24 C
Dar es Salaam
Thursday, October 3, 2024

Contact us: [email protected]

Shule ya Sekondari ya Sayansi ya Mtakatifu Joachim yafikisha miaka 10 ya mafanikio

Na Safina Sarwatt, Same

Mwaka 2013, Kanisa Katoliki Jimbo la Same lilianzisha Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Mtakatifu Joachim, yenye mchepuo wa sayansi, ikiwa na lengo la kupanua wigo wa wataalamu wa masomo ya sayansi na kuleta mageuzi katika maendeleo ya taifa.

Shule hii imejikita katika kuwapa vijana wa Kitanzania elimu bora na malezi mazuri ili kukabiliana na upungufu wa wataalamu wa sayansi, hasa wakati huu ambapo nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 10 ya shule hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Same, Mhashamu Baba Askofu Rogate Kimaro, alielezea changamoto zilizowakabili mwanzoni na mafanikio waliyopata.

“Tulianza kwa changamoto nyingi, lakini kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu na nia ya dhati ya kutoa huduma kwa jamii, tumeweza kufika hapa,” alisema Askofu Kimaro.

Shule hii, iliyosajiliwa mwaka 2013, imepata msaada mkubwa kutoka kwa serikali na wahisani kama Italia, huku ikifanya juhudi za kuboresha elimu kwa kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujitegemea.

Meneja Mkuu wa shule, Padre Deogratius Mchagi, alieleza kuwa shule imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na uongozi makini na jitihada za walimu na wanafunzi.

Shule ina maabara za kisasa, maktaba kubwa, na inatoa mafunzo ya vitendo kama vile kutengeneza mabwawa ya samaki na bustani za mboga. Pia, mazingira bora yamewezeshwa kwa kupandwa miti zaidi ya 4,000 kama sehemu ya juhudi za utunzaji wa mazingira.

Mkuu wa shule, Charles Shogolo, alieleza kuwa wanafunzi wamekuwa wakifaulu vizuri kwenye mitihani ya kitaifa, na malengo yao ni kufikia viwango vya juu zaidi.

Mwenyekiti wa bodi ya shule, Angella Kessy, alionyesha furaha kwa wazazi wanaowapeleka watoto wao katika shule hii. Alitoa wito kwa wazazi kuwa na muda wa kutosha kwa ajili ya malezi ya watoto, akisema, “Wazazi wanapaswa kutafakari walipoteleza na kuanza upya majukumu yao.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles