30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

‘SIMU, SIGARA HUINGIZWA GEREZANI KAMA DAWA ZA KULEVYA’

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

JESHI la Magereza limesema mahabusu wanaingiza sigara na simu za mkononi gerezani kwa njia ya haja kubwa na ukeni kama wanavyosafirisha dawa za kulevya.

Hayo yalibainishwa jana na ASP Absalom Mokily, anayetoa elimu kwa wananchi katika banda la Magereza, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria.

“Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Magereza namba 149 ya mwaka 2003, inazuia kabisa baadhi ya vitu kuingizwa gerezani, ikiwemo simu, silaha, kisu, nondo bila ruhusa.

“Mahabusu wanaokwenda mahakamani na kurudi ndio wanaosababisha kuingia kwa simu gerezani, wapo wafungwa unawakuta wana pakiti hata tatu za sigara.

“Kama wanavyosafirisha dawa za kulevya kupitia njia ya haja kubwa na vitu kama sigara na simu zinaingia gerezani kwa mfumo huo kwa wanaume… kwa wanawake wanaingiza vitu hivyo kwa kuficha ukeni.

“Tukifanya upekuzi ule wa kuwabinua na kuwapekua katika makalio, wanasema tunawadhalilisha, pale tunapotumia utu katika upekuzi, wao wanaitumia vibaya nafasi hiyo,” alisema.

ASP Mokily alisema kwa mujibu wa kanuni zao, mtumishi akibainika ameingiza vitu hivyo na kumpa mfungwa ama mahabusu, anafukuzwa kazi na mahabusu ama mfungwa akikutwa navyo anafikishwa mahakamani.

“Tukubali sisi ni binadamu, huwezi kumdhibiti mtu kwa asilimia 100, mahabusu ndio wanaingiza vitu gerezani, mfungwa hawezi kwa sababu sehemu anazokuwepo hazina maduka, mfano shambani.

“Kuna kifaa cha ukaguzi, kile kifaa kinatambua vitu vya chuma, lakini plastiki hakiwezi kutambua kama imeingizwa kwenye haja kubwa ama ukeni.

“Tatizo hili si kubwa sana kama linavyozungumzwa kwa sababu linatokea zaidi magereza yaliyopo mijini, kwa sababu yanabeba wafanyabiashara, lakini mikoani huwezi kukuta matatizo kama haya,” alisema.

Akizungumzia hoja ya mahabusu na wafungwa wa kike kutoka gerezani wakiwa wajawazito ama na watoto, alisema taarifa hizo si sahihi.

“Uwezekano wa mahabusu ama mfungwa mwanamke kukutana na mwanaume faragha ni mdogo kutokana na mazingira ya magereza, mazingira yake si rafiki kwa tendo la ndoa.

“Wapo wafungwa ama mahabusu wanaoingia gerezani wakiwa wajawazito, mtu akiingia na ujauzito wa wiki ama siku huwezi kumjua, akikaa muda mrefu mimba inavyokua ndipo watu wanasema kapatia mimba gerezani.

“Anapoingia gerezani mfungwa ama mahabusu hakuna utaratibu wa kumpima mimba… kutokana na utengano wa mahabusu na wafungwa, hicho kitu hakuna, ni hadithi tu, hasa ukizingatia mlinzi wa mwanamke ni askari mwanamke,” alisema.

Alisema ukitafuta takwimu za wangapi waliwahi kupata mimba gerezani, huwezi kuzipata kwa sababu uhalisia na mipaka ya magereza ni vigumu mfungwa ama mahabusu kupata mimba.

ASP Mokily alisema sheria za magereza haziruhusu tendo la ndoa kwa mtu aliyekuwepo gerezani na kwamba miundombinu yake si rafiki kwa tendo hilo.

“Tendo la ndoa ni haki ya mtu, tutaruhusu pale ambapo sheria itaruhusu kwani tuko kwa ajili ya utekelezaji, lakini  kuna changamoto endapo kutakuwepo na sheria ya aina hiyo.

“Uraini kila siku unasikia watu wanakwenda kupima DNA kwa ajili ya kutaka kujua baba halisi wa mtoto, itakuwaje ikitokea mahabusu ama wafungwa waruhusiwe tendo la ndoa kisha wapate mimba wakiwa gerezani?

“Kama watu wako pamoja uraiani hawaaminiani je, mwanamke akitoka na mtoto gerezani mwanaume ataamini vipi kama mimba ilikuwa yake? Hiyo changamoto moja, lakini nyingine Serikali italazimika kuingia gharama kubwa ya kurekebisha miundombinu.

“Gharama itakuwepo ya kujenga mahali pa kukutana, gharama za kutunza wajawazito, mwingine anaweza kuwa na mimba anapasua tofali anakula, gerezani hakuna matofali, huoni kama hizo ni gharama nyingine?” alihoji.

Alisema kwa kuzingatia haki za binadamu, kwa baadae kama itaonekana kuna haja ya kuwepo kwa faragha gerezani, idara mbalimbali na wadau wafanye mjadala mpana utakaowezesha kufanya mabadiliko ya sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles