NA THERESIA GASPER
MWANAMITINDO na mbunifu wa mavazi nchini, Johar Sadiq, ameanzisha mradi maalumu unaojulikana kama Binti Foundation, ambao lengo lake ni kusaidia mahitaji mbalimbali kwa watoto wa shule za msingi nchini.
Johari alisema wameanza na wanafunzi 500 kutoka shule nne za Kinondoni ikiwemo shule ya Kumbukumbu, Mwananyamala, Msasani na Ananasifu.
“Awali tulikuwa tumelenga watoto wa kike lakini kwa sasa tumeona ni vema tusaidie kwa wanafunzi wote wakike na wakiume lengo ni kumsaidia mwanafunzi kupata mahitaji ambayo yatamuwezesha kumsaidia katika masomo yake,” alisema.
Alisema japo kwa sasa kuna mfumo wa elimu bure, lakini kuna vitu vingine wazazi hawawezi kuvimudu hivyo mradi huo utawasaidia kupata madaftari, kalamu, viatu, nguo za shule na vitu vingine mbalimbali.