25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

MAFINDOFINDO CHANZO CHA MARADHI YA MOYO KWA WATOTO

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WATAALAMU wa masuala ya afya wanashauri kwamba mwanamke kabla ya kubeba ujauzito ni muhimu kujiandaa miezi sita kabla. Katika kipindi hicho anapaswa kula vyakula bora na kujiepusha na ulaji usiofaa.

Wanasema mwanamke anapaswa kuwa makini pia katika kipindi cha wiki 12 ya kwanza ya ujauzito atakaobeba.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Naiz Majani anasema kipindi hicho ni muhimu kwani ndipo ambapo viungo vya mwili wa mtoto huanza kuumbwa ndani ya tumbo la mama yake.

“Viungo vya mtoto huanza kuumbwa tumboni mwa mama katika kipindi cha wiki 12 ya kwanza ya ujauzito ambacho kwa kawaida wanawake wengi wanakuwa bado hawajajijua kama tayari wamepata ujauzito.

“Sasa basi, mama anapokuwa amejiandaa kubeba ujauzito miezi sita kabla, anakuwa anakula vyakula bora, anaachana na ulaji usiofaa, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na mambo mengine kama hayo, inakuwa imesaidia kumwepusha mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo mbalimbali,” anasema.

Dk. Naiz anasema mambo ni tofauti kwa wanawake wengi hasa wale wanaoishi katika nchi zinazoendelea jambo ambalo humuweka mtoto aliyepo tumboni katika hatari ya kupata magonjwa.

“Mimba nyingi nchini ni za kushtukiza, wanawake wengi wanajikuta tayari ni wajawazito wakati wakiwa hawajajiandaa kubeba mimba. Nchi za wenzetu wanapotaka kubeba ujauzito hujiandaa miezi sita kabla.

“Wanazingatia mno suala hili kwa sababu wanatambua wazi kwamba kipindi cha wiki 12 za kwanza za ujauzito ni muhimu kwani ndipo ambapo viungo vya mtoto huanza kuumbwa tumboni mwa mama yake,” anasema.

Dk. Naiz anasema iwapo mama hajajiandaa katika kipindi cha miezi sita kabla huwa ni hatari kwa mtoto aliyembeba tumboni mwake kwani ataendelea na maisha yake ya kawaida mfano ulaji usiofaa, uvutaji sigara na unywaji pombe hivyo humuathiri mtoto.

Tatizo la moyo kwa mtoto

Daktari huyo anasema kwa asilimia 90 bado wataalamu hawajajua sababu hasa za mtoto kuzaliwa na tatizo la moyo.

“Kwa asilimia 10 tu ndiyo tunajua sababu ya mtoto kuzaliwa na tatizo hili. Kwenye hii asilimia 10 mara ngingi chanzo huwa ni matatizo anayoyapata mama katika kipindi cha miezi mitatu ya ujauzito.

“Unakuta huenda mama alipata homa kali wakati wa ujauzito, virusi vya rubella, shinikizo la damu, kisukari au alikuwa anakunywa dawa bila ushauri wa daktari. Lishe duni, mama asipopata virutubisho vya folic acid, uvutaji sigara, unywaji pombe na sababu nyinginezo ikiwamo kurithi ingawa si kwa asilimia kubwa,” anasema.

Anasema ndiyo maana wataalamu wanashauri mjamzito kuhudhuria kliniki katika kipindi chote ili wafuatilie afya ya mtoto aliyepo tumboni na ukuaji wake.

Anasema katika kipindi hicho cha awali mama hupewa chanjo mbalimbali ikiwamo dhidi ya ugonjwa wa rubella ambao unaweza kumsababishia mtoto kupata magonjwa ya moyo.

“Mama asipopata chanjo ya rubella katika kipindi cha ujauzito humuweka mtoto aliyembeba tumboni mwake katika hatari ya kuzaliwa akiwa na magonjwa ya moyo,” anasema.

Dk. Naiz anasema magonjwa ya moyo kwa watoto yapo ya aina mbili ambayo ni yale ya kuzaliwa nayo na yasiyokuwa ya kuzaliwa nayo.

“Haya ya kuzaliwa nayo chanzo chake nimeeleza hapo awali kwamba huweza kutokea iwapo mama hatapatiwa baadhi ya chanjo ikiwamo ya rubella na kama ataendelea na ulaji usiofaa,” anasema.

Dalili za tatizo

Daktari huyo anasema watoto waliozaliwa na tatizo la moyo huwa wanaonesha dalili tofauti tofauti ikiwamo kuzaliwa na uzito mdogo kuliko kawaida.

Anasema wengine wanabadilika rangi isiyokuwa ya kawaida na wengine wakinyonya ziwa la mama hata kidogo tu huchoka haraka.

“Unakuta mama anasema akimuweka mtoto wake kwenye ziwa anyonye, ananyonya kidogo – anachoka haraka na kutokwa jasho kwa wingi, wazazi wengine wanadhani ni afya, si kweli. Mtoto akinyonya kidogo na kutokwa jasho jingi ni ishara kwamba ana tatizo la moyo, wamuwahishe hospitalini.

“Watoto wachanga huwa hawafanyi mazoezi, kwa hiyo zoezi kubwa kwao ni kunyonya.

 “Lakini kwa watoto wanaoweza kujieleza wanasema nikicheza kidogo nachoka haraka na atakuwa anatokwa na jasho kwa wingi. Kuchoka haraka ni dalili yao kubwa na unaweza kukuta wengine hawakui vizuri kama watoto wa rika lao, kwa mfano ikiwa amezaliwa na kilo mbili baada ya wiki mbili unaweza kukuta ana kilo hizo hizo au zikiongezeka ni kidogo mno,” anasema.

Anasema wapo wengine ambao hufikishwa kwao wakiwa tayari umri wao umekwenda ambao walianza kuonesha dalili za kuumwa kifua mara kwa mara.

“Mtoto akiumwa kifua mara kwa mara wazazi na walezi hudhani kuwa ni tatizo la nimonia lakini kumbe ni moyo. Unakuta mtoto amelazwa kwa nimonia hata mara tatu hadi nne pasipo kujua ni shida ya moyo,” anasema.

Dk. Naiz anasema mzazi anapoona mtoto wake anahema haraka haraka kupita kiasi, au anapata homa ya mapafu mara kwa mara hizo zote ni dalili za magonjwa ya moyo.

Kuhusu mafindofindo

Anasema iwapo mtoto ataugua mafindofindo (tonsillitis) na asitibiwe inavyopaswa huwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo katika ukuaji wake.

“Ipo dhana mtoto akiugua mafindofindo wazazi wanamtibu kienyeji nyumbani (pasipo ushauri wa daktari) – wanakwenda dukani na kununua dawa za kumtibu au wanampatia maji ya moto anywe, si sahihi.

Anasema vipo vyanzo vya aina mbili ambavyo husababisha tezi kuvimba, chanzo kikubwa kikiwa ni virusi na kwa asilimia ndogo husababishwa na bakteria.

“Sasa hatumaanishi kwamba tezi zote zikivimba lazima upate dawa, isipokuwa ipo tezi ambayo ikivimba lazima upewe dawa kutibu na hiyo aina ya tezi usipopata dawa ndipo unaishia kupata tatizo la moyo.

 “Hapa JKIC tumegundua asilimia kubwa ya

watoto wanaofikishwa kwetu waliwahi kuugua mafindofindo walipokuwa wadogo na hawakutibiwa ipasavyo, yaani mtoto alizaliwa akiwa hana tatizo la moyo lakini anajikuta akipata wakati wa ukuaji wake na kuhitaji upasuaji mkubwa,” anasema.

Yanapaswa kugunduliwa mapema

Dk. Naiz anasema magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yanapaswa kugundulika mapema ili kuokoa maisha ya mtoto husika.

“Katika kundi hili kuna magonjwa yapatayo saba, haya yanapaswa kugundulika mapema ingawa yapo mengine si magonjwa ya kuzaliwa nayo ambayo yanapaswa nayo kugundulika mapema kabla mtoto hajafikisha mwaka mmoja.

“Mtoto akizaliwa na magonjwa ya moyo hapaswi kufanyiwa kitu chochote, upasuaji hufanyika mara moja ili kumsaidia kutibu tatizo,” anasema.

Anasema kwa kuwa watoto wengi huwa hawagunduliki mapema asilimia 25 hufariki kabla ya kufikisha mwaka mmoja.

“Asilimia nyingine 25 wakibahatika kufikisha mwaka mmoja na nusu hufariki dunia na wakifikisha miaka miwili hadi  mitatu asilimia 80 hadi 90 hufa iwapo wakicheleweshewa matibabu,” anasema.

Hali ilivyo

Anasema watoto wengi huchelewa kugundulika mapema kwani hucheleweshwa kufikishwa hospitalini na wazazi au walezi wao.

“Wazazi wengi hushindwa kuwawahisha mapema kwa sababu, mara nyingi magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo dalili zake hufanana na magonjwa mengine ya kawaida kwa watoto kama malaria, nimonia na utapiamlo.

“Kwa kuwa zile dalili zinafanana na magonjwa mengine ya watoto, wakati mwingine huchukua muda mrefu hadi mtu anayemuona mgonjwa ahisi kwamba huenda mtoto husika anasumbuliwa na tatizo la moyo na amlete kwetu tumfanyie vipimo,” anasema.

Anasema wengine hufikishwa hospitali wakiwa katika hatua mbaya kiasi kwamba haiwezekani tena kuwafanyia upasuaji.

Anabainisha kuwa kuna aina ya magonjwa ya moyo ambayo mtoto huzaliwa nayo hivyo anatakiwa afanyiwe upasuaji akiwa na mwezi mmoja, mitatu au mwaka mmoja, akizidi umri huo haiwezekani tena.

Idadi inaongezeka

Dk. Naiz anasema kwenye taasisi hiyo idadi ya watoto wanaopokelewa wakisumbuliwa na magonjwa ya moyo inazidi kuongezeka kila mwaka.

Mpango wa kupima ujauzito

Anasema kwa kuwa watoto wengi wanacheleweshwa kufikishwa hospitalini, JKCI imeanzisha mpango wa kupima watoto tangu wakiwa tumboni.

“Mpango huu tuliuanza mapema mwaka jana na tayari wajawazito zaidi ya 10 tumewachunguza na kati yao wanne mimba zao ziligundulika kuwa watoto waliowabeba wanakabiliwa na magonjwa ya moyo.

“Tunajua si rahisi kupima wakina mama wengi lakini tumeweka makundi maalumu kwa mfano mama ambaye aliwahi kuzaa mtoto mwenye tatizo la moyo, au kama kuna historia ya watu waliozaliwa na matatizo ya moyo kwenye familia yao, wenye kisukari na shinikizo la damu ndio ambao tunawapa kipaumbele.

“Wengine wanafanyiwa kwenye kliniki zao za ujauzito ambapo huko wakigundulika kuwa wamebeba watoto wenye maumbile tofauti wanapewa rufaa na kuja hapa,” anasema.

Anasema wazazi ambao waligundulika watoto wao wana matundu kwenye moyo, waliwashauri wakajifungulie Hospitali ya Taifa Muhimbili ili tuwe nao karibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles