Molinga, Shikalo wakwama Caf

0
904

Mohamed Kassara Na Damian Masyenene

WACHEZAJI watatu wa kimataifa wa Yanga, David Molinga, Farouk Shikalo na Moustapha Selemani, hawatacheza mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United ya Zambia baada ya kushindwa kupata vibali kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Molinga alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga ambao walikosa michezo miwili ya hatua ya awali ya michuano hiyo dhidi ya Township Rollers baada ya leseni yake kuchelewa kutokana na kusajiliwa na timu hiyo wakati usajili wa CAF umefungwa, hivyo kutakiwa kulipa faini.

Hatua hiyo inaifanya Yanga kulazimika kusubiri kuwatumia wachezaji hao kwenye hatua inayofuata ya michuano hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mratibu wa kikosi cha Yanga, Hafidh Saleh alithibitisha wachezaji kukosa vibali, huku akieleza suala hilo limeachwa kwa uongozi ambao unajaribu kulitafutia ufumbuzi kabla ya mchezo dhidi ya Zesco.

“Ni kweli hadi sasa wachezaji wetu watatu Molinga, Shikalo na Seleman bado hawajapata vibali vya kucheza michezo ya kimataifa, hivyo kuna dalili za kukosa mchezo ujao, uongozi unaendelea kushughulikia suala hilo kuona linamalizika mapema.

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ameonyesha kufurahishwa na kambi ya Mwanza ambayo ni maalum kwa ajili ya kuikabili Zesco United.

Katika maandalizi hayo, tayari Yanga imewasili Mwanza kwa kambi ya siku tisa, ambapo ikiwa jijini hapa, itacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Pamba na Toto Africans (Septemba 10).

Mbali ya michezo hiyo, timu hiyo pia itashiriki katika shughuli za kijamii zilizoandaliwa na wanachama wa timu hiyo jijini hapa, ikiwamo kufanya usafi na kuchangia damu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, Jumamosi.

“Kambi ya Mwanza itasaidia, ile ya Moshi ilitupatia bahati hata kama tulikuwa na changamoto ya viwanja vya mazoezi, lakini hapa tuna viwanja vizuri pia tutapata mechi mbili za kirafiki.

“Hizo mechi mbili zitatusaidia kuandaa mpango wa mechi zetu mbili dhidi ya Zesco namna gani tutacheza, tutaendelea kufanya vitu ambavyo hatujafanya kwenye michezo mingine ya ligi itatusaidia kufanya vyema,” alisema Zahera.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here