Susan Uhinga, Tanga
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Muhagama, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano pamoja na kuheshimiana ili kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Waziri Jenista ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 13, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya sherehe za kilele cha Mwenge wa Uhuru ambazo zinaambatana na kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere.
Amesema Sherehe hizo zitahudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ally Mohamed Shein na waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Watanzania wanatakiwa kuuenzi mwenge wa Uhuru kwa kutenda mambo muhimu aliyokuwa akiyafanya Mwalimu Nyerere.
“Mwenge wetu wa Uhuru ni wa kuuenzi kutokana na umuhimu wake wa kuendelea kutukumbusha umuhimu wa kutunza amani upendo na mshikamano wetu ambao ulianzishwa na muasisi na wa taifa,” amesema Waziri Jenista.
Sherehe za kilele cha mbio za mwenge wa uhuru Zitakazoambatana na Ibada maalumu ya kumuombea mwalimu Nyerere zitafanyika kesho jijini Tanga.