26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

WABUNGE WALALAMIKIA OPERESHENI SANGARA

Na MAREGESI PAUL-DODOMA


BAADHI ya wabunge, wamelalamikia mkakati wa Serikali wa kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, hatua inayotwa Operesheni Sangara.

Wamesema pamoja na nia njema ya kupambana na uvuvi huo, utaratibu unaotumika ni haramu kwa kuwa washiriki wa operesheni hiyo wanawanyanyasa wavuvi na kuwasababishia umaskini.

Malalamiko hayo yalitolewa jana na wabunge hao walipokuwa wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Masele (Chadema), aliitaka Serikali iangalie upya utekelezwaji wa operesheni hiyo kuepuka madhara yanayoweza kuendelea kutokea.

“Mheshimiwa mwenyekiti, hiyo operesheni ya kuzuia uvuvi haramu naiomba Serikali iiangalie upya kwa sababu wavuvi wananyanyaswa kwa kupigwa na kutozwa faini kubwa ambazo hazitambuliwi katika sheria.

“Pia, naomba Serikali iifanyie mabadiliko ile sheria ya uvuvi na itakapokuwa ikibadilishwa wadau wa uvuvi washirikishwe kwa sababu ndiyo wanaohusika moja kwa moja na masuala ya uvuvi,” alisema Masele.

Mbunge wa Viti Maalumu, Agness Marwa (CCM), alisema kutokana na madhara wanayopata wavuvi kupitia Operesheni Sangara, kuna haja Rais Dk. John Magufuli na mamlaka nyingine, aingilie kati kuwanusuru wavuvi.
Pamoja na hayo, mbunge huyo alilitaka Bunge liunde kamati maalumu ya kufuatilia operesheni hiyo ingawa pia Waziri Mpina anaweza kujiuzulu uwaziri kama ataona ameshindwa kutimiza wajibu wake.

Mbunge wa Viti Maalumu , Felister Bura (CCM), alisema kuna kila sababu kwa Serikali kuingilia kati utendaji wa operesheni hiyo kwa kuwa baadhi ya wavuvi wamefariki dunia baada ya samaki na nyavu zao kukamatwa na kudaiwa kulipa faini kubwa za fedha ambazo hawana.

“Hiyo Operesheni Sangara na nyingine zinazofanyika katika Maziwa ya Tanganyika, Nyasa na Rukwa, zimewafanya watu wapoteze maisha kwa sababu wanapokamatwa, wanatozwa faini kubwa za fedha,” alisema Bura.

Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM), alisema washiriki wa Operesheni Sangara wanaitumia vibaya operesheni hiyo kwa kuwanyanyasa wavuvi kwa kuwa wanakamata nyavu zenye matundu makubwa ambayo hayana madhara katika uvuvi.

Mbunge wa Monduli, Julius Karanga (Chadema), alisema wafugaji wataendelea kusafirisha mifugo yao kwenda nje ya nchi kupitia njia za panya kwa kuwa mazingira ya ufugaji nchini ni mabaya.

WAZIRI MPINA

Awali, akiwasilisha bajeti ya wizara yake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, alisema wakati wa Operesheni Sangara iliyoanza mwaka jana, viongozi na watumishi 35, walikamatwa wakijihusisha na uvuvi haramu.
Aliwataja watumishi na viongozi hao kuwa ni wenyeviti wa halmashauri, madiwani, wenyeviti wa serikali za vijiji, maofisa uvuvi, vyombo vya ulinzi na usalama na watumishi wengine.

Mpina alisema Serikali iliamua kuanzisha operesheni hiyo baada ya kufanya tathmini ya sekta ya uvuvi na kubaini kasoro mbalimbali katika sekta hiyo katika Ziwa Victoria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles