24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Simba nje ‘FA Cup’

32*‘Waarabu wa Tanga’ Coastal Union wawatandika 2-1

NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM

WEKUNDU wa Msimbazi Simba, jana walitupwa nje ya michuano ya Kombe la FA, baada ya kufungwa bao 2-1 na Coastal Union na kupoteza matumaini ya kucheza michuano ya kimataifa kupitia kombe hilo.

Mchezo huo wa mwisho wa robo fainali ya michuano hiyo, ulichezwa kwenye  Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Coastal Union walianza kuliona lango la Simba kwa kupata bao la kuongoza dakika ya 19 ya mchezo kupitia kwa mchezaji wake, Yusuph Sabo.

Bao hilo liliongeza kasi kwa Coastal ambao dakika ya 30, walipoteza nafasi ya wazi ya kujipatia bao kupitia kwa mchezaji wake, Ahmed Shiboli, aliyeunganisha vema pasi ndefu ya Juma Maazi.

Coastal Union walifanya mabadiliko  dakika ya 35 ili kuongeza nguvu kwa kumpuzisha, Ibrahim Twaha na nafasi yake kuchukuliwa na Nassoro Kapama.

Wagosi hao wa Kaya kutoka Tanga, walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili Simba walirejea uwanjani na kocha Jackosn Mayanja kufanya mabadiliko kwa kumtoa  Justice Majabvi na kumuingiza Hamis Kiiza.

Mabadiliko hayo yaliweza kuzaa matunda kwa Simba kwani dakika ya 49 Kiiza alisawazisha bao akiunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na Ibrahim Ajib.

Bao hilo liliwaamsha wachezaji wa Coastal Union, ambao walipeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Simba bila mafanikio.

Dakika ya 63 mwamuzi wa mchezo huo, Anderw Shamba, alimuonyesha kadi ya njano, Adeyun  Saleh wa Coastal Union, baada ya kumtolea maneno machafu mshika kibendera.

Mayanja aliongeza nguvu tena kwa kufanya mabadiliko dakika ya 66, alimtoa Daniel Lyanga na kumuingiza Paul Kiongera, huku Abdulhalim  Humud wa Coastal Union akionyeshwa kadi ya njano dakika ya 80 kwa kumfanyia madhambi Lufungo.

Novatus Lufungo aliiua timu yake ya Simba katika dakika ya 83, baada ya kumwangusha Shiboli aliyekua akielekea langoni mwao ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kumzawadia kadi nyekundu hivyo kupelekea Coastal Union kupata penalti iliyopigwa na Sabo ambaye aliiwezesha  timu hiyo kutinga hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa mabao 2-1 baada ya kufunga penalti hiyo kwa ustadi.

Wakati huo huo droo ya nusu fainali ya kombe hilo, inatarajiwa kufanyika leo saa tatu usiku na kuonyeshwa moja kwa moja ‘live’ kupitia kituo cha runinga cha Azam Two,  kwa kuzihusisha timu za Azam FC, Mwadui FC na Yanga SC.

Michuano hiyo iliyoanza kwa kushirikisha timu 64 mwishoni mwa mwaka jana, imefikia hatua ya nusu fainali baada ya Azam FC kuiondoa Prisons (3-1), Mwadui FC kuiondosha Geita Gold (3-0), Yanga SC kuwaondoa Ndanda FC kwa mabao (2-1) na Coastal Union kuitupa nje Simba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles