32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Sura mbili Uchaguzi Serikali za Mitaa

ANDREW MSECHU-Dar es Salaam

IKIWA zimebaki siku tano kukamilika kwa uchukuaji na urejeshaji fomu za kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, Kamati Kuu ya CCM, imeeleza kuridhishwa na hatua za awali za mchakato huo, huku Chadema wakitoa malalamiko baadhi ya maeneo.

Taarifa ya CCM iliyotolewa na Katibu wa Itikadi wa chama hicho, Humphrey Polepole, ilisema kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika jana, kimeridhishwa na mchakato unaoendelea na kuahidi kuchukua hatua pale itakapobainika kanuni zimekiukwa.

“Kikao, pamoja na mambo mengine kimefanya tathmini ya zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanzia uandikishaji, mchakato ndani ya chama na maandalizi ya kuelekea siku ya kupiga kura Novemba 24, 2019.

 “Kamati Kuu imejiridhisha kuwa mchakato wa chama wa kuwapata wagombea wa CCM kwa ujumla umekwenda vizuri, na kupitia kikao hiki chama kinapenda kutoa pongezi kwa viongozi na wanachama ambao wameshiriki zoezi hili la kidemokrasia na kwa uwazi katika chama chetu,” alisema Polepole.

Alisema Kamati Kuu imeelekeza katika maeneo ambayo taratibu za uchaguzi kwa namna moja au nyingine hazikufuatwa, taratibu za kikatiba na za kikanuni ziendelee ili kuhakikisha haki inatendeka kama ilivyo desturi ya CCM.

Polepole alisema kuwa itakapothibitika taratibu zilivunjwa kwa hila, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa katiba na kanuni zinazoongoza uchaguzi, maadili ya viongozi na utumishi katika chama.

Alisema katika kikao hicho kilichokaa chini ya Mwenyekiri wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, Kamati Kuu inawataka Watanzania wajitokeze kwa wingi na kushiriki kwa amani kutumia haki yao ya kidemokrasia kuwachagua viongozi wao ambao watakamilisha safu ya uongozi wa awamu ya tano ambao umejipanga kuwaletea maendeleo kwa haraka.

BARUA YA CHADEMA

Kwa upande wake, Chadema jana kilisema kimewasilisha barua yenye taarifa ya malalamiko dhidi ya ukiukwaji wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kutokana na baadhi ya matukio yaliyofanywa na wasimamizi wa uchaguzi tangu kuanza kwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu Oktoba 29.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema barua hiyo iliandikwa Oktoba 29, 2019 na kutiwa saini na Reginald Munisi kwa niaba ya Katibu Mkuu na kuwasilishwa kwa Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo na Msajili wa Vyama vya Siasa jana.

“Juzi tulitoa malalamiko yetu ya ukiukwaji wa kanuni, ikiwa ni siku ya kwanza tu ya kuanza kwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu, tayari tumeshapeleka barua rasmi kwa waziri anayehusika na Msajili wa Vyama vya Siasa,” alisema Mrema.

Barua hiyo inatoa malalamiko ya ukiukwaji wa kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za mwaka 2019 zilizowekwa katika tangazo la Serikali Namba 371 la Aprili 26, 2019 na mwongozo wa uchaguzi wa viongozi wa ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa uliotolewa na Tamisemi.

Alisema katika barua wameeleza baadhi ya matukio yaliyofanywa na wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi juzi ikiwa ni siku ya kwanza ya uchukuaji na urejeshaji fomu.

Mrema alisema matukio tisa yaliyoainishwa katika barua hiyo ni pamoja na wasimamizi na wasaidizi wao kutofungua ofisi ili kutoa fomu kwa wagombea wa Chadema hata baada ya muda wa kutoa fomu ambao ni saa 1.30 asubuhi.

Mengine ni wasimamizi na wasaidizi hao kutoa nakala zisizokuwa na nembo wala mihuri ya halmashauri, kutoa nakala za fomu bila kuambatanisha fomu za maadili na kukataa kutoa fomu za kuomba kugombea baada ya mgombea kurejesha fomu ya kuomba kuteuliwa.

Mrema alisema malalamiko mengine ni wasimamizi na wasaidizi wao kukataa kuwapatia fomu wagombea kwa kisingizio cha kutotoa mchango wa Mwenge, kudai maeneo yao yana wagombea wa CCM tu, kutoa fomu kwa wagombea wasiothibitishwa na chama, kunyimwa fomu kwa makusudi kwa wagombea katika baadhi ya maeneo na mgambo na polisi kutuhumiwa kukamata na kushikilia fomu za wagombea wa Chadema.

KAULI YA JAFO

Waziri wa Tamisemi, Jafo alithibitisha kupokea barua hiyo jana na kwamba pamoja na malalamiko hayo ya Chadema, amepata malalamiko mengi ya moja kwa moja kupitia ujumbe wa simu na simu kutoka maeneo mbalimbali nchini na tayari ameshatoa maagizo kwa watendaji kuhakikisha kasoro hizo hazijirudii.

Alisema katika kata 3,956 zinazoshiriki uchaguzi huo, wamepata malalamiko kutoka kata 333, yanayohusisha ucheleweshwaji wa fomu na mizengwe ya hapa na pale, hivyo kufanya kata 3,623 kutokuwa na malamamiko hadi kufikia jana.

“Kutokana na hali hiyo, tumetoa maelekezo ya jumla kwa wadau wote, kuanzia maofisa wanaotoa fomu na kuzipokea na wale washiriki kutoka vyama vyote vya siasa, kuhakikisha wanafuata kanuni, maelekezo na taratibu zilizowekwa.

“Kwa kuwa jana (juzi) ilikuwa ni siku ya kwanza, tumetoa maelekezo ili kutatua mapungufu yaliyojitokeza, kwa leo (jana) katika  maeneo mengi hatujapata malalamiko, ila tunatarajia kuwa malalamiko haya hayatajirudia kwa siku zilizobaki, hadi zoezi hili litakapomalizika Novemba 4,” alisema.

Alisisitiza barua hiyo ya malalamiko kutoka Chadema na kutoka kwa wagombea wa vyama vingine, ndiyo iliyomsukuma kutoa maelekezo ya pamoja jana ili kuhakikisha haki inatendeka katika mchakato huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles