24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

KINGUNGE AMWAMBIA MAGUFULI CCM NI CHAMA CHAKE

Rais Dk. John Magufuli akimjulia hali mwanasiasa mkongwe, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, anayetibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam jana baada ya kung’atwa na mbwa. PICHA IKULU
Na MWANDISHI WETU - Dar es Salaam

MWANASIASA mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, aliyelazwa Wodi ya Mwaisela katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni chake, hivyo hakiwezi kuwa kinyume na yeye kwa kuwa alishiriki kukiunda.

Kauli hiyo aliitoa jana mbele ya Rais Dk. John Magufuli aliyefika hospitalini hapo kumjulia hali.

“CCM ni chama changu, nimetoka nimekiacha, lakini nimefanya kazi zote, nimekiunda mimi, hakiwezi kuwa kinyume changu hata kidogo,” alisema.

Baada ya kuzungumza maneno hayo yaliyosikika katika video inayosambaa katika mitandao ya kijamii, Magufuli, alimjibu kuwa ameongea maneno muhimu.

“Asante sana, hayo maneno yako ni muhimu sana, kwamba CCM ni chama chako, hakiwezi kuwa kinyume chako, kwa hiyo wewe siku zote ni CCM ndani ya moyo wako. Mungu akubariki sana,” alisema Magufuli.

Awali, Bingwa wa Upasuaji wa MNH, Dk. Ibrahim Mkoma, alimweleza Rais Magufuli kuwa hali ya Kingunge inaendelea vizuri.

Pia Kingunge alimshukuru Magufuli kwa kumjulia hali na alimweleza kuwa anajisikia nafuu baada ya kupata matibabu.

Pamoja na kumpa pole na kumwombea apone haraka, Magufuli, alisema anatambua mchango mkubwa wa Kingunge katika siasa na maendeleo ya nchi.

Kingunge anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo baada ya kushambuliwa na mbwa nyumbani kwake Makumbusho, Dar es Salaam, siku chache zilizopita, huku ikiwa ni siku ya nne tangu mkewe Peras afariki dunia.

Jana asubuhi alipatiwa taarifa za kifo cha mke wake huyo na alisubiriwa apumzike ili baadaye atoe mwongozo wa nini kifanyike.

Akiwa hospitalini hapo, Rais Magufuli pia aliwajulia hali wagonjwa wengine wanaoendelea kutibiwa.

Katika Wodi ya Sewahaji, alimjulia hali Richard Kajumulo ambaye ni kaka wa Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka, Said Abeid Salim, Amina Shirwa, Hamad Lila na amempa pole Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk. Zainab Chaula, aliyefiwa na mama yake mzazi wakati akiwa wodini humo.

Pia aliwajulia hali mapacha walioungana; Maria na Consolata Mwakikuti waliolazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa matibabu ya moyo.

Maria na Consolata walimshukuru Magufuli kwenda kuwaona na kuwapa pole. Pia wameongoza sala ya kumwombea yeye na nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, alisema matibabu ya Maria na Consolata ambao ni wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Ruaha (RUCU) yanakwenda vizuri.

Profesa Janabi alisema taasisi hiyo imefanikiwa kutoa matibabu kwa wagonjwa wa moyo 14,000 katika mwaka uliopita na inashika nafasi ya tatu barani Afrika kwa utoaji wa huduma bora za matibabu hayo.

Katika hatua nyingine, Magufuli aliwashukuru na kuwapongeza madaktari wa MNH na JKCI kwa kazi kubwa wanayofanya kutibu wagonjwa na amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili ili kuboresha huduma zaidi.

“Nawashukuru madaktari na wafanyakazi wote, mnafanya kazi kubwa ya kuwatibu wagonjwa, pia mmeboresha hospitali na inaonekana ni safi, mimi niwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira yenu ya kazi ili muendelee kutoa huduma nzuri,” alisema Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles