29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAFUTA HATI UWANJA WA YANGA

Mkwasa aukana

PATRICIA KIMELEMETA NA CHRISTINA GAULUHANGA

HATIMAYE, Rais Dk. John Magufuli amefuta hati ya umiliki wa shamba la ekari 715 lililopo eneo la Gezaulole, Kigamboni, linalojulikana kwa jina la Nafco, ambalo lilikuwa linamilikiwa na mfanyabiashara maarufu, Yusuph Manji.

Manji akiwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga kabla ya kuachia ngazi, Septemba 2016, alitoa sehemu ya shamba hilo kwa klabu hiyo na kuahidi kujenga uwanja wa  kisasa pamoja na kituo cha mazoezi baada ya siku tisini ikiwa wanachama wangempa ridhaa.

Mbali ya shamba hilo, pia serikali imefuta hati ya umiliki wa shamba lingine la ekari 5,400 la Kampuni ya Amadori.

Wakati akitoa shamba hilo, Manji alisema eneo hilo lilisajiliwa kwa  jina la kampuni ijulikanayo ‘Yanga Yetu’ na halikuwa na mgogoro wowote wa ardhi, kisha  alimkaribisha Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi.

Zoezi la uwekaji wa jiwe la msingi lilifanyika mbele ya mjumbe wa bodi ya wadhamini wa klabu hiyo, Mama Fatuma Karume, ambaye alijigamba  kuwa, kiwanja hicho kitakuwa sehemu ya machinjio ya watani wao wa jadi, timu ya Simba.

“Uwanja wa mazoezi utaanza kujengwa ndani ya siku tisini pindi wanachama wangeruhusu, na ujenzi wake hautachukua zaidi ya miezi nane.

“Nataka uwanja wa mpira na mazoezi ujengwe tofauti, natumaini wanachama wa Yanga watakubali ombi langu ili nianze ujenzi mapema,” alisema Manji, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi.

Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wapenzi, wanachama na mashabiki wa Yanga, jana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alitangaza kufuta umiliki wa  shamba hilo pamoja na lingine la ekari 5,400 linalomilikiwa na kampuni ya Amadori.

“Shamba la Nafco, ambalo linamilikiwa na Manji na lingine la kampuni ya Amadori lenye ekari 5,400, tumefutia hati ya umiliki na kulirudisha serikalini, ili yaweze kupangiwa matumizi mengine baadaye,” alisema Lukuvi.

Katika hatua nyingine, serikali imeivunja rasmi Wakala wa Uendelezaji wa Mji wa Kigamboni (KDA) na kuitaka kukabidhi majukumu yake kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni.

Alisema kuanzia sasa Manispaa ya Kigamboni itahusika kupanga na kusimamia ardhi yake kama manispaa nyingine zinavyofanya, na kwamba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaendelea kusimamia masuala yote yanayohusu ardhi kwa ujumla wake.

Lukuvi aliongeza kuwa, kuanzia sasa wakazi wa mji wa Kigamboni wasizuiwe kupewa hati  za umiliki wa ardhi pamoja  na  vibali vya ujenzi.

 

 

 

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alipoulizwa anachukuliaje uamuzi huo wa serikali, alisema hawezi kulizungumzia kwa kina suala hilo, kwavile hakuwahi kukabidhiwa rasmi mpango wa uendelezaji wa uwanja huo.

“Kwa sasa plani tuliyonayo ni kuuboresha uwanja wetu wa Kaunda na tayari tumeanza kumwaga vifusi, huo mwingine unaosema siwezi kuuzungumzia kwavile sikuwahi kukabidhiwa rasmi mpango wa uendelezaji wake kwa maana na bajeti,” alisema Mkwasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles