Grace Kisyombe
Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), limefanya mkutano na wateja wake wakubwa na wenye viwanda katika Kanda ya kati, kikao hicho kilihusisha wawekezaji wenye viwanda katika mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida.
Akifungua rasmi mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge amesema serikali iliahidi kuwapatia Watanzania huduma ya umeme iliyo bora na yenye uhakika ili kuweza kuwakwamua kiuchumi wananchi hususan walioko maeneo ya vijijini.
Dk. Mahenge ametaja miradi midogo na mikubwa inayoendelea mkoani humo ni pamoja na ule wa uboreshaji wa kituo kikubwa cha gridi cha Zuzu ambacho kinaongezewa uwezo kutoka uwezo wa kupokea megawat 48 hadi kufikia Megawati 400, kazi ambayo inafanywa na serikali kwa ushirikiano na mdau wa maendeleo ambaye ni African development bank.
Dk. Mahenge amewaomba wawekezaji kutumia fursa hiyo ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kuwekeza zaidi katika viwanda mbali mbali hasa ikizingatiwa kuwa Dodoma sasa ndio Makao Makuu ya Serikali.
Naye Meneja Mwandamizi Tanesco Kanda ya Kati, Mhandisi Athanaius Nangali amesema wana miradi mingi inayoendelea katika maeneo mbali mbali ya Kanda ya kati, akiitaja miradi hiyo ni pamoja na ule wa upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Singida kutoka Megawat 32 hadi kufikia uwezo wa Megawati 400.
“Kwa Mkoa wa Dodoma kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa ‘Ring circuit’ ya njia ya usafirishaji umeme itakayo jengwa kutokea Kituo cha Zuzu hadi Kituo cha Msalato, kuelekea Ihumwa katika mji wa serikali, kutokea hapo Ihumwa njia hiyo itakwenda mpaka maeneo ya Kikombo, ambapo pia kutakuwa na kituo cha uwezo wa 220/33kv na njia hiyo itaunganisha kikombo hadi Zuzu,” amesema Nangali.