Na ZAINAB IDDY – DAR ES SALAAM
LICHA ya juzi Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, kuiomba msamaha Simba kutokana na kauli yake kwamba klabu yake imefanya mazungumzo na kiungo Clatous Chama, Wekundu hao wameonekana kukomaa naye baada ya kuwasilisha malalamiko Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Juzi Mwakalebela akifanya mahojiano na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam, alisikika akieleza kuwa Yanga imefanya mazungumzo na nyota huyo wa Simba, ili kuangalia uwezekano wa kumsajili ili awatumikie msimu ujao.
Lakini baada ya Mwakalebela kusikika akifichua hilo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara katika mahojiano na kituo hicho hicho cha redio alisema wanakusudia kumshtaki kiongozi huyo kwa kuvunja kanuni za usajili.
Manara alisema, kilichofanywa na Mwakalebela ni uvunjaji wa kanuni za usajili za TFF na hata Shirikisho la Soka la Kimataifa(Fifa), ambazo zinakataza klabu kufanya mazungumzo na mchezaji anayemilikiwa na klabu nyingine, ikiwa bado ana mkataba wa zaidi ya miezi sita.
Kwa mujibu wa Manara, Chama ambaye ni raia wa Zambia, mkataba wake na Wekundu hao utafikia tamati Julai mwakani.
“Chama ana mkataba hilo halina ubishi na TFF na vyombo vingine wanajua, nashangaa kiongozi mkubwa wenye uzoefu wa soka kama Mwakalebela anazungumza vitu ambavyo ha ukakika nayo.
“Hata mtu akienda TFF leo hii, mkataba wa Chama uko pale ataangalia na kujiridhisha, anamaliza mkataba Julai 2021, iko wazo kabisa,” alisema Manara.
Baada ya Manara kutangaza azma ya klabu yake kulifikisha jambo hilo TFF, saa chache baadaye, Mwakalebela, alijitokeza na kuomba radhi wapenzi wa soka nchini kupitia mitandao ya kijamii na vituo mbalimbali vya redio, ambapo alisema:
“Napenda kuchukua nafasi hii kuweza kuelezea suala lilijitokeza la kumzungumzia mchezaji wa Simba, Chama, inaonekana Simba hawajalipokea vizuri, lakini ukweli nilikua nafanya utani kama walivyokuwa wanatufanyia wao kwa Tshishimbi.
“ Naomba msamaha kwa Simba na wapenzi wa Yanga, nimefanya vile nikijua ni utani wa jadi tuliokuwa nao kwa sababu hapa katikati tumekuwa tukitaniana kuchukuliana wachezaji, naomba radhi pia kwa TFF, sijazungumza na mchezaji huyo.
“Ninaahidi jambo hili halitajitokeza, nadhani utani nilifanya ulivuka mipaka, naomba jambo hili limalizike na tuendelee na urafiki wetu kama kawaida,” alisema.
Mwakalebela ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF, alikiri kuwa kama kiongozi wenye weledi, akimhitaji mchezaji huyo alitakiwa kwenda kuzungumza na uongozi wa Simba kwanza.
Jana mchana, Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo alitoa taarifa ya kupokelewa kwa barua ya Simba ikilitaka shirikisho hilo kumchukulia Mwakalebela kutokana na kitendo cha uvunjaji wa kanuni za soka.
Taarifa ya Ndimbo ilieleza kuwa , tayari suala hilo limewasilishwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ambayo ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.