CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM
KONGAMANO la kwanza la Usalama Barabarani limefanyika Machi 30, mwaka huu, likiwa limebeba ujumbe wa ‘Paza sauti, zuia ajali okoa maisha.’
Mwaka huu kongamano hilo lilifanyika badala ya maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani, kama ilivyokuwa awali ambapo wadau mbalimbali walikutana kwa lengo la kujadili fursa na changamoto zinazoweza kupatiwa majibu ya kupunguza ajali.
Katika kongamano hilo, wadau wa usalama walipata fursa ya kujadili changamoto zilizopo sekta ya usafiri na umuhimu wa maboresho ya sheria ya mwaka 1973 inayodaiwa kupitwa na wakati.
Wadau hao wanasema mabadiliko hayo yakipitishwa yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza au kumaliza kabisa ajali, ambazo nyingi zinasababishwa na makosa ya kibinadamu na uzembe.
Shirika la Afya Duniani – WHO, linasema ajali za barabarani zinaendelea kupoteza maisha ya watu wengi ambapo kila mwaka watu milioni 1.25 hufariki dunia.
Takwimu zinaonesha kwamba vijana walio katika umri kati ya miaka 15 hadi 29 hupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani.
Ripoti WHO inasema asilimia 90 ya vifo vya ajali barabarani vinatokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, japokuwa wana asilimia 54 tu ya magari duniani. Utafiti unaonesha nusu ya vifo vya majeruhi vinaweza kuepukika iwapo waathirika watapatiwa huduma bora mara baada ya ajali.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ajali za waendesha baiskeli na watembea kwa miguu ni asilimia 26 ya vifo vyote vitokanavyo na ajali za barabarani, ambapo idadi hii inafikia asilimia 33 barani Afrika.
Pia iligundua baadhi ya magari yaliyouzwa katika asilimia 80 ya nchi zote, yameshindwa kufikia viwango vya msingi vya usalama.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), wakishirikiana na wadau mbalimbali walifanya tafiti mbalimbali ili kuboresha hali ya usalama.
Mratibu wa Mradi wa Usalama Barabarani Tamwa, Gladness Munuo, anasema ipo haja kwa Serikali kufanyia kazi mapendekezo ya wadau wa usalama ili kupunguza ajali nchini.
Anasema tafiti nyingi zimefanyika na kuonyesha viashiria vya ajali, hivyo ni wakati sasa kwa serikali kuchukua hatua.
Gladness anasema wao tayari wamefanya tafiti zao kwa kushirikiana na asasi nyingine na kwamba wanachosubiri sasa ni muswada upitishwe.
Anasema kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana na wanahabari kuhamasisha na kuhabarisha umuhimu wa kufahamu sheria za usalama.
“Ni muhimu sasa kundi hili kupewa mafunzo yatakayoboresha habari zao,”anasema Gladness.
Anasema ajali za barabarani zimekuwa chanzo cha tatu katika kusababisha vifo hivyo, madereva, wamiliki wa vyombo vya usafiri na wananchi, wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni, alama na ishara za barabarani ili kupunguza vifo na majeruhi wanaotokana na ajali.
Anataja viashiria vitano vya ajali za barabarani vinavyosababishwa na udhaifu wa kibinadamu kuwa ni ulevi, vizuizi vya watoto, mikanda ya kwenye siti, mwendokasi na kutokuvaa kofia ngumu (helmet) kwa madereva na abiria wa pikipiki.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, analitaka
Baraza la Usalama Barabarani kusimamia utekelezaji wa mpango mkakati wa baraza awamu ya nne.
Anasema ni vyema kukawa na mwongozo wa utendaji na utekelezaji wa majukumu ya kamati za usalama barabarani za mikoa na wilaya ili kudhibiti ajali za barabarani na kuimarisha utendaji wa kamati.
“Kikosi cha Usalama Barabarani kisimamie ukaguzi wa magari ili kuhakikisha magari mabovu yanaondoka barabarani,” anasema Lugola.
Anasema pia baraza lihusike kuweka msukumo wa uanzishwaji wa mfumo wa lazima wa ukaguzi wa magari ili uanze kutumika haraka hapa nchini.
Lugola anashauri baraza hilo likamilishe uundwaji wa kamati za usalama barabarani za mikoa na wilaya haraka, ili kamati hizo zianze kazi hatimaye kwenda na mabadiliko yanayofanyika ndani ya baraza.
“Hii ni pamoja na kuweka msukumo katika mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya usalama barabarani yanayolenga kuleta mabadiliko ya muundo wa baraza kulifanya liwe tendaji,” anasema Lugola.
Anasema asilimia 76 ya ajali za barabarani hapa nchini hutokana na makosa ya kibinadamu, ambapo kati ya hizo asilimia 40 ya ajali hutokana na uzembe wa madereva.
“Ajali nyingi hapa nchini zinaweza kuzuilika iwapo tutabadili tabia zetu kwani kwa mwaka 2018 madereva 1556 walisababisha ajali kwa uzembe, madereva 364 mwendokasi, madereva 61 ulevi na madereva 725 walisababisha ajali kwa kuendesha pikipiki kizembe,” anasema Lugola.
Anasema pia watu 103 walisababisha ajali kwa kuendesha baiskeli kizembe na watembea kwa miguu 259 walisababisha ajali kwa uzembe wao.
Anaasema ili kufikia malengo ni vema askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakaepuka vitendo vya rushwa na badala yake kusimamia maadili na weledi wa kazi zao.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu, anasema takwimu alizonazo zinaonyesha ajali hizo zinapungua na kwamba mwishoni mwa wiki iliyopita kulikuwa na ajali mbili tu nchi nzima zilizosababisha kifo kimoja na majeruhi mmoja.