33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

SPIKA: MWIJAGE LETE MAJIBU YA UHAKIKA

Gabriel Mushi, Dodoma

Spika wa Bunge, Job Ndugai amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kutoa majibu ya uhakika leo saa 11 jioni kuhusu uhaba wa mafuta ya kula nchini.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo Mei 8, bungeni jijini Dodoma, baada ya sakata hilo kuibuka tena kwa baadhi ya wabunge wa CCM akiwamo Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje na Hussein Bashe wa Nzega Mjini kuomba mwongozo kwa Spika kuhusu uhaba wa sukari na upungufu wa mafuta ya kula nchini ambapo wenye viwanda wamesitisha kuzalisha kwa kukosa mafuta ghafi.

Akiomba mwongozo huo, Bashe aliungana na Lubeleje na kusema kuwa bei ya mafuta aina ya Korie ya lita 10 imepanda kutoka Sh 23,000 hadi 40,000, lita 20 kutoka Sh 50,000 hadi 73,000.

“Huoni kuna haja ya kutoa muongozo kuwa serikali ije na kauli rasmi kuhusu hii mgogoro wa mafuta na sukari tunafanya nini kama nchi kuweza kumpunguzia mzigo mwananchi kwani ongezeko la bei ni zaidi ya asilimia 20 kwa kipindi cha miezi mitatu wakati waziri jana alisema bado upimaji unaendelea kati ya taasisi ya TBS (Shirika la Viwango), Mkemia mkuu wa serikali na UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam),” amesema.

Kutokana na miongozo hiyo, Spika Ndugai alisema licha ya waziri kutoa maelezo bado hayatoshelezi hivyo aeleze tena kwa kuwa ongezeko la takwimu hizo ni kubwa.

Akitoa ufafanuzi, Mwijage alimuomba Spika ampe muda hadi saa 11 jioni leo atapeleka majibu ya uhakika kuhusu sakata hilo.

“Ningependa watu waelewe vizuri ongezeko la uhaba wa mafuta, watu walielewe vizuri suala hili, Tanzania tunazalisha mafuta kutokana na mbegu mbalimbali za alizeti, karanga ufuta na pamba.

“Kiasi hakikidhi mahitaji kwani tunazalisha asilimia 30 kutokana na mbegu, zile asilimia 30 zinazobaki zina soko huuzwa nje ya nchi kama Sweden, ili kukidhi mahitaji ya nchi huagizwa mafuta ghafi au yaliyosafishwa kutoka nchi za Indonesia na Malaysia.

Baada ya ufafanuzi huo wa waziri, Spika Ndugai alisema: “Bahati nzuri nitakuwa hapa, ni utamaduni duniani kote tunapokuwa bungeni lazima tuseme ukweli, ukigeuza Bunge kuwa mahali pa kubangaiza hivi haitakuwa sawa sawa, kwa hiyo saa 11 tuje na maelezo ya jambo hilo.

“Nimetoa nafasi hiyo kidogo tupate picha ya serikali, mnatukifikisha mahali pagumu sana kwa mambo madogo sana, hivi kweli nchi hii leo wale wote tuliosoma Chemistry (Kemia) kupima mafuta kujua ghafi au safi hiyo ina maajabu gani?

“Kitu cha dakika 15, watu wanazunguka na nilisema siku ya waziri, kama TRA hamuwaamini, mkemia mkuu ana maabara yake, pelekeni Afrika Kusini, Nairobi au London dakika  chache majibu unapata, unapiga kodi mambo yameisha”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles