26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Stars yapewa mbinu kuiliza Burundi Dar

Mohamed Kassara -Dar es salaam

BAADA ya timu ya Taifa Tanzania, Taifa Stars, kuanza kwa sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Burundi juzi katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022, wachambuzi wa soka nchini wameipa ujanja kuelekea mchezo wa marudiano utakaopigwa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii.

Stars ilipata sare hiyo, ukiwa ni mchezo wa kusaka tiketi ya kuingia makundi ya kufuzu fainali hizo za Dunia, uliochezwa kwenye Uwanja wa Inwari, jijini  Bujumbura.

Timu hizo zinatarajia kurudiana Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo mshindi wa jumla atatinga moja kwa moja katika hatua ya makundi ya kuwania tiketi hiyo.

Wakizungumza na MTANZANIA jana kwa nyakati tofauti, wachambuzi kadhaa wametoa maoni tofauti ya nini kifanyike ili kuifanya timu hiyo kuichapa Burundi.

Kocha wa Tanzania Prisons, Adorf Rishard alisema Stars isifikiri imemaliza kazi, badala yake inatakiwa kuongeza juhudi zaidi katika mchezo wa marudiano.

Alisema kocha wa Stars, Etienne Ndayiragije, anatakiwa kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa na nidhamu ya hali ya juu katika mchezo huo ili kuwanyima fursa wapinzani wao hao ya kupata bao la mapema.

“Nimefurahishwa na kiwango kilichooneshwa na timu yetu jana (juzi), nimpongeze mwalimu kwa timu kucheza kwa kufuata maelekezo kuanzia mwanzo hadi mwisho, ilikuwa inashambulia pia ilikuwa makini kudhibiti mashambulizi, kwa kweli  lengo la kwanza limetimia.

“Kikubwa kwenye mchezo wa marudiano ni kushambulia mwanzo mwisho, lakini hilo lisitufanye kuwapa nafasi wapinzani, tunatakiwa kucheza kwa nidhamu ya juu zaidi ya mchezo wa kwanza, hivyo kocha awaandae wachezaji kisakolojia wajue kwamba hawajamaliza kazi, badala yake wajitume  zaidi ili kushinda,” alisema kocha huyo ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji waliopeleka Stars katika fainali za Mataifa Afrika (Afcon) kwa mara kwanza mwaka 1980.  

Nahodha wa zamani wa  Stars, Ally Mayay alisema kocha Ndayiragije anatakiwa kutumia siku hizi chache kupunguza makosa kwenye safu ya ulinzi ili kuhakikisha timu hairuhusu bao nyumbani.

“Niliiona timu ilivyocheza jana (juzi), kiufupi ilicheza vizuri japo kuna mapungufu kadhaa yalionekana, mpango alioenda nao mwalimu wa kushambulia, ulizaa matunda, lakini shida ilikuwa kwenye eneo la ulinzi, hasa upande wa beki wa kulia na eneo la ushambuliaji.

“Katika mchezo wa marudiano, lazima ahakikishe anapata muunganiko mzuri kwenye eneo la ushambuliaji, alianza na Mbwana Samatta, Simon Msuva na Hassan Dilunga, lakini hakukuwa na nafasi ya kufunga waliyotengeza, alipoingia Idd Seleman hali ilibadili, hivyo ninaona kocha anatakiwa kufanya kila awezalo kuboresha eneo hilo,” alisema kiungo huyo zamani wa Yanga.

Naye, mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars, Peter Tino alisema timu hiyo ina nafasi kubwa kuichapa Burundi nyumbani, lakini hilo litazingatia na namna tutakavyouchulia mchezo huo.

“Tunaweza kuwafunga Burundi hapa nyumbani, lakini wachezaji wasijisahau, wahakikishe wanapambana kikweli kweli kwa kuwa wapinzani wao wana timu nzuri, hivyo wasipokuwa makini watajikuta wanapata matokeo wasiyoyatarajia nyumbani.

“Wasifikiri kupata sare ya 1-1 ndiyo watakuwa wamemaliza kazi, mchezo wa nyumbani utakuwa wa wazi sana kila timu ina nafasi sawa ya kushinda, Burundi watakuja kushambulia kwa kuwa hawana cha kupoteza, hivyo ni vema tahadhari zikachukuliwa mapema ili kuepuka kucheza kwa mazoea,” alisema Tino.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles