33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

TABIA 15 ZINAZOWEZA KUATHIRI KINYWA, JINSI YA KUZIDHIBITI

WATU wengi wamekuwa wakisumbuliwa na meno bila kutambua chanzo chake. Leo tutaangalia mambo mbalimbali ambayo yanaweza kuathiri afya ya kinywa na namna ya kudhibiti hali hiyo.

Kutafuna kucha

Tabia hii inaweza kusababisha sehemu ya jino kusagika, kuwa dhaifu na hata kuvunjika. Pia na matatizo katika viungo vya taya na hivyo kuleta maumivu karibu na eneo la masikio (Temporomandibular joint dysfunction). Chanzo cha tabia hii kinaweza kuwa ni mazoea tu, au msongo wa mawazo na kazi.

Ili kuacha tabia hii kata kucha kwa kutumia kifaa maalumu kwa wakati, epuka msongo wa mawazo na jitahidi kuwa na mpangilio mzuri wa kazi zako.

Kusafisha meno kwa kutumia nguvu

Usitumie nguvu wakati wa kusafisha meno kwani unaweza kusababisha kuharibika kwa fizi zako na sehemu ya jino inayopakana na ufizi. Tumia mswaki wenye brashi laini na muda wa wastani wa dakika mbili, mara mbili kwa siku.

Kutumia meno yako kama kifaa

Tabia kama kufungua kizibo cha chupa, kufungua pakiti ngumu kama za maziwa kwa meno, kushika vitu kama sindano, kushikilia au kumenyea nyaya (kwa mafundi wa umeme, betri), kushikilia misumari (mafundi ujenzi) n.k.

Kazi ya meno ni kutafuna chakula si kutumika kama kifaa mbadala. Tabia hizi zinaweza kusababisha meno kuvunjika au kujiumiza mdomoni, au hata kumeza vitu hivyo kwa bahati mbaya.

Tabia ya kutafuna vitu vigumu kama mchele

Hii husababisha meno kusagika au kuweka nyufa na maumivu au ganzi kwa baadhi ya meno na hata kuvunjika kwa kipande cha jino. Tabia hii huanza taratibu kwa kuiga na baadae kuwa mazoea. Kuwa mbali na vitu hivyo vinavyotamanisha kutafuna kunaweza kusaidia kuacha tabia hii.

Kula vitu vyenye sukari mara kwa mara

Kula kashata, ufuta, ubuyu, visheti, biskuti, pipi, keki, bazoka (Big G, orbit, n.k.) mara kwa mara, hasa vile vyenye sukari huongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa kuoza kwa meno. Mabaki ya vyakula hivi hutumiwa na bakteria (wanaoozesha meno) kutengeneza asidi inayoharibu sehemu ngumu ya nje ya jino na kuacha matundu. Punguza matumizi ya vyakula vyenye sukari, njia mojawapo ikiwa ni kuvitumia vyakula hivyo wakati unapokula milo mikuu mitatu.

Matumizi ya kahawa

Rangi ya kahawa huweka rangi kwenye enameli (sehemu ngumu ya nje ya jino) na asidi iliyopo ndani yake huweza kusababisha enameli kulika, hivyo rangi ya asili ya meno kupungua na kuanza kuwa na rangi ya njano kadiri muda unavyopita.

Kutafuna penseli au kalamu

Tabia ya kutafuna penseli au kalamu inafanywa na watu wengi hasa wanapokuwa kwenye masomo, au kazi zinazohusisha kuandika na wakati mwingine msongo wa kazi nyingi. Tabia hii inaweza kusababisha meno kusagika kama itafanyika kwa muda mrefu. Kama unatabia hii ni vizuri ukatumia bazoka isiyo na sukari (sugarless gum), kila unapohitaji kutafuna kitu. Matumizi ya bazoka husaidia kuongeza na kusisimua mate kutoka mdomoni hivyo kuimarisha meno na hata kuzuia mashambulizi ya asidi.

Kuvuta sigara

Matumizi ya sigara na tumbaku za aina yoyote huweza kusababisha meno kubadilika rangi na kuongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa fizi. Pia matumizi ya tumbaku yanaweza kukusababishia saratani kwenye ulimi na mdomo. Tumia mbinu mbalimbali kukwepa na kuacha kabisa kuvuta sigara. Pamoja na madhara mengi ya kiafya yanayoweza kusababishwa na uvutaji wa sigara, sigara haina faida yoyote katika mwili na maisha ya binadamu kwa ujumla.

Kutafuna barafu

Kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya barafu na vinywaji baridi na vikali, baadhi ya watu hupendelea kutafuna barafu wakati wa kunywa vinywaji vyao. Kutafuna barafu kunaweza kusababisha meno kuvunjika, au kuweka nyufa zisizoonekana. Hii huweza kusababisha kupata maumivu au hali ya kufa ganzi wakati wa matumizi ya vitu vya baridi au vya moto. Pia barafu iliyovunjika inaweza kuwa imechongoka na kuweza kusababisha kidonda kwenye fizi na ulimi. Inashauriwa badala ya kutafuna barafu, iache iyeyuke mdomoni, kama wewe unapendelea raha ya ubaridi wa barafu mdomoni kwako.

Kusaga na kutafuna meno (Bruxism)

Kusaga na kutafuna meno ni tabia inayohusisha msuguano wa meno unaotokea wakati wa usiku au hata mchana hivyo husababisha meno kusagika, kulika na kuweka nyufa ndogo ndogo kwenye sehemu ngumu ya jino na kuumwa kwa misuli ya uso na viungo vya taya. Pia meno huweza kupata ganzi mara kwa mara na kupata shida ya kutafuna. Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kutumia kizuizi kinachoitwa “night guard” wakati wa usiku na ushauri nasaha kutoka kwa daktari wa afya ya kinywa. Ganzi kwenye meno inaweza kutibiwa kwa kupaka dawa maalumu inayozuia ganzi pamoja na kutumia dawa ya meno inayopunguza ganzi (toothpaste special for sensitive teeth)

Matumizi ya chupa za lishe kumlazia mtoto

Hii itamfanya mtoto awe anategemea kulala akiwa na chupa mdomoni–ya juisi, maziwa au lishe yoyote. Matumizi ya chupa hizi bila mpangilio yanaongeza uwezekano wa kuoza meno kwa kasi (rampart caries). Inashauriwa chupa hizi zitumike kwa matumizi ya lishe tu, si kitu cha kumbembelezea mtoto ili alale usingizi.

Kutoga ulimi, mdomo, mashavu

Kutoga ulimi kunaweza kusababisha kuvuja kwa damu nyingi pale mshipa mkubwa wa damu utakapotobolewa. Pia kidonda kisipotunzwa vizuri huweza kupata maambukizi na kushindwa kupona kwa wakati. Kipini cha urembo kinachowekwa kwenye ulimi, mdomo au mashavu kinaweza kusababisha jino kuvunjika pale kiking’atwa kwa bahati mbaya– au kutengeneza nyufa ambazo zitakuwa zinauma na hata kusababisha ganzi kila unapokula kitu cha baridi, moto au hata hewa ya baridi ikiingia mdomoni.

Matumizi ya tembe za kulainisha koo (throat lozenges)

Tembe hizi mara nyingi huwekwa kiwango kikubwa cha sukari hivyo kukuongezea hatari ya kuoza kwa meno. Tabia ya matumizi ya chembe kama kiburudisho ni hatarishi kwa afya ya meno. Matumizi yasiyo sahihi, ni matumizi ya mara kwa mara yasiyohitajika. Tembe hizi zikitumika kwa muda mfupi hazina madhara yoyote kwenye meno.

Matumizi mabaya ya mvinyo

Mvinyo una kiwango kikubwa cha asidi ambayo huharibu sehemu ngumu ya nje ya jino inayoitwa enameli na kuacha matundu madogo kwenye meno yanayosababisha kuhifadhi vitu vinavyoweka rangi kwenye meno. Mfano; mvinyo mwekundu una chembechembe zinazoitwa ‘chromogens’ pamoja na ‘tannins’ ambavyo huweka rangi kwenye meno. Wanywaji wengi wa mvinyo hunywa taratibu kwa muda mrefu, hivyo kufanya tindikali (acid) iliyomo kwenye mvinyo iharibu meno. Pia tindikali hiyo husababisha kumomonyoka kwa enameli (dental erosion) na kuifanya kuwa dhaifu. Kama meno yako yameathirika kwa kuwa na rangi isiyokuridhisha na wakati mwingine kufa ganzi kutokana na kumomonyoka kwa enameli na unafikiri imetokana na matumizi ya mvinyo kama maelezo hapo juu, basi punguza matumizi haya na pata ushauri wa daktari wa kinywa na meno kutibu tatizo la ganzi.

Kutafuna popoo, tambuu na mirungi

Hii hufanya meno kuwa na rangi isiyopendeza, meno hupoteza uimara wake na kutengeneza nyufa, mdomo kutoa harufu mbaya, huongeza uwezekanao wa kupata ugonjwa wa fizi na ina kilevi kinachosababisha uteja (addiction). Matumizi ya vitu hivi hujenga tabia ya mazoea (addiction) ambayo inahitaji ushauri nasaha na matibabu kutoka kwa madaktari wa saikolojia.

Makala hii imeandaliwa na Daktari wa kinywa, Deogratias Kilasara (DDS, MDent).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles