Na Asifiwe George, Dar es Salaam
SHIRIKA la Maendeleo la Japan (JICA) na Wizara ya Fedha na Mipango, wamesaini mkataba wa mkopo wa Sh bilion 116 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mwakilishi Mkuu wa Ofisi ya JICA Tanzania,Toshio Nagase, alisema mradi huo utahusisha mfululizo wa mageuzi ya sera za maendeleo ambao utaondoa vikwazo katika mazingira muhimu ya biashara, hasa sekta ya viwanda na kutoa ajira.
Alisema mradi huo, utashughulikia maeneo makuu yenye vikwazo kwa lengo la kurahisisha usajili wa biashara na upatikanaji wa leseni ili kupata ufanisi na umahiri wa utawala wa forodha hasa katika bandari.
“Shirika limedhamiria kuunga mkono Serikali mpya katika njia mbalimbali ili kuharakisha juhudi za kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda na uchumi wa kati kama ilivyoainishwa katika Dira ya Mandeleo ya mwaka 2025 , “alisema.
Naye Ofisa Habari wa JICA, Helen Masele alisema mkopo huo pia utasaidia kuboresha ufanisi wa ulipaji na urekebishaji motisha ya kodi.
Wakati huo huo, shirika hilo limekubali kufanya utafiti wa awali wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya usambazaji wa maji visiwani Zanzibar.
Alisema madhumuni ya utafiti huo, ni kufanya upembuzi yakinifu wa mradi kitaalamu kwa lengo la kuboresha mazingira ya kuishi kwa watu wa Zanzibar.
“JICA imekuwa ikisaidia miradi miwili ya sekta ya maji tangu mwaka 2005/2010, ambapo zaidi ya Sh bilioni 50 zilijenga visima vikubwa, hifadhi za maji, mabomba ya maji na vifaa vya usambazaji wa maji,” alisema Masele.