo tangu mwaka 2013, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakilalamika kuwa si raia wa Tanzania.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Uraia na Pasipoti wa Uhamiaji, Gerald Kihinga, katika mahojiano na gazeti hili mapema wiki hii, ambapo alisema uchunguzi huo ulianza muda mrefu, lakini yeye alikaidi alipoitwa kutoa maelezo ya upande wake.

Kihinga alikiri  kufanya naye mahojiano ya awali na alisisitiza kuwa  endapo ataonesha ushirikiano wataangalia suala la kumpa dhamana.

Kuhusu uraia wa ndugu zake, Kihinga alisema watakapomaliza mahojiano watakachobaini ndiyo kitakachowafanya kuanza uchunguzi kwa ndugu zake.

Inadaiwa kuwa Mei mwaka 2013, ndiyo yalifanyika mahojiano ya mwisho kuhusu suala hilo ambapo pia wazazi wake walihojiwa.

Inadaiwa kuwa kutokana wakati wa sakata hilo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliunda kamati kuchunguza uraia wa Kabendera.

Inadaiwa kuwa Dk. Nchimbi, aliwaagiza maofisa wa uhamiaji kutowasumbua wazazi wa Kabendera kuhusiana na uraia wao, agizo ambalo linadaiwa kutolewa baada ya Kabendera kumwandikia barua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles