31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, Yanga safi, Azam yapigwa

chirwaMWANI NYANGASSA, MBEYA Na THERESIA GASPER- DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Simba jana iliendelea kuwasha moto kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuchomoza na ushindi ugenini wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Matokeo hayo yalizidi kuwapa jeuri Simba ya kuendelea kukomaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 20 wakiwa wamecheza mechi nane, huku Stand United walioshinda bao 1-0 dhidi ya Azam FC wakijiimarisha nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi 19 baada ya kushuka dimbani mara tisa.

Wakati Simba ikiendelea kupeta kileleni, mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga nao walifanikiwa kurudi kwenye kasi yao baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-1, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Yanga iliyocheza mchezo wake wa saba jana, imefanikiwa kupanda hadi nafasi ya nne baada ya kufikisha pointi 14 sawa na wapinzani wao Mtibwa walioshuka nafasi ya tano, wakiwa wametofautiana kwa wastani wa mabao ya kufungwa na kufunga.

Kwa upande wao Azam walioanza ligi kuu msimu huu kwa kusuasua, waliendelea kupoteza matumaini ya kunyakua ubingwa baada ya kipigo walichopata ugenini dhidi ya wenyeji wao Stand katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Simba kwa upande wao walifunga bao la kuongoza dakika ya sita kupitia kwa Ibrahim Ajib, baada ya kupiga shuti la mpira wa adhabu uliotokana na Shiza Kichuya kuangushwa ambao ulitinga moja kwa moja wavuni.

Dakika ya 15, Fredrick Blagnon wa Simba ambaye aliangushwa katika eneo la hatari na Sankhani Mkandawile wa Mbeya City, aliikosesha Simba bao la pili baada ya kukosa penalti iliyotolewa na mwamuzi, Alex Mahagi.

Simba ambao walitawala zaidi mpira kipindi cha kwanza, waliendeleza mashambulizi na kufanikiwa kutikisa nyavu kwa mara ya pili dakika ya 34 mfungaji akiwa Kichuya, baada ya kuambaa na mpira kutoka winga ya kushoto na kupiga shuti lililojaa wavuni.

Baada ya mapumziko, Mbeya City walifanya mabadiliko ya kumtoa John Kabanda na kuingia Hemed Mirutabose ambaye alibadili kasi ya mpira na kufanya shambulizi kali dakika ya 51 ambalo  halikuzaa matunda.

Kwa upande wa Yanga, Mzambia Obrey Chirwa, alizinduka na kufunga bao lake la kwanza ligi kuu katika dakika ya 45, baada ya kuunganisha krosi iliyopigwa na Simon Msuva kabla ya Mtibwa kusawazisha dakika ya 63 kupitia kwa Haruna Chanongo, baada ya kutokea piga nikupige langoni kwa Yanga.

Simon Msuva aliiandikia Yanga bao la pili dakika ya 68, baada ya kuambaa na mpira na kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Mtibwa, Benedict Tinoco, huku Donald Ngoma aliyeingia kipindi cha pili akifunga bao la tatu dakika ya 79 akiunganisha pasi safi ya Geofrey Mwashiuya.

Katika michezo mingine ya ligi hiyo, Mwadui FC iliibamiza African Lyon mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga huku Kagera ikichomoza na ushindi ugenini wa bao 1-0 dhidi ya Majimaji ya Songea.

Mbao FC iliwachakaza ndugu zao Toto Africans kwa kuwafunga mabao 3-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza huku maafande wa JKT Ruvu wakitoka suluhu nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles