25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Taasisi yatoa tiba ya meno bure kwa wagonjwa 700

Mwandishi wetu -Dar es salaam

WAKAZI wa Wilaya ya Kilwa wamepata neema ya kupata huduma ya bure ya tiba ya afya ya kinywa na meno kupitia asasi isiyo ya kiserikali ya Bridge2 Aid ya nchini Australia kati ya Agosti 15 na 22, mwaka huu.

Madaktari bingwa wa afya ya kinywa na meno na wasaidizi wao kutoka katika taasisi hiyo, walijitolea kuja nchini kufanya matibabu haya pamoja na daktari wa afya ya kinywa na meno wa Wilaya ya Kilwa.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa taasisi hiyo, George Alexander, alisema licha ya kutoa tiba hiyo bure, pia madaktari bingwa wao watawafundisha maofisa tabibu sita wilayani humo jinsi ya kutoa huduma ya kwanza kwenye matibabu ya afya ya kinywa na meno ikiwemo ung’oaji salama wa meno.

“Lengo letu ni kuhakikisha pengo kubwa la uhaba wa madaktari wa afya wa kinywa na meno linazibwa kwa kuwapatia watu huduma stahiki.

“Hii ni kwa sababu asilimia kubwa ya programu nilizoshiriki utakuta daktari wa afya ya kinywa na meno mmoja katika wilaya nzima na unakuta wilaya hiyo ni kubwa na daktari wa meno wa wilaya anapaswa atembelee yote kwa ajili ya matibabu, ni changamoto kubwa sana,” alisema Alexander.

Daktari wa afya ya kinywa na meno wa Wilaya ya Kilwa,  Dk. Hussein Rwanda, alisema programu hiyo ni muhimu kwao na nchi kwa ujumla kwani wilaya nyingi ni kubwa na mara nyingine inabidi mtu asafiri hadi kilometa 120 kupata matibabu.

“Kwa kupitia programu hii ambayo mafunzo yanatolewa ya huduma ya kwanza ya afya ya kinywa na meno, huduma zinasogezwa karibu zaidi kwa wananchi,” alisema. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles