RAMADHAN HASSAN-DODOMA
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, amesema kwa mwaka wa fedha 2020/21 Serikali imetenga Sh bilioni 228 kwa ujenzi wa maboma ya madarasa na zahanati ambapo alidai kwamba ana uhakika Serikali itatoa fedha.
Kauli hiyo aliitoa jana bungeni wakati akijibu hoja za wabunge waliohoji kuhusu umaliziwaji wa maboma ya zahanati, ujenzi wa shule na vituo vya afya.
“Mheshimiwa Naibu Spika tumetenga Sh bilioni 228 kwa mwaka wa fedha 2020-2021 na hizo tunaenda kuzitoa,” alisema Dk. Kijaji.
Alisema Serikali imetoa Sh bilioni 19.5 katika bajeti ya mwaka 2019/20 kukamilisha ujenzi wa nyumba za walimu 364 na zahanati 52.
Dk. Kijaji alisema Serikali ilitenga Sh bilioni 19.5 katika mwaka wa fedha 2019/20 kwa ujenzi wa nyumba 364 za walimu pamoja na zahanati 52.
Alisema kwamba fedha hizo Serikali imeishazitoa zote.
Dk. Kijaji alisema kwa mwaka wa fedha 2017-2018 Serikali ilitenga jumla ya Sh bilioni 38 kwa ujenzi vituo vya afya 96 ambapo alidai kwamba fedha hizo zote zilitolewa.