TMA yaanza safari mpya

0
775

Asha Bani- Dar es Salaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imeanza safari mpya jana baada ya kubadilika kutoka kuwa wakala na kuwa mamlaka kamili kisheria.

Akizundua mamlaka hiyo jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema 

taarifa za hali ya hewa zina umuhimu kwa shughuli za kiuchumi, ikiwemo za kilimo, uvuvi, usafiri wa anga na majini.

 “TMA nawapongeza katika utendaji wao kwani wamekuwa ni mfano wa kuigwa katika taasisi nyingine, hasa katika masuala ya kupangilia bajeti na matumizi yake.

“Katika hili nawapongeza pia, na mkiendelea kufanya vizuri kuna haja ya kuangaliwa hata masilahi yenu pia,” alisema Kamwelwe.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema Wakala wa Hali ya Hewa ambao ulifikia ukomo wake jana, ulianzishwa mwaka 1999 kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa Serikali sura 245 marejeo ya 2002.

Dk. Kijazi alisema ili kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa, Serikali imeona ni vyema kuhuisha na kuwa mamlaka kwa lengo la kuendelea kutoa huduma bora zaidi za hali ya hewa.

Akielezea mafanikio waliyoyapata wakiwa wakala, alisema walipata cheti cha ubora cha utoaji huduma za hali ya hewa kwa viwango vya kimataifa katika sekta ya usafiri wa anga (ISO 9001:2008) mwaka 2011.

Alisema Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kwa taasisi za hali ya hewa Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata cheti hicho.

 “Pia tuliendelea kuwa taasisi ya kiungo ya kuratibu taarifa za matukio ya Tsunami nchini (National Tsunami warning Centre).

“Wataalamu wa wakala wametoa mchango mkubwa wa kitaalamu katika Shirika la Hali ya Hewa Dunini (WMO) na kuzisaidia baadhi ya nchi wanachama barani Afrika na nje ya Bara la Afrika kuboresha huduma za hali ya hewa katika nchi zao,” alisema Dk. Kijazi.

Pia alisema Tanzania imeingia katika rekodi ya dunia kwa vituo viwili, cha Bukoba na Songea kutambuliwa rasmi kuwa na takwimu za muda mrefu za zaidi ya miaka 100.

Alisema wakala umeanzishwa mwaka 1999 na sasa wamekuwa mamlaka kamili waliokidhi mahitaji yote kisheria kwa mujibu wa sheria namba 2 ya 2019 iliyopitishwa na Bunge na kusainiwa na rais.

“Kutokana na uboreshaji huo, kwa sasa utabiri umekuwa ukifanyika kwa usahihi kwa asilimia 96 kutoka ile ya awali ya 87 na kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa kutokana na pia kuwepo kwa vifaa vya kisasa,” alisema Dk. Kijazi.

Alisema hata hivyo kuna vituo vya mamlaka hiyo ambavyo vinatambulika rasmi, ikiwa ni pamoja na kilichopo Bukoba na Songea.

“Vinasadia kutoa taarifa mbalimbali ambazo pia zinatumika katika kufanya tafiti mbalimbali, ikiwemo utabiri wa hali ya hewa, tafiti za kilimo,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi wa TMA, Dk. Burhan Nyenzi, alisema bodi ilifanya kazi kuhakikisha taarifa zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa usahihi zaidi.

Alisema bodi ilikuwa na kazi ya kuhakikisha pia vituo vinaboreshwa na kuongezeka, kutoa taarifa na kusimamia utoaji wa taarifa zake nchi nzima.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here