Maregesi Paul, Dodoma
Spika wa Bunge, Job Ndugai ameitaka serikali kuangalia namna ya kuzuia unyanyasaji wanaofanyiwa watu na mifugo wakati wa kukabiliana na watu wanaoingia katika maeneo ya Hifadhi za Taifa na kwenye mapori ya akiba.
Amesema kwamba pamoja na kwamba wananchi wanatakiwa kufuata sheria, utaratibu wa kupiga risasi mifugo na kupiga wanachi hauwezi kukubaliwa kwa kuwa watendaji wa operesheni hiyo wanaweza kutumia adhabu mbadala dhidi ya wakosaji.
Spika Ndugai amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Mei 22, alipokuwa akiahirisha bunge baada ya mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/19.
“Kitendo cha kukamata au kuuza mifugo iliyokamatwa kinawafilisi wananchi na pia kinasababisha ndama wafe baada ya mama zao kuuzwa au kuuawa,” amesema.
Pamoja na hayo amesema washiriki wa matukio hayo wanatakiwa kuwa na ubinadamu kwani hata wao wakikamatiwa magari na nyumba zao na kuuzwa watajisikia vibaya.