NA ASHA BANI
BAADHI ya shule kongwe nchini hazitarajiwi kufunguliwa katika mwaka mpya wa masomo unaoanza kesho, kutokana na kutokamilishwa kwa ukarabati uliokuwa unaendelea.
Shule hizo ni pamoja na Jangwani Sekondari, Azania za Dar es Salaam na Milambo ya Tabora ambazo ni kati ya shule 89 zinazotakiwa kukarabatiwa katika programu maalumu ya Serikali iliyopangwa kufanyika ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana alipokuwa katika ziara ya kuangalia hatua iliyofikiwa ya ukarabati wa shule za Azania na Jangwani, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leornad Akwilapo, alisema wizara inaendelea na programu hiyo.
Hata hivyo, Akwilapo aliwapa karipio na onyo kali Wakala wa Majengo (TBA) kwa kushindwa kusimamia na kutekeleza miradi hiyo kwà wakati kama ambavyo mkataba unasema jambo lililowafanya kusogeza mbele siku ya ufunguzi wa shule hizo hadi Januari 22.
Alisema wizara baada ya kufanya tathmini ya kina, imegundua kuwa kwenye shule zinazokarabatiwa na TBA, kumekuwa na tatizo la ukamilishwaji wa miradi katika muda uliopangwa.
Shule nyingine zinazokarabatiwa na TBA ni Kibaha, Kigoma, Tosamaganga, Malangali, Minaki na Nangwa.
“Miradi yote iko nyuma ya ratiba, na mbaya zaidi ni kwamba baadhi ya shule haziko tayari kabisa kupokea wanafunzi na wakaendelea na masomo yao kwa ukamilifu, yaani mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji hayajakamilika.
“Hivyo basi, baada ya mashauriano na wenzetu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, tumekubaliana kuhairisha kuanza kwa muhula wa kwanza kwa shule za Milambo, Jangwani na Azania,” alisema Dk. Akwilapo.
Alisema katika shule hizo muhula wa kwanza utaanza Januari 22 nà ratiba za masomo zitarekebishwa ili kufidiwa wakati wa likizo ndefu ya Julai.
Dk. Akwilapo aliwaagiza TBA, kutekeleza majukumu yao kulingana na mikataba waliyokubaliana, vinginevyo watachukuliwa hatua inayostahili.
Pia alielezea mchanganuo wa ukarabati wa shule hizo kuwa katika awamu ya kwanza ambayo imetekelezwa kwa miaka miwili tangu 2016, jumla ya shule 46 kati ya 89 zipo kwenye mpango wa ukarabati huo.
Alisema shule 10 za sekondari ambazo ni Mpwapwa, Musoma Ufundi, Mtwara Ufundi, Ifakara, Kantalamba, Tanga Ufundi, Ifunda Ufundi, Moshi Ufundi, Bwiru Wavulana na Kibiti, zinaendelea kukarabatiwa kwa usimamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST).
Pia Shule za Sekondari za Iyunga, Chidya, Tambaza, Zanaki na Kisutu zinakarabatiwa chini ya uongozi wa shule na bodi zao kwa usimamizi wa halmashauri za wilaya husika.
Alisema Shule ya Sekondari Ndwika ambayo iko Wilaya ya Masasi, inajengwa upya chini ya halmashauri baada ya taarifa ya wahandisi kubaini kuwa majengo yake hayawezi kufanyiwa ukarabati.
Pia shule za sekondari za Nyakato na Ihungo zitajengwa upya kufuatia kuharibiwa vibaya na tetemeko la ardhi lililotokea katika Mkoa wa Kagera Septemba, mwaka juzi.
“Vilevile Wizara kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania inakarabati shule za sekondari 17 ambazo ni Ilboru, Same, Pugu, Mwenge, Nganza, Mzumbe, Kilakala, Tabora Wavulana, Tabora Wasichana, Msalato, Dodoma, Ruvu, Korogwe, Bwiru Wasichana, Sengerema, Bihawana na Kondoa Wasichana,” alisema na kuongeza kuwa hadi sasa shule 10 zimeshakamilika na saba zitaanza kukarabatiwa hivi karibuni bila kuathiri masomo.
Aliongeza kuwa maelekezo ya Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako ni kuhakikisha kuwa wanafanya usimamizi wa karibu ili miradi yote ya TBA ianze kwenda kulingana na mikataba.
Akijitetea kuhusu kuchelewesha kwa miradi hiyo, Kaimu Meneja wa Mkoa TBA, Manasseh Shekalage, alisema hiyo inatokana na baadhi ya maeneo waliyogundua yanahitaji ukarabati zaidi.