Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
ALIYEKUWA Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, amedai mahakamani kwamba akiwa madarakani hakuwahi kuziona barua zilizotoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zikizuia Kampuni ya Alex Stewart kusamehewa kodi.
Mgonja alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya jopo la mahakimu linaloongozwa na John Utamwa, Saul Kinemela na Sam Rumanyika.
Katibu Mkuu huyo wa zamani alikana kuziona barua hizo, alipoulizwa swali na Wakili wake, Profesa Leonard Shahidi.
Aliulizwa iwapo aliwahi kuiona barua ya TRA iliyoandikwa Juni 24, mwaka 2003, kwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ikizungumzia msamaha wa kodi usitolewe kwa Kampuni ya Alex Stewart.
Alidai hakuwahi kuziona barua hizo akiwa katika wadhifa ya Katibu Mkuu badala yake amekuja kuziona mahakamani.
“Nisingeweza kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kuzuia mchakato wa kuipa msamaha Kampuni ya Alex Stewart. Nilimshauri Waziri wa Fedha kuisamehe kodi kampuni hiyo kama inavyofanywa kwa makampuni mengine kwa sababu mkataba ulikuwa tayari umeshasainiwa,”alidai.
Alidai ilikuwapo barua kutoka kwa Waziri wa Fedha wakati huo akiwa Basil Mramba kwenda kwa Katibu Mkuu akiomba ushauri kuhusu msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.
Waziri katika barua yake, alisema kampuni hiyo ilianza kudai madai yake kwa kazi iliyopewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kwamba hakudhani kama wangetiliana saini bila kuliarifu Baraza la Mawaziri hivyo alimtaka Mgonja kuandika muhtasari upelekwe katika baraza hata kama
walikuwa wamechelewa.
Anadai baada ya kuombwa katika barua hiyo kutoa ushauri alipeleka kwa mwanasheria wa wizara kwa ajili ya ushauri lakini hakumbuki alimshauri kitu gani na kama alijibu labda Katibu Mkuu mwingine alipokea na kulifanyia kazi.