23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyakazi Tigo kizimbani kwa kuwaibia mamilioni wateja

KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

WAFANYAKAZI wanne wa kampuni ya mawasiliano ya  Tigo na wananchi sita wanaodaiwa kushirikiana nao wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya kujipatia mamilioni ya fedha kwa kuingilia miamala ya fedha za wateja, udanganyifu na kutakatisha fedha.

Waliofikishwa mahakamani ni Raia wa Burundi, Hamis Singa (30) ambaye ni kiongozi wa wafanyakazi wa Tigo mjini Babati na wenzake wanne (si wafanyakazi wa kampuni hiyo) ambao wanatuhumiwa kujipatia Sh milioni 26 kutoka kwa wateja wa Vodacom na Airtel  kwa njia ya ulaghai.

Wengine ni wafanyakazi watatu wa Tigo Mlimani City na wenzao wawili (si wafanyakazi wa kampuni hiyo) ambao wanadaiwa kujipatia zaidi ya Sh milioni 20 na kutakatisha fedha hizo huku wakijua ni zao la uhalifu.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salim Ally.

Wakisomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, ilidaiwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka saba likiwemo moja la kutakatisha fedha.

SINGA WA BABATI

Wankyo aliwataja washtakiwa kuwa ni Hamis Singa, Jailos Joseph (33), Singa Mnunga (32), Japhet Mkumbo (33) na Omari Omari (33) wote ni wakulima wanaishi Babati na Arusha.

Alidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa tarehe isiyofahamika kati ya Januari na Julai, 2019 maeneo ya Arusha, Manyara na sehemu nyingine nchini walikula njama ya kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Shtaka la pili washtakiwa wanadaiwa katika kipindi hicho kwa ulaghai walijipatia Sh 26,432,441 kwa kuhamisha fedha hizo kutoka kwa wateja wa Vodacom na Airtel.

Washtakiwa wanadaiwa katika shtaka la tatu walisambaza ujumbe usemao ‘Tuma pesa kwenye namba hii’ huku wakijua ujumbe huo wa uongo wenye nia ya kupotosha umma.

Shtaka la nne kwa washtakiwa wote, wadaiwa kusambaza ujumbe wa uongo kwa watu mbalimbali ukielekeza kutuma fedha kwenye simu iliyosajiliwa kwa majina mengine.

“Mheshimiwa Hakimu shtaka la tano lina wakabili washtakiwa wote wanadaiwa kusambaza ujumbe wa uongo kwa nia ya kujipatia fedha.

“Shtaka la sita linamkabili mshtakiwa Hamis, anadaiwa akiwa mwajiriwa wa Kampuni ya Tigo kwa ulaghai alipata uwezo wa kuingilia miamala ya fedha ya mawakala wa tigo kwa nia ya kujipatia fedha.

“Shtaka la saba kwa washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh 26,432,441 huku wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu,”alidai Wankyo.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote sababu kesi hiyo imefunguliwa chini ya sheria ya Uhujumu Uchumi ambapo mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo. Kesi itatajwa Agosti 15 mwaka huu.

TIGO MLIMANI CITY

Wakati huo huo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile wamefikishwa wafanyakazi wengine wa Tigo wa Mlimani City Dar es Salaam, Kokubelwa Karashani (35), Khalfani Milao (29) na Godfrey Magoye (30)  pamoja wenzao wawili, Mohammed Abdallah (25) na Mosses Kilosa (29).

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matano yakiwemo kulanjama, kujipatia fedha kwa udanganyifu, kuingilia miamala ya fedha za wateja na kutakatisha fedha.

Wafanyakazi hao wa Tigo wanadaiwa kuingilia miamala ya wateja na kumpa taarifa mshtakiwa Mohammed Abdallah.

Washtakiwa wanadaiwa kujipatia Sh 20, 378,627 kwa udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha huku wakijua kinatokana na zao la uhalifu.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu kitu, kesi yao itatajwa Agosti 15 mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles