|Bakari Kimwanga, Morogoro
Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amesema umeme wa mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge ndiyo utatumika kuendeshea treni mpya ya umeme.
Dk. Kalemani ameyasema hayo leo Mjini Morogoro, kwenye kikao cha mawaziri na makatibu wakuu ambao wizara zao zinatekeleza mradi huo.
“Mradi huu utazalisha Megawati 2,100 na ndiyo utakaotumika kuendeshea treni ya kisasa ya umeme ya Standard Gauge.
“Hivyo tumekutana hapa kujadili taarifa ya wataalamu kuhusu mradi, kutafakari changamoto na kuzifanyia kazi pamoja na kutembelea eneo la mradi,” amesema Dk. Kalemani.
Pia Waziri huyo wa Nishati, amesema Serikali itachukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayekwamisha uwekezaji wa mradi huo ambao unahusisha wizara 11.
Kikao hicho kimewakutanisha watalaamu na viongozi wengine mbalimbali wakiwamo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba.