33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

SONKO AMPENDEKEZA MIGUNA MIGUNA UNAIBU GAVANA

NAIROBI, KENYA


GAVANA wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko, amempendekeza mwanasiasa mtata wa upinzani, Miguna Miguna, kuwa naibu gavana wa kaunti hiyo.

Sonko alitoa tangazo hilo lisilotarajiwa juzi jioni kwa njia ya barua kwenda kwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, akisema Miguna ametimiza matakwa yote yanayohitajika kikatiba.

Barua hiyo ilianza kusambaa kwenye mitandao ya jamii usiku wa juzi na kuzua mjadala miongoni mwa Wakenya kutokana na uteuzi wake kuja wakati usiotarajiwa.

Wakili huyo amevunja ukimya, akiviambia vyombo vya habari jana kuwa hana habari na uteuzi huo, akiutaja kama hatua ya kukwepa hali halisi.

“Sina taarifa katika kile karibu kila mtu anaonekana kukizungumza. Ni njama za kukwepesha hali halisi,” alisema Miguna.

Lakini iwapo atakubali, ndoa yake ya kisiasa na Gavana Sonko huenda ikakabiliwa na vizingiti kadhaa vya kisheria, kisiasa na kimaadili.

Ijapokuwa mawakili wa mwanasiasa huyo wa upinzani, Cliff Ombeta na Nelson Havi, wameelezea matumaini yao kuwa atakubali kuwa Naibu Gavana wa Nairobi, kuna vizingiti, ambavyo huenda vikakwamisha ndoto hiyo.

Chini ya Katiba ya Kenya, katika Kipengele cha Sita cha Uraia na Uongozi, ofisa yeyote wa Serikali sharti awe raia wa Kenya.

“Ofisa wa Serikali au ofisa wa jeshi hatakubaliwa kuwa na uraia wa mataifa mawili,” kinanukuu Kipengele cha pili (78) 2 cha Katiba.

Miezi miwili iliyopita, Serikali ilimfurusha Miguna hadi Canada ambako ni raia na kutangaza kitambulisho chake cha Kenya hakitambuliki.

Miguna ambaye ana uraia wa Canada na Kenya, alitarajiwa kurudi nchini hapa juzi kutoka Canada licha ya kutimuliwa mara mbili na Serikali katika kipindi cha miezi mitatu kwa madai aliukana uraia wake.

Aliahirisha safari yake kurudi hapa, akisema Idara ya Uhamiaji haikumpatia paspoti halali kama ilivyoagizwa na mahakama.

Alikuwa arudi nyumbani siku ambayo barua ya kuteuliwa kwake inaaminika kuandikwa.

Hata hivyo, Miguna ameshikilia kuwa hataomba paspoti ya Kenya na kusisitiza yeye ni Mkenya kwa kuzaliwa.

Iwapo Miguna ataondolewa vizingiti vya kisheria, atakabiliwa pia na kibarua kigumu cha kuwashawishi madiwani wa Kaunti ya Nairobi kumwidhinisha.

Kaunti ya Nairobi ina madiwani 124 na Miguna atahitaji kuungwa mkono na madiwani wasiopungua 90 ili aweze kuwa naibu gavana.

Nafasi ya naibu gavana wa Nairobi ilibaki wazi kufuatia kujiuzulu kwa Polycarp Igathe Januari 12, mwaka huu baada ya kutoelewana na Sonko katika usimamizi wa masuala ya Kaunti.

Igathe kwa sasa ameteuliwa kuwa mmoja wa maofisa wa wakuu wa Benki ya Equity, moja ya benki kubwa zaidi nchini hapa.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Beatrice Elachi, alisema Miguna atahitajika kutatua masuala kuhusu uraia wake na Serikali ya Kenya kabla kuhojiwa na wabunge wa jimbo hilo.

“Gavana ametupatia jina la aliyempendekeza. Tutafuata sheria. Katiba iko wazi kuwa naibu gavana lazima awe raia wa Kenya.

“Ningemshauri Miguna atatue kwanza matatizo yake na Serikali ya Kenya. Yeye ni raia wa Canada. Shughuli hii itatuchukua miezi mitatu hadi minne,” Elachi alikaririwa na Kituo cha Redio cha Hot 96 FM akisema.

Wakati kukiwa na utata kuhusu iwapo Miguna ataidhinishwa, wanasiasa na wananchi wamegawanyika kuhusu uteuzi wake huo.

Seneta wa Nairobi, Johnson Sakaja, ameandika kwenye Twitter kuwa mwanasiasa huyo hawezi kuwa naibu gavana wa Nairobi.

Aidha Kiongozi wa wengi katika Kaunti ya Nairobi, Abdi Guyo, juzi jioni aliongoza madiwani wa Jubilee kupinga uteuzi huo, akisema Miguna si mwanachama wa chama chao.
Lakini chama hicho tawala kinaonekana kugawanyika, huku kinara wa walio wengi bungeni, Aden Duale na mwenzake wa Seneti, Kipchumba Murkomen, wakiunga mkono na kuitaka Serikali impatie wakili huyo paspoti ili aweze kurejea nchini.
Uteuzi huu pia umewashangaza wengi, ikizingatiwa Sonko na Miguna wana sifa na maadili tofauti.
Wawili hao wamekuwa wakirushiana maneno makali na kutofautiana vikali kuhusu uongozi wa Jiji la Nairobi tangu kabla na baada ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Mei 2016, Sonko alisema licha ya Miguna kumshambulia kila mara, atakapochaguliwa kuwa gavana atampa wadhifa katika Serikali yake.

Sonko alionyesha dhamira hiyo Machi mwaka huu alipotoa orodha ya watu iliyomjumuisha Miguna kwenye ukurasa wake wa Facebook, akiomba maoni kutoka kwa wafuasi wake juu ya nani anayefaa zaidi kuwa naibu wake gavana.

Lakini Miguna alitumia maneno makali kumjibu gavana huyo: “Ndugu yangu Sonko, siwezi kuhudumu chini au pamoja na jambazi na unaelewa?”

Wakati wa mdahalo wa wagombea wa ugavana Nairobi, Miguna aliwakabili vikali Sonko na mtangulizi wake, Dk. Evans Kidero kwa kushirikiana na wahuni kufuja fedha za kaunti.

Kwa upande wake, Sonko alimjibu Miguna kwa kumtaja kama punguani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles