22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Azam: Esperance si ya kutisha sana

EsperanceNA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

BAADA ya ushindi wa bao 2-1 katika ardhi ya nyumbani, klabu ya Azam imesema kuwa timu yao haina tofauti kubwa na timu ya Esperance, tofauti yao ni kuwa wenzao wana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira.

Azam ilichanga karata zake vizuri Jumapili kwa kufanikiwa kuwafunga Waarabu hao wa Kaskazini mwa Afrika, katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Mabao ya Azam yalifungwa na Farid Mussa dakika ya 68 na Ramadhani Singano ‘Messi’ dakika ya 70, huku bao la wapinzani wao hao likifungwa dakika ya 33 na Haithem Jouini

Akizungumza baada ya kumalizika mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam, Denis Kitambi, alisema wapinzani wao wameonekana kuimudu sana mbinu hiyo ya kumiliki mpira kwa muda mrefu licha ya kutoibuka na ushindi.

“Hilo ndilo tatizo lililopo kwenye timu yetu na ndicho kitu pekee walichotuzidi Esperance, wachezaji wetu wamekuwa na tatizo la kushindwa kumiliki mipira kwa muda mrefu hasa kwenye mechi za kimataifa, tutahakikisha tunalifanyia kazi kabla ya kurudiana nao,” alisema.

Alisema licha ya kufanikiwa kupata ushindi, wana kazi kubwa mbeleni kuhakikisha wanapata mabao mengi zaidi kwenye mchezo wa marudiano Aprili 20 mwaka huu, Uwanja wa Rades Tunis, ili waweze kupenya hatua hiyo na kusonga mbele.

“Tumepata ushindi wa mabao 2-1 lakini haututoshi kujihakikishia wepesi kwenye mchezo wa marudiano kwani wapinzani wetu wana faida ya bao la ugenini, hivyo tunahitaji tupate mabao mengi ili kujiweka salama zaidi katika kufuzu hatua inayofuata,” alisema.

Alisema katika mchezo huo walilazimika kutumia mfumo wa aina mbili 4-3-3, ambapo baadaye walirejea katika mfumo wa kawaida wa 3-5-2, ili kwenda sambamba na wapinzani wao.

“Kukosekana kwa Shomari Kapombe kwa asilimia 70 kulisababisha kubadilisha mfumo wetu wa 3-5-2, ambao tumekuwa tukiutumia mara nyingi na kuufanyia mazoezi kwa kipindi chote, hivyo kulazimika kutumia mfumo huu wa 4-3-3 kabla ya kurudi kwenye mfumo wetu huo wa awali,” alisema.

Alisema licha ya John Bocco kutokuonyesha mchezo mzuri na kushindwa kumaliza nafasi za wazi walizopata, lakini walilazimika kumtumia kwa faida ya urefu wake ili kudhibiti mipira ya juu kutokana na wapinzani wao kuwa warefu.

“Hatukuwa na namna ya kumtoa Bocco hata kama hakuonyesha kiwango kizuri na Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’, kwa faida ya urefu wao ili waweze kuokoa mipira ya juu,” alisema.

Alisema kikosi chao kilifanikiwa kutengeneza nafasi nyingi za kupachika mabao lakini walishindwa kuzitumia na kufanikiwa kutumia makosa ya dakika tano waliyoyafanya Esperance kupata mabao hayo.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Esperance, Ammar Souayeh, amesema hali ya hewa ilichangia kuwatoa mchezoni dakika za mwishoni wachezaji wake na kujikuta wakiwapa nafasi Azam ya kushinda.

Ammar, alisema hali ya hewa ilibadilika hivyo kuwapa wakati mgumu wachezaji wake na kujikuta wakitoka mchezoni na kuwapa nafasi nzuri Azam kutumia mapungufu hayo kupata ushindi.

“Tumepoteza mchezo dakika za mwishoni ambapo wapinzani wetu wameweza kuzitumia vizuri dakika tano walizopata, lakini matokeo haya ni sawa na kupata sare hivyo tunahitaji kuhakikisha tunawafunga nyumbani na kusonga mbele,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles