Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Katika kuhakikisha sekta ya kilimo inakua na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kupitia mfuko wake wa dhamana wa wakulima wadogo (SCGS)imetoa rai kwa mabenki mengine nchini kujitokeza kushirikiana kuboresha mikopo kwa wakulima.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya awamu ya pili kuongeza mkataba wa ushirikiano kati ya TADB na Benki ya Biashara Tanzania(TCB) kwa ajili ya kutoa dhamana ya mikopo ya kilimo,mifugo na uvuvi iliyofanyika leo Februari 1, 2024 jijini Dar es Salaam.
Amesema mfuko huo ulianzishwa mwaka 2018 ambapo serikali ilitoa sh bilioni 57 na kufikia sasa wana bilioni 250.77, hivyo kwa miaka mitano mfuko umeweza kuwafikia watanzania.
“Mikopo itakayotolewa na TCB kwa wakulima itapitia kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo,mifugo na uvuvi na sisi TADB tutatoa dhamana ya hadi asilimia 70 kwa mikopo yote hasa kwa vijana,wanawake na miradi inayosaidia kupunguza au kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,”amesema Nyabundege.
Ameeleza kuwa mkataba huo utasaidia kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogo na itakua njia rahisi ya kuwafikia wengi zaidi hasa waliopo pembezoni mwa miji,mikoa na wilaya.
“Mkataba huu tulioingia leo ni wa awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza TCB kupitia dhamana ya TADB ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 34.1 kwa wanufaika wa moja kwa moja 2,638 na wasio wa moja kwa moja zaidi ya 7,750 ambapo zaidi ya asilimia 95 walikua wakulima wadogo,” amesema.
Ameongeza kuwa benki hiyo imefanya maboresho na kuongeza wigo wa dhamana kutoka asilimia 50 hadi 70 kwa miradi ya wanawake,vijana na miradi ya mabadiliko ya tabianchi ambapo pia itasaidia upatikanaji wa mikopo na kuchochea ongezeko la ajira kwa vijana.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo amesema mikopo hiyo itawasaidia kuwapa mitaji itakayowawezesha kutoka kwenye kilimo cha kujikimu na kwenda kwenye kilimo cha biashara kwa riba nafuu ambapo pia itasaidia kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla.
“Tunaishukuru TADB kwa kutuongezea nguvu kwa ajili ya kuwafikia wakulima,wafugaji na wavuvi wengi zaidi, mikopo hii itapatikana katika matawi yote ya TCB nchi nzima na nia hasa ya kuongeza mikataba hii ni kuhakikisha tunawafikia wakulima wa pande zote za muungano kwa kuwaongezea mitaji kwa riba nafuu,”amesema Mihayo.
Ushirikiano wa TCB na TADB umefanya jumla ya taasisi za kifedha zinazonufaika na mfuko wa dhamana wa wakulima wadogo (SCGS) kufikia 16.